BAADA ya kuukosa ubingwa kwa miaka mitatu, hatimaye Real Madrid wamewavua ubingwa Barcelona, ikiwa imebaki raundi moja ya mechi za Ligi Kuu ya Hispania – La Liga.
Mabingwa hao wapya wa Hispania walitawazwa jana Alhamisi kwenye uwanja wao wa mazoezi wa Valdebebas jijini Madrid, baada ya kuwafunga Villareal 2-1 huku mahasimu wao Barcelona wakifungwa na Osasuna.
Zinedine Zidane alisema kwamba ubingwa huo umeifanya siku ya jana kuwa ya kipekee, kwamba alikuwa mwenye furaha na kombe hilo limekuwa muhimu hata kuliko wangechukua ubingwa wa Ulaya.
Kocha huyo Mfaransa alisema tangu awali kwamba lengo lao kubwa msimu huu lingekuwa ni kuurejesha ubingwa Santiago Bernabe na kwamba ni muhimu hata kuliko Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), na sasa pamoja na wachezaji wake wamefanikisha hilo.
Mashujaa walikuwa wale wale – Karim Benzema aliyefunga mabao mawili na nahodha Sergio Ramos aliyekuwa imara kwenye beki ya kati, uongozi kwa ujumla na pia ndiye alikuwa akienda kufunga bao la pili akaangushwa na kuzaa penati aliyompa Benzema apige.
Kwa ushindi huo hakuna timu inayoweza kuwafikia. Huu ni ubingwa wa 34, nane zaidi ya Barca na ni ubingwa wa tatu katika miaka 12, wakiwa wamepata zaidi ubingwa wa Ulaya kuliko wa nyumbani katika muongo mmoja.
Wamevunja utawala wa Barcelona kushikilia ubingwa, huku mahasimu hao wa Katalunya wakiwa katika mzozo kuanzia kwenye bodi ya wakurugenzi hadi kwenye timu. Nahodha wao, Lionel Messi alijawa hasira kwenye mechi yao ya Alhamisi dhidi ya Osasuna, akiwalaumu wachezaji wenzake kwa udhaifu walioonesha.
Zidane amefanya makubwa Real Madrid, akitwaa ubingwa wa UCL mara tatu mfululizo kabla ya kuondoka kwenye klabu ghafla mwishoni mwa msimu, kisha akaombwa na Rais Florentino Perez, na kurejea katikati ya msimu uliofuata.
Hawakutarajia kukabidhiwa kombe hilo mbele ya watu pungufu ya 300 katika uwanja wao wa mazoezi, lakini imebidi hivyo kwa sababu za hadhari ya kusambaa kwa virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu; Covid-19.
Wala hawatakuwa na shamrashamra za kuzunguka na basi lao kubwa la wazi hadi Cibeles kujumuika na washabiki wao, kwa sababu hizo hizo za virusi vya corona.
“Ligi ya Mabingwa Ulaya ni Ligi ya Mabingwa, lakini La Liga hunifanya kuwa mwenye furaha zaidi, kwa sababu La Liga ndio mpango mzima. Ni hisia za aina yake kwa sababu kile wachezaji hawa walichofanya ni kikubwa sana, sina maneno zaidi ya kusema kwa sababu ya mhemko,” akasema mchezaji huyo wa zamani wa Real.
Los Blancos hao wameshinda mechi 10 mfululizo za La Liga tangu ligi iliporudia Juni baada ya kuwa imesimamishwa Machi mwaka huu kupisha hatua za kupambana na virusi vya corona. Upande wa pili, Barcelona walikuwa wachovu, ambapo mpira wa adhabu ndogo uliochongwa na Messi ulikuwa ndio pekee tishio.
“Hatukutarajia kabisa kumalizia jinsi hii, lakini huu ndio ufupisho wa mwaka kwetu. Tumekuwa timu dhaifu tunaoweza kufungwa na timu yenye nguvu na tamaa ya kufanya hivyo. Tumepoteza alama nyingi ambazo hatukutakiwa na tumekosa uendelevu mzuri. Tunatakiwa kujikosoa, kuanzia kwa wachezaji lakini pia kwa klabu yote. Sie ni Barcelona na tunatakiwa kushinda kila mechi,” Messi akaiambia televisheni ya Hispania akijawa hasira.
Sijui kama nitainoa Barcelona katika Ligi ya Mabingwa:-
Barcelona, Hispania. Kocha wa FC Barcelona, Quique Setien ameingiwa na hofu ya kibarua chake huko Camp Nou baada ya kikosi chake kushindwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga’.
Baada ya hapo jana, Barcelona kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Osasuna, Setien alisema hajui kama ataendelea kuinoa timu hiyo hasa wakati ambao Ligi ya Mabingwa Ulaya itakaporejea mwezi, Agosti.
“Ningependa kuendelea kuifundisha Barcelona lakini sina uhakika kuwa nitaendelea kuwa hapa,” alisema kocha huyo.
Lionel Messi alipoulizwa kuhusu kiwango chao mwaka huu baada ya kipigo kutoka kwa Barcelona, anaamini wamewafanya wapinzani wao kutwaa kirahisi Ligi hiyo.
Kuhusu kauli ya Messi, Setien alisema anaelewa hali ambayo anapitia kwa sasa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina kutokana na kushindwa kwao kuutetea ubingwa huo.
“Nakubaliana na Messi, tunapaswa kujikosoa tulichofanya kilikuwa tofauti na tulichopaswa, tusipofanya hivyo itatugharimu zaidi,” alisema.
Real Madrid wametwaa ubingwa wa La Liga kwa mara ya 34 huku wapinzani wao, Barcelona wakiwa wamebeba mara 26, wameachwa kwa makombe nane katika Ligi hiyo.
In Summary: Barcelona wamepoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wa La Liga kwa mara ya tatu mfululizo baada ya usiku wa jana, Real Madrid kuishushia kipigo cha mabao 2-1 Villarreal.