Menu
in , , ,

Rais wa Fifa Februari 26

*Kikosi kazi cha mageuzi chaundwa

*Blatter atupiwa noti feki za dola

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa) limepanga kufanya uchaguzi wa rais atakayechukua nafasi ya Sepp Blatter Februari 26, huku likiunda kikosi kazi kwa ajili ya kuweka upya mfumo wa shirikisho hilo lililozongwa na tuhuma za rushwa.

Blatter aliyechaguliwa majuzi ameamua kung’oka mapema kupisha wengine, baada ya kubaini kwamba haungwi mkono na ulimwengu wa soka, licha ya kupitishwa na wajumbe wa mashirikisho ya soka walio wengi.

Pamoja na mambo mengine, kikosi kazi kinachoundwa na watu 11 kitashughulikia mpango wa kuwapo ukomo wa uongozi kwa rais na pia uchunguzi kuhakikisha wanaoongoza Fifa ni watu waadilifu, Blatter mwenyewe ametangaza.

Blatter (79) anaachia ngazi huku maofisa wake waandamizi saba na wengine wa zamani wakiwa na kesi ya jinai inayowahusisha na rushwa, wizi wa fedha na utakatishaji fedha nchini Marekani. Walidakwa muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu wa Fifa uliomchagua Mswisi huyo.

Uswisi yenyewe imeanzisha upelelezi juu ya mienendo ya rushwa ndani ya shirikisho hilo, ambapo nyaraka kadhaa zilicotwa kwenye ofisi za watendaji wake. Baadhi ya madai ya rushwa ni juu ya uteuzi wa Urusi na Qatar kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022.

Kadhalika yamekuwapo madai kwamba Afrika Kusini walitoa hongo ili kufanikisha kuwa wenyeji wa kwanza barani Afrika wa fainali hizo, 2010 na pia maofisa wa Fifa wamekuwa wakipenyeza rushwa ili kuepuka kesi au mivutano mbalimbali.

Inaelezwa kwamba wakuu wa mashirikisho kadhaa ya soka kwa mataifa na mabara wamemtaka Kiongozi wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini awanie nafasi hiyo ili airejeshe soka kwenye hadhi yake.

Pamoja na kwamba Blatter alitangaza kuachia ngazi tangu Juni 2 mwaka huu, siku nne tu baada ya uchaguzi uliomweka madarakani, atabakia kwenye kiti chake akifanyakazi kwa miezi tisa zaidi.

Mgombea aliyeshindwa kumng’oa kwenye uchaguzi huo, Prince Ali bin al-Hussein Jumatatu hii alimtaka Blatter aondoke madarakani mara moja ili mambo yasizidi kwenda mrama, akisema urais huo hauwezi kuendelea tena.

Pesa bandia ukumbini
Pesa bandia ukumbini

Katika tukio la ajabu Jumatatu hii, msanii wa vichekesho wa Uingereza, Lee Nelson alivamia mkutano wa Blatter na wanahabari, akasogelea pale Blatter alipokuwa amekaa na kujaribu kumkabidhi kitita cha noti za dola feki za Marekani.

Msanii huyo ambaye jinale halisi ni Simon Brodkin alimwambia Blatter: “Sepp, hizi (fedha zile feki) ni kwa ajili ya Korea Kaskazini 2026 (akimaanisha rushwa ili fainali za Kombe la Dunia 2026 zifanyike Korea Kusini).”

Ilibidi Blatter kuwaita walinzi wa Fifa kwa ajili ya kuingilia kati kumwondosha Nelson, lakini kabla ya kufanya hivyo alimmwagia Blatter noti hizo zikimpeperukia kichwani na kumzunguka huku Blatter akionesha kukasirishwa na kitendo hicho.

Blatter alinyanyuka kuondoka ukumbini na akapata salamu ya mwisho kutoka kwa Nelson aliyemwambia: “Cheers, Sepp – zote (fedha) ziko hapo. Baada ya hapo wahusika waliziondoa noti hizo feki kisha baada ya dakika 10 Blatter akarejea kuendesha mkutano wake.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version