RAIS wa Simba, Ismail Aden Rage amevunja ukimya na kueleza kuwa amelazimika kumwandikia barua Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi kumwomba aruhusu mchakato wa uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uendelee.
Jumapili iliyopita Malinzi alitangaza kusimamisha uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliopangwa kufanyika Juni 29 mwaka huu hadi pale klabu hiyo kongwe nchini itakapounda kamati ya maadili.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari ya Bunge mjini hapa jana mchana, Rage alisema amelazimika kumwandikia barua Malinzi ili kuinusuru klabu hiyo iliyokubwana migogoro kwa takriban miaka miwili sasa.
“Juni 15 mwaka huu (Jumapili) majira ya saa 1:30 usiku nilipokea barua kutoka kwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi akinitaka utekelezaji wa mambo matatu; kwanza kuunda kamati ya maadili, kusimamisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa Simba na mwisho kuhakikisha maagizo hayo yawe yamekamilika kufikia Juni 30 mwaka huu,” alisema Rage.
Alisema amelazimika kumlima barua Malinzi kwa kuwa maamuzi ya kusitisha mchakato wa uchaguzi huo kutakuwa na madhara makubwa kwa klabu ya Simba msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa vile kutaathiri zoezi la usajili.
“Klabu ya Simba ni muhimu sana katika maisha yangu, nimeichezea na kuitumikia kama katibu mkuu 1982 na nimeingia katika kumbukumbu muhimu kwa kuwa Rais wa kwanza wa klabu hii,” alisema Rage na kuongeza:
“Kwa kutambua hilo, leo (jana) nimemwandikia barua Malinzi kumwomba asisitishe uchaguzi wetu, aache ufanyike Juni 29 kama iilivyopangwa. Ninatambua anayo mamlaka ya kuweza kuuchelewesha.
“Usajili umeanza tangu Juni 15 mwaka huu, kusitisha uchaguzi ni kutoitendea haki klabu ya Simba kwa sababu mimi na uongozi wote unaomaliza muda wake tumezuia usajili hadi pale viongozi wapya watakapopatikana,” alisema zaidi Rage.
Kuhusu kuunda kamati ya maadili, Rage alisema masuala mengi ya kimaadili yanayowakabili baadhi ya wagombea akiwamo Michael Wambura aliyeenguliwa katika kinyang’anyiro cha Urais, yako juu ya uwezo wa klabu ya Simba, hivyo anayarudisha TFF.
“Ukiangalia masuala mengi ya kimaadili ambayo Rais wa TFF ametaka yaundiwe kamati ya maadili ya klabu ili yasikilizwe yako juu ya uwezo wa Simba,” alisema Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM).
“Angalieni kwa mfano, Wambura anakabiliwa na makosa ya enzi za FAT (Chama cha Soka Tanzania – sasa TFF), Simba hata ikiunda kamati ya maadili haina mamlaka ya kuyasikiliza, hivyo nimeyarudisha kwa Malinzi kule TFF,” alisema Rage.
Alisema wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji ya Simba ni watuhumiwa wa kuvunja maadili ya klabu na kanuni za soka, hivyo maamuzi ya kamati hiyo kuunda kamati ya maadili ya klabu yatakuwa yanakiuka misingi ya ‘fair play’ (mchezo wa kiungwana).
Hiyo si mara ya kwanza kwa Rage kupinga maamuzi ya Malinzi kwani Desemba mwaka jana alipinga pia agizo la Kamati ya Utendaji ya TFF kumtaka aitishe mkutano mkuu wa dharura wa wanachama wa Simba kwa ajili ya kumaliza mgogoro ulioibuka ndani ya uongozi wa klabu hiyo.
Lakini, licha ya Rage kuandika barua kwa Malinzi, tayari Kamati ya Uchaguzi ya Simba imetoa tamko kwamba haitasimamisha mchakato wa uchaguzi kwa vile Rais huyo wa TFF hana mamlaka kikatiba kuizuia kuendelea na mchakato huo.
Aidha, Rage alitumia mkutano huo kukanusha taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari jana kuwa ameivunja Kamati ya Uchaguzi ya Simba inayoongozwa na Damas Ndumbaro ambayew ni daktari wa sheria.
“Sijaivunja Kamati ya Uchaguzi ya Simba kwa sababu sina mamlaka ya kuivunja kikatiba na sijaongea na chombo chochote cha habari kuhusu hili,” alisema Rage.
====