Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage jana aligeuka mbogo alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu hatma ya kocha wa timu hiyo, Patrick Phiri ambaye mkataba wake unamalizika leo.
Awali kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika wiki iliyopita, Rage alitangaza kuwa klabu hiyo
imemuongezea mkataba kocha huyo pamoja na
kumpandisha cheo kocha huyo na kuwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo.
Hata hivyo, Rage hakuweka wazi mkataba huo mpya na Phiri ni wa muda gani na badala yake alidai kuwa mkataba huo ni siri kati ya klabu na kocha huyo raia wa Zambia.
Lakini habari zilizopatikana ndani ya klabu hiyo zinadai kuwa kocha huyo bado hajasaini mkataba na mabingwa hao wa soka nchini.
“Jamani tumechoka na habari hizi za Phiri, andikeni mnachojua, nimeshaelezea kuwa tumemuongezea mkataba na sio lazima tuweke wazi mkataba wetu ni wa muda gani,” alisema Rage.
Hata hivyo, licha ya upande wa Simba kuelezea kuwa wamempa mkataba mpya kocha huyo, Phiri amekuwa mgumu kuzungumzia kitu chochote juu ya suala hilo.
Na hata alipotafutwa jana mchana kwa ajili ya kuweka wazi kama kweli amesaini tena mkataba na klabu hiyo simu yake ilikuwa haipatikani kwa muda mrefu.
Kabla ya Rage kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuelezea kuingia mkataba mpya na Phiri, kocha huyo alikuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na klabu ya Azam FC ambayo hivi karibuni imeachana na kocha wake, Mbrazil Itamar Amorin.