*Shabiki apiga polisi kumtafuta Ferguson
Homa ya soka inaendelea kuzitesa nchi za Hispania na Uingereza, ambapo Rais wa Klabu ya Barcelona, Sandro Rosell ameachia ngazi huku mashabiki wa Manchester United wakiweweseka.
Rosell amejiuzulu baada ya kukumbwa na kashfa ya usajili wa mshambuliaji kinda kutoka Santos ya Brazil, Neymar, ambapo inadaiwa alidanganya juu ya bei yake.
Rais huyo alishitakiwa na mwanachama wa klabu hiyo mahakamani kwa madai kwamba bei aliyonunuliwa mchezaji huyo si ambayo ilitangazwa na kwamba rais ni mfujaji wa fedha zao.
Uamuzi huo pia unakuja wakati Mahakama ya Hispania ikianza uchunguzi wake juu ya mauzo na manunuzi ya Neymar na madai kwamba amefuja pauni milioni 48.6.
Hata hivyo, Rosell anasema kwamba kila kitu kilifanyika kwa usahihi na yupo tayari kutoa ushahidi na ufafanuzi mbele ya jaji.
Uongozi wa juu wa Barca sasa unashikwa na Makamu wa Rais, Josep Maria Bartomeu na haijulikani kama mabadiliko hayo yatawaathiri Barca wanaoongoza ligi lakini wakiwa wamekabwa koo na Atletico Madrid na Real Madrid.
SHABIKI AITA POLISI KUMTAFUTA FERGUSON
Msimu mbaya wa Manchester United umeshuhudia shabiki wa klabu hiyo akipiga simu polisi (999) akimtafuta kocha aliyeachia ngazi mwaka jana, Sir Alex Ferguson.
Shabiki huyo ambaye alikuwa amelewa lakini alifikisha ujumbe unaoaminiwa kuwa wa wengi, alitaka Fergie arudi Old Trafford kuchukua nafasi ya Mskochi aliyemwachia kiti, David Moyes ambaye maji yanaelekea kumfika shingoni.
Shabiki huyo alipiga simu Kituo cha Polisi cha Greater Manchester usiku wa saa 4.30 Jumatano akilalamikia matokeo ya Mashetani Wekundu kufungwa na Sunderland na kutolewa kwenye Kombe la Ligi.
Polisi wa Manchester wamesema ni kweli kwamba inatia uchungu na kuleta msongo wa mawazo timu unayoipenda inapofungwa lakini wakakumbusha kwamba namba ‘999’ inatakiwa kupigwa kwa ajili ya masuala ya dharura tu.
Hapakuwa na dharura yoyote kwa United kufungwa, kwa sababu ilishafungwa zaidi ya mechi nne hapo Old Trafford na mwelekeo wao ulikuwa si mzuri, lakini hata kama ingekuwa ghafla polisi hawahusiki.
Man U walifungwa 2-1 kwa penati na hao Black Cats baada ya matokeo ya mechi zao mbili kwenda 3-3 na penati nyingi kukoswa na wachezaji wanaochukuliwa kuwa mahiri kwenye mchezo huo mkali.
Jamaa aliyepiga simu polisi aliulizwa iwapo alitaka kuripoti tukio la jinai naye akasema ndiyo, ila akaongeza kwamba alitaka kuzungumza na Fergie.
“Ndio. Nataka kuripoti tukio la jinai, na jinai yenyewe ni kwamba Manchester United wamepigwa, walikuwa hovyo kabisa, matokeo haya siyo, walipewa muda wa ziada na kwa kweli huu ni upuuzi na uchafu mtupu, je, Polisi mnaweza kutusaidia kumrudisha Ferguson?”