*Real Madrid wawafunza soka Dortmund
Robo fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano hii zimekuwa za ushindi wa mabao matatu kwa timu mbili bora.
Wakati Chelsea wakichezea kichapo cha 3-1 ugenini Ufaransa mbele ya Paris Saint Germain (PSG), Real Madrid waliwachakaza Borussia Dortmund 3-0 kwao.
Chelsea walianza hovyo na kupachikwa bao la kwanza dakika ya tatu tu kupitia kwa mshambuliaji Ezequiel Lavezzi aliyefanya kazi kubwa ya kutuliza mpira gambani, kujikunja na kufyatua mchomo wa juu.
Kama mabeki wa Chelsea wangekuwa waangalifu wangemzuia vizuri, kwani baadhi walishindwa kumsogelea, mwingine akalala chini na wengine wakausindikiza mpira kwa macho ukimshinda kipa Petr Cech.
Chelsea walisawazisha kwa penati ya Eden Hazard dakika ya 27 na kupata nguvu zaidi ya kurudi mchezoni, ambapo penati ilitokana na Thiago Silva kumzuia vibaya Oscar ndani ya eneo la penati baada ya Zlatan Ibrahimovich kumpotezea Mbrazili huyo utawala wa mpira kwenye eneo la wenyeji.
Chelsea walijikuta wakipachikwa bao la pili ambalo lawama zilielekezwa kwa David Luiz, kwani ndiye alisababisha mpira wa adhabu ndogo kwa kumchezea vibaya beki wa kushoto aliyepanda, Blasio Matuidi.
Lakini kana kwamba haitoshi, alikuwa Luiz tena aliyekuwa nyuma ya kipa wa Chelsea aliyeukwamisha mpira wavuni mwa timu yake yenyewe, pengine akidhani alikuwa akiokoa.
Luiz alitolewa nje baada ya kipindi cha kwanza kwenye mechi iliyopita dhidi ya Crystal Palace kwa kucheza hovyo, lakini kwenye robo fainali hii Mourinho alimwacha hadi mwisho, licha ya kunyanyua kidole chake kuashiria ni hali isiyokubalika baada ya matukio hayo.
Chelsea waliloweshwa bao la tatu katika dakika ya mwisho ya nyongeza, pale mchezaji Pastore alipotokea eneo la kona, akawalamba chenga wachezaji wa Chelsea waliokuwa wamejipanga na wengine wakabaki wakimwangalia hadi alipomchambua Cech kwa upande huo huo aliokuwa wa kushoto kwa kipa.
Wachezaji wa Chelsea walidhani madhara hayangekuwa makubwa kwao, hasa baada ya Edinson Cavani kuwa na kosakosa nyingi na pia Ibrahimovich kuumia na kutoka nje kabla ya Pastore kuja kuwashangaza kwa maudhi.
Baada tu ya bao hilo, ambapo mpira ulikuwa ukimalizika, Mourinho alimkumbatia na kumpiga mgongoni kocha wa PSG, Laurent Blanc kana kwamba anaonesha kumkubali yeye na timu yake.
REAL MADRID WATAKATA
Real Madrid walifanikiwa kuwatandika Borussia Dortmund kwa mabao 3-0 kwenye mechi nyingine ya robo fainali katika Uwanja wa Santiago Bernabeu usiku wa Jumatano.
Gareth Bale alifunga bao la kwanza dakika ya tatu, Isco akifunga dakika ya 27 kabla ya mchezaji bora wa dunia, Cristiano Ronaldo kupachika la tatu dakika ya 57 akimpita kwa manjonjo kipa Roman Weidenfeller kabla ya kutumbukiza mpira kimiani.
Dortmund wanaofundishwa na watakuwa na kazi nzito nyumbani wiki ijayo kwenye mechi ya marudiano.