Wakati Qatar wamesafishwa na madai kwamba walitoa mlungula kupata uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2022, Chama cha Soka cha England (FA) kimelaumiwa kwa kwenda kinyume na kanuni za kuomba uenyeji kwa fainali za 2018.
Ripoti ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) inasema kwamba hapatakuwa na upigaji kura mpya na kwamba FA walijielekeza vibaya kitabia walipotaka kushawishi mpigaji kura muhimu awe upande wao.
Fifa wanasema kwamba Qatar wapo vizuri, wataendelea na uenyeji kwa sababu taratibu na kanuni zote zilifuatwa na hapakuwa na rushwa iliyotembea. Pamekuwa na madai ya muda mrefu kutoka kwa baadhi ya wadau kuhamisha uenyeji wa fainali za soka nchini Qatar wakati wa majira ya joto 2022.
Urusi ndio waandaaji wa fainali za 2018 na wamekuwa wakichagizwa pia kutokana na misimamo ya kisiasa ya Rais Vladimir Putin za kuivamia Ukraine na kuimega kuwa sehemu ya Makamu Mwenyekiti wa Fifa, Mwingereza Jim Boyce amesema anadhani sasa ni muhimu kwa watu kujielekeza katika fursa ambazo hizo zinatoa kwa wadau.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, mwana wa mfalme, Prince William na wachezaji maarufu wa zamani kama David Beckham walijitumbukiza kwenye kampeni wakati upigaji kura ulipowadia jijini Zurich Desemba 2010. Walikutana na wajumbe wa Fifa kwa nyakati tofauti.
Taarifa ya FA, hata hivyo, imekanusha madai ya Fifa na kusema ilijiongoza kwa uwazi na uadilifu mkubwa kama England na pia mtu mmoja mmoja kwa wale binafsi walioshiriki, ikisema inashangazwa na kulaumiwa huko, wakati yenyewe ilichofanya ni kuishikiniza Fifa kuweka mambo wazi na kuhakikisha hakuna rushwa kwenye mchakato.
Katika ripoti yake yenye kurasa 42, mtaalamu huru wa Fifa juu ya maadili na usuluhishi, Hans Joachim Eckert anadai kwamba FA walitaka kukutana na baadhi ya watu ili kuhakikisha wanapata uenyeji, jambo analosema halikuwa sahihi.
Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Fifa, Mwingereza Jack Warner aliachia ngazi 2011 akikabiliwa na tuhuma za rushwa. Msuluhishi huyo anasema matendo ya FA yaliharibu sura ya Fifa katika mchakato mzima wa kuomba uenyeji.
Prince William ambaye ni rais wa FA, anasema alihisi fahari kubwa kuwa sehemu ya watu waliokuwa wakisaka England kuwa mwenyeji. Uchunguzi wa Fifa ulikuwa unaangalia mwenendo wa nchi zote tisa zilizoomba uenyeji wa fainali za ama 2018 au 2022 na uchunguzi ulianzishwa baada ya kutolewa madai ya kuwapo vitendo hivyo 2010.
England waliambulia kura mbili tu wakati awali walishaeleza kuwa na matarajio makubwa ya kushinda uenyeji huo. Nchi nyingine zilizoshiriki ni pamoja na Australia, Japan, Korea Kusini, Uholanzi na Ubelgiji kwa pamoja, Marekani, Ureno na Hispania kwa pamoja.
Ilishangaza kuona Qatar wamewashinda Australia, Japan, Korea Kusini na Marekani kwenye kuwa mwenyeji wa fainali hizo kwa 2022, ndipo zikaanza tuhuma kwamba dola za mafuta zilimwagwa kwa wajumbe ili waipigie kura nchi hiyo ndogo na itakayokuwa ya kwanza Mashariki ya Kati kuwa mwenyeji.