*Lewandowski wa Dortmund apiga manne
Mambo yamewaendea kombo Hispania katika mechi za nusu fainali za kwanza, baada ya Real Madrid kufuata nyayo za Barcelona kwa kukandikwa mabao manne.
Katika mechi iliyopigwa jijini Dortmund Jumatano hii usiku, Borrusia Dortmund waliwapa wakati mgumu vijana wa Jose Mourinho kwa kuwapeleka mchakamchaka tangu mwanzo wa mechi na kuishia kwa ushindi wa 4-1.
Barca waliofungwa 4-0 na Bayern Munich jijini Munich, wanabidi kutafuta suluhu sawa na Real kwa ajili ya mechi za marudiano wiki ijayo, vinginevyo itakuwa fainali ya timu za Ujerumani pekee.
mchezaji anayewaniwa na klabu kubwa za Ulaya, Mpoland Robert Lewandowski ndiye aliyewaua Real, kwa kupachika mabao dakika ya nane, 50, 55 na la 66 kwa penati wakati Real walijiliwaza kwa bao la kusawazisha mapema dakika ya 43 kupitia nyota wao tegemeo, Cristiano Ronaldo.
Baada ya kupata bao la kwanza, Dortmund walijisahau, ndipo Real wakatumia fursa hiyo, japokuwa palikuwa na malalamiko ya hapa na pale kutoka Dortmund juu ya faulo walizochezewa bila kupewa mipira ya adhabu, ikiwamo penati muda mfupi kabla Ronaldo hajasawazisha.
Lewandowski anakuwa mchezaji wa kwanza kuwafunga Real zaidi ya mabao mawili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, na Jumatano hii alionekana kuwa fiti, na kama si uhodari wa golikipa Diego Lopez, angeweza kuwa amefunga mabao sita, kwani Lopez alipangua mawili ya wazi yaliyokuwa yakikaribia kutikisa nyavu karibu na mtambaa wa panya.
Real Madrid walitawala sehemu ya mwisho ya kipindi cha pili, lakini jitihada za kupata bao muhimu la pili zilikwama, hivyo kuishia kwa kipigo hicho, warudi Madrid kujiweka sawa kwa mechi ya marudiano, ambapo itabidi washinde walau 3-0 ili kuvuka kwa faida ya bao la ugenini.