MACHO na masikio ya wengi yanaanza kuelekezwa nchini Morocco, kila mdau na shabiki anatamani kuona nchi yake anayoshabikia au ya kuzaliwa inakwenda kufanya vizuri kwenye mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON. Michuano ijayo inatarajiwa kufanyika nchini Morocco ambako wenyeji wamefuzu moja kwa moja kwenye mashindano hayo, huku wakiungana na mataifa mengine yaliyofanikiwa kupenya.
Tathmini iliyofanywa TANZANIASPORTS inaonesha kuwa zipo kanda ambazo timu zao pendwa hazijafuzu na zingine zimefuzu kwa mbinde, pamoja na zile zilizofuzu kwa shangwe kubwa. Je kanda hizo zimefanya nini?
Afrika Mashariki wamerudi walewale
Ukanda huu umeonesha ushindani mkubwa na kurudisha mataifa yaleyale yaliyofuzu katika fainali za mwaka 2023 ingawaje Taifa moja limeongezeka. Katika fainali za AFCON 2025 ukanda wa Afrika mashariki unatarajiwa kuwakilishwa na Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika fainali zilizopita DRC na Tanzania zilipangwa kundi moja. Kwa sasa Uganda linakuwa taifa la tatu kuwakilisha ukanda wa Afrika mashariki, ambapo DRC inaingia kama mwanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki ya kisiasa. Lakini kama inatazamwa uanachama wa CECAFA basi kuna wanachama wawili hai Tanzania na Uganda ndiyo wamefuzu fainali hizo huku majirani zao Kenya wakishindwa kufurukuta kabisa.
Miamba ya Ukanda wa kusini wa COSAFA
Hakuna ubishi kuwa soka katika ukanda wa kusini mwa afrika linazidi kuchanja mbuga. Matiafa mengi kutoka ukanda wa kusini mwa Afrika yamefanikiwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika hapo mwakani nchini Morocco. Mathalani Chama cha Soka cha Nchi za Kuisni mwa Afrika (COSAFA) kimeweka rekodi ya aina yake baada ya baadhi ya wanachama wake kutinga katika fainali hizo.
COSAFA wameweka rekodi kuwa na wanachama wengi waliofuzu mashindano ya AFCON kuliko ukanda wowote. COSAFA wamezishinda kanda ya magharibi, kanda ya afrika ya kati, Kanda ya Afrika Kaskazini na kanda ya Afrika Mashariki. Katika ukanda wa COSAFA nchi zilizofuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2025 ni pamoja na Angola,Botswana,Comoro,Msumbiji,Afrika kusini,Zambia na Zimbabwe. Jumla ya Mataifa 7 kutoka COSAFA yamefuzu fainali hizo. Gumzo limekuwa kubwa kutokana na ushiriki wa wanachama wengi wa COSAFA na kudhihirisha kuwa soka la ukanda huo limepiga hatua kubwa.
Ukanda wa WAFU
Miongoni mwa mambo ya kusikitisha ni kukosekana kwa Ghana katika fainali zijazo za AFCON. Kwenye fainali hizo nchi ya Ghana haitashiriki kwa sababu imeshindwa kufuzu licha ya kuwa na maelfu ya wachezaji wanaosakata soka barani Ulaya na kwingineko. Ghana watawashuhudia washindani wao Senegal,Gambia,Nigeria kwa kutaja chache zikiwa miongoni mwa nchi zitakatimua vumbi kwenye fainali hizo.
Kitendo cha kuongezeka timu toka COSAFA kinamaanisha idadi ya nchi za afrika maagharibi na wanachama wa chama soka cha WAFU wameshindwa kufua dafu mbele ya washindani wa kusini mwa Afrika. Kwa kawaida mashindano ya AFCON tangu yakiitwa CAN yalikuwa yanatawaliwa zaidi na washiriki kutoka Afrika magharibi, lakini hali ya mambo imebadilika.
Afrika kaskazini
Ukanda huo ulikuwa unatawala kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa Afrika magharibi. Lakini kuruhusu wanachama 7 wa COSAFA kufuzu AFCON 2025 ni dhahiri hali ya mambo katika ukanda huo si shwari. Morocco, Algeria,Tunisia ni miongoni mwa mataifa yenye historia nzuri kwenye mashindano ya CAF.
Lakini kadiri miaka inavyokwenda ngazi ya vilabu wamekumbana na hali ngumu na kuwalazimu kuajiri hadi makocha wanaotoka ukanda wa COSAFA pamoja na kusajili vipaji kutoka kusini kwa Jangwa la Sahara ambapo miaka nyuma wengi walikwenda kufanyiwa majaribio kwanza kabla ya kununuliwa., hali ya mambo imebadilika na sasa vipaji toka kusini mwa jangwa la sahari wananunuliwa moja kwa moja na kudhihirisha ukame wa vipaji na ushindani kutoka ukanda huo. Pengine COSAFA wamebisha hodi kwenye soka la Kimataifa.
Afrika ya Kati ukimya mwingi
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kijiografia inapatikana pia ukanda wa Afrika ya kati. Nchi hiyo ndiyo kinara wa mashindano wa AFCON. Hata hivyo ukanda huu nao unaonekana kukosa maarifa kama ya wanachama wa COSAFA ambao wamefanikiwa kufuzu kwa mkupuo tofauti na zamani. Ukanda wa Afrika ya Kati hauna rekodi ya kutisha lakini kwenye mchezo wa soka kila kitu kinawezekana kwa wakati. Ni dhahiri wanachama wa COSAFA watatuma ujumbe mzito kwenda Afrika ya kati kutokana na kufuzu kwa wingi.