Ulimwengu wa soka umepokea kwa masononeko uamuzi wa wamiliki wa Leicester kumfukuza kazi kocha Claudio Ranieri.
Ametemwa siku 298 tu tangu alipowapatia ubingwa kwa mara ya kwanza kwenye historia ya klabu hiyo, zaidi ya miaka 100 iliyopita.
Ranieri amefukuzwa timu ikiwa pointi moja na nafasi moja tu juu ya nafasi ya kushuka daraja huku mechi 13 zikiwa zimebaki. Taarifa ya Leicester inasema bodi imechukua uamuzi huo kwa masikitiko lakini hapakuwa na la kufanya.
Amefukuzwa pungufu ya saa 24 tangu watoke Hispania walikofungwa 2-1 na Sevilla kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwenye mechi ya mkondo wa kwanza katika 16 bora.
Foxes walitwaa ubingwa wa England msimu uliopita ambao wanashindwa kuutetea sasa, wakati ule wakimaliza ligi wakiwa pointi 10 mbele ya washindani wao wa karibu na si ajabu wakashuka daraja sasa; itakuwa ni mara ya kwanza bingwa mtetezi kushuka daraja tangu 1938.
Wamepoteza mechi zao tano za Ligi Kuu ya England (EPL) zilizopita na ni wao pekee katika ligi nne za juu England wasiokuwa na bao lolote mwaka 2017.
Kura ya maoni iliyoendeshwa na kuchapishwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) inaonesha kwamba asilimia 13 tu ya waliohojiwa wanaona ilikuwa sawa kwa Ranieri kufukuzwa wakati asilimia 87 wanasema haikuwa sawa.
Mchambuzi wa masuala ya soka na mchezaji wa zamani wa Leicester, Gary Lineker anasema kwamba alidondosha machozi alipopata habari za kufukuzwa kwa Ranieri ambaye amekuwa akijiita Tinkerman.
Mapema mwezi huu wa Februari, wamiliki wa Leicester walieleza kwamba walikuwa bado wanamuunga mkono kocha wao huyo bila kuyumba na wangeendelea naye, lakini sasa wanasema hadhi ya klabu inaporomoka hivyo wamelazimika kubadili uongozi.
Makocha kadhaa wanatajwa kuweza kuchukua nafasi hiyo, akiwamo Mtaliano mwenzake, Roberto Mancini aliyepata kuwafundisha Manchester City, Guud Hiddink, Michael O’Neill na Paul O’Neill.