*Kukabidhi ofisi Julai 8, 2014
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Klabu ya Soka ya Simba, Ismail Aden Rage, anatarajiwa kukabidhi ofisi kwa viongozi wapya walioko chini ya Rais, Evans Aveva, ifikapo Jumanne Julai 8 mwaka huu katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza nami jana, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa tayari uongozi uliopita unaendelea na maandalizi ya nyaraka mbalimbali za klabu hiyo ili kuwapa viongozi hao wapya waliochaguliwa Jumapili.
Kamwaga alisema pia uongozi huo mpya unatarajiwa kufanya kikao chake cha kwanza cha Kamati ya Utendaji leo kuanzia saa tano asubuhi na tayari wajumbe wote wamejulishwa uwepo wa kikao hicho.
“Sasa tuko katika kutayarisha na kuweka mambo yote sawa, ofisi watakabidhiwa rasmi Julai 8,” alisema Kamwaga ambaye alirithi mikoba ya Evodius Mtawala ambaye alijiuzulu nafasi hiyo na kuajiriwa katika Shirikisho la Soka Nchini (TFF).
Mbali na Aveva, viongozi wengine wapya walioingia madarakani ni pamoja na Makamu wa Rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Saidi Tully, Collins Frisch, Iddi Kajuna, Ally Suru na Jasmine Badour ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
Kiongozi huyo mstaafu wa Simba amemtaka Aveva, kutekeleza ahadi zake alizozitoa wakati anajibadi kwa wapiga kura kubwa likiwa ni kuvunja makundi ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Tabora jana, Rage, alisema kwa kufanya hivyo Aveva na viongozi wenzake wataijenga Simba mpya ambayo itapata mafanikio na sivinginevyo.
“Kwanza nawapongeza wote waliochaguliwa, lakini kubwa Aveva anapaswa kuvunja haraka makundi ambayo yapo katika klabu hiyo ili aweze kufanya kazi yake vizuri”, alisema Rage.
Aliwataka wanachama walioko ‘msituni’ kurejea haraka na kuhakikisha umoja ndani ya klabu unajengwa kwa faida ya Simba.
“Huu si muda wa kuendelea na malumbano, tuache makundi, walioko msituni watoke na tukubali matokeo,” Rage alisema.
Aliongeza kuwa kama makundi hayatavunjwa uongozi wa Aveva hautafanya kazi yake vizuri na badala yake muda si mrefu itaibuka migogoro ambayo itachafua hali ya hewa ya klabu hiyo.
Alisema kuna mazuri mengi aliyoyafanya akiwa kiongozi wa klabu hiyo hivyo uongozi wa Aveva unapaswa kuyaiga na kuyaendeleza kwa manufaa ya Simba.
Rage alisema mbali ya hayo, uongozi huo unapaswa kusimamia na kufuata katiba ya klabu hiyo kama mhimili wa utendaji wao wa kazi.