*Wadau wasema ni msiba usio na kilio
*Atinga Qatar kuchambua mechi ya leo
Unaweza kusema ni kifo na msiba wa kujitakia kwa mwanasoka wa Manchester United, Rio Ferdinand aliyekataa kuchezea timu ya taifa ya England.
Wengi waliungana naye kumshutumu kocha Roy Hodgson alipoacha kumwita kwenye timu mwaka jana, na Ferdinand mwenyewe akasema aliumizwa.
Lakini miezi michache baadaye, kocha huyo huyo amemwita mchezaji yule yule, akakataa na kukusanya visababu visivyo na kichwa wala miguu.
Wakati England leo wakicheza na San Marino kisha Jumanne dhidi ya Montenegro, Ferdinand amedai yupo kwenye ratiba ngumu ya matibabu.
Beki huyo wa kati alitangaza kujitoa baada ya kocha wa Man United, Alex Ferguson kueleza kushangazwa na kuitwa kwake timu ya taifa wakati ana idadi ya mechi anazotakiwa acheze na kuendelea na matibabu.
Kujitoa huko kulionekana pigo kwa England, kutokana na ukweli kwamba alikuwa anachukuliwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza ulinzi kutokana na uzoefu wake na pia kuna wengine wanaomudu nafasi hiyo ni majeruhi.
Hata hivyo, kocha Hodgson anasema licha ya kusikitishwa na Ferdinand kujitoa, anakiamini kikosi chake.
Alighadhabishwa na uamuzi wa Ferdinand, hasa baada ya kubainika kwamba ataendelea kuchezea Manchester United mechi zijazo na jana alikwea pipa kwenda Qatar, ambapo atakuwa mchambuzi kwenye mechi hiyo hiyo ya England dhidi ya San Marino.
“Hakuna tabu, kwa hiyo yeye sasa anajishughulisha na klabu yake na shughuli binafsi,” akasema Hodgson kwa huzuni, na alipoulizwa iwapo ndio mwisho wa Ferdinand kimataifa, alisema ni suala la kusubiri tu na kuona.
Ferdinand anayesema ana matatizo ya mgongo ameshambuliwa na vyombo vya habari vya England, magazeti mengi yakisema ni kifo kilichofuatiwa na maziko yasiyo na waombolezaji.
Nahodha wa England, Steven Gerrard anayechezea Liverpool, amesema kamwe hatakaa akose uzalendo kwa taifa lake.
Ferdinand anadai kwamba kazi anayoifanya sasa ni ya kawaida na amekuwa akifanya hivyo siku zilizopita, na kuwa hata asingeifanya lazima angefuatilia mechi hiyo kwenye televisheni.
Wachambuzi wa masuala ya afya na michezo wamedai muda wote wa kuruka na ndege hadi Qatar na kurudi utazidisha maumivu yake ya mgongo, na kwamba afadhali angekubali kuchezea nchi yake.
Alipoachwa kwenye mechi za UEFA, wanahabari walitumia muda mwingi wa vikao vya kocha Hodgson kumuuliza kwa nini alimwacha Ferdinand na kama timu haingeathirika.
Ferdinand amekuwa akitamba kwenye mitandao ya jamii ya Facebook na Twitter, na alizidi wakati akimtetea mdogo wake dhidi ya Terry.
Alifika mahali pa kumwita Ashley Cole (mweusi) wa Chelsea aliyemtetea Terry kwenye kesi hiyo kuwa ni sawa na ice cream yenye rangi nyeupe juu na nyeusi ndani.
Kujitoa kwa Ferdinand kunamwacha Hodgson na mabeki wanne wa kati – Joleon Lescott (Manchester City), Chris Smalling (Man United), Steven Taylor (Newcastle United) na Steven Caulker wa Tottenham Hotspurs ambaye hajapata kuchezea timu ya taifa hata mara moja.
Ferdinand amejitoa kwa sababu zake, huku Michael Dawson wa Spurs na Gary Cahil wa Chelsea ambao wangeweza kucheza nafasi yake ni majeruhi.