Menu
in ,

Robin Van Persie atua Manchester United

Na: Israel Saria
*Fungate la miaka nane la RVP na Arsenal laisha

Hatimaye sakata la Robin van Persie limehitimishwa kwa Arsenal kukubali kumuuza kwa Manchester United.
Licha ya kuichezea Arsenal dhidi ya Cologne nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki iliyopita, Mholanzi huyo alisimamia uamuzi wa kutoongeza mkataba.
RVP alikuwa anawaniwa pia na Manchester City na Juventus ya Italia, lakini baadaye klabu mbili hizo zilionekana kujing’atua pembeni na kuwaachia nafasi Man U.
Makubaliano yaliyofikiwa ni kwa nahodha huyo wa msimu uliopita kuuzwa kwa kitita cha Pauni milioni 24, dau ambalo awali Man U waliliona kubwa.

Tabasamu sasa ni kubwa kwa Mashetani Wekundu hao, na wanaweza kumwanzisha RVP kwenye mechi yao ya kwanza ya ligi Jumamosi hii dhidi ya Everton itakayokuwa ugenini.
Makubaliano hayo yanamaliza mvutano wa muda mrefu kati ya klabu mbalimbali, kocha Arsene Wenger akimshawishi mchezaji huyo bora wa mwaka abaki, huku tetesi zikiwa nyingi na tofauti.
Imeelezwa kwamba sasa kilichobaki ni kwa RVP mwenyewe kukubaliana na maslahi aliyopangiwa, kukamilisha vipimo vya afya, lakini ilivyo ni kwamba kikwazo kikubwa kimeshavukwa.
RVP alikuwa amebakisha mwaka mmoja tu katika mkataba wake na Washika Bunduki hao wa London, na iwapo hangeuzwa, angehama bure mwishoni mwa msimu.
Van Persie anatarajiwa ataingia mkataba wa miaka minne na klabu hiyo inayonolewa na Sir Alex Ferguson. Ataunganisha nguvu na Wayne Rooney kwenye mashambulizi.
Wawili hao watakuwa tishio kwa wapinzani wa United uwanjani, kwani walishika nafasi ya kwanza na ya pili kwa ufungaji bora, wakiwa na mabao 57 jumla. RVP alikuwa na mabao 30 katika ligi.
Pengine hilo ndilo jambo lililokuwa likiwasukuma Arsenal wamng’ang’anie, lakini ndiyo hivyo, fungate la RVP na Arsenal limefikia tamati baada ya miaka  minane.
Arsenal walifanya kila lililo ndani ya uwezo wao kumshawishi aendelee kubaki, lakini amefuata nyayo za wenzake, akina Cesc Fabregas, Samir Nasri, Emmanuel Adebayor, Patrick Viera na wengine.
Hata hivyo, Van Persie anaondoka mashabiki wengi wakiwa wamechoshwa au kukinaishwa naye, kutokana na jinsi alivyoandika kwenye tovuti yake akibeza mipango ya baadaye ya klabu, akidai ndio msingi wa kutopenda kuongeza mkataba Emirates.
Anaondoka wakati pengo lake linaonekana lilishazibwa. Wapo wachezaji wapya aina ya Olivier Giroud, Lukas Podolski na Santi Cazorla.
Pamekuwa na tetesi pia kwamba RVP anakimbia ushindani kwa wachezaji wapya wanaoingia Arsenal na kwamba si kweli alikuwa anahofu hakuna mipango thabiti ya kukisuka kikosi na kutafuta mataji kama alivyodai.
Kunyakuliwa kwa RVP na United kunawaacha majirani zao – City katika ukiwa, kwa sababu ni majuzi tu kocha wao, Roberto Mancini alieleza kusikitishwa kwake na jinsi usajili usivyoshika kasi Etihad.
Uhamisho huu ndio dau kubwa zaidi United walilotoa baada ya lile la Dimitar Bebatov mwaka 2008 kutoka Tottenham, ambapo iliwatoka Pauni milioni 30.75.
Makubaliano hayo pia yamefikiwa wakati pakiwa na maswali mengi kuhusu kitita alichotengewa Ferguson kwa ajili ya usajili msimu huu.
Licha ya Rooney, Ferguson anajivunia  nyota Danny Welbeck na Javier Hernandez, huku pakiwa na tetesi kwamba Berbatov ataondoka Old Trafford.
Madau ya awali ya Manchester United na Juventus yalikataliwa na Arsenal, kwa maelezo kwamba yalikuwa madogo. Juventus walionekana kuwa na ari zaidi, lakini baadaye wakasita, huku Man U nao wakikaa kimya, wengi wakadhani hawatakubali kuongeza dau.
Wakati mpango huo ukielekea kufa kifo cha kawaida kwa Arsenal kumlinda mtu wao, inadaiwa Ferguson alikutana na Wenger na kuzungumza naye moja kwa moja kabla ya safari ya timu nchini Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya.
Wenger hakutaka kumuuuza nyota wake kwa klabu hasimu kama Man U, lakini hatajilaumu kwa vile mashabiki hawamtaki RVP tena, na hata nchini Ujerumani alizomewa.
RVP alizaliwa jijini Rotterdam Agosti 6, 1983 na alianza kuichezea klabu ya Feyenoord ya Uholanzi mwaka 2002. Wenger alimtwaa kwa ajili ya Arsenal kumnyakua 2004 na kumkuza hadi alipofika.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version