Nyota wa Manchester United, Robin van Persie atakuwa nje ya dimba kwa kati ya wiki nne hadi sita baada ya kuthibitishwa na madaktari kwamba alipata jeraha kubwa la goti kwenye mechi baina ya United na Olympiakos Jumatano iliyopita.
RVP (30) alifunga mabao yote matatu katika mechi dhidi ya Wagiriki na kuwavusha United kwenye robo fainali watakayocheza Aprili mosi au pili na kurudiwa wiki moja baadaye dhidi ya Bayern Munich.
Mdachi huyo alitolewa nje kwa machela dakika za mwisho za mechi hiyo muhimu, kwani Kocha David Moyes anapimwa kwa matokeo ya mechi tatu – hiyo ya Olympiakos, ya Jumamosi hii dhidi ya West Ham United na dhidi ya watani wao jirani, Manchester City.
RVP msimu huu haujamwendea vizuri ikilinganishwa na miwili iliyopita ambapo alikuwa mfungaji bora mfululizo. Hadi sasa amefunga mabao 17 katika mechi 25 alizochezea United na ameshakuwa nje ya dimba kati ya Desemba na Januari msimu huu kwa majeraha ya paja.
Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal hakuwapo katika mechi zote za Kombe la FA na Capital One, wakati ambapo United walipoteza mechi nne kati ya tano walizocheza. United wanashika nafasi ya saba na wapo katika wakati mgumu wa kumaliza nafasi nne za juu.