PSG wamtega Di Maria
*Bale hataondoka Real Madrid
*West Ham wamtaka Kounate
Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) wameeleza kuandaa kitita kikubwa cha fedha kwa ajili ya kumnunua Angel Di Maria wa Manchester United.
Di Maria alisajiliwa kiangazi kilichopita kwa kuvunja rekodi za Uingereza, kwani ada ya uhamisho ilikuwa pauni milioni 59.7 lakini hajakuwa na ufanisi uwanjani.
PSG wanaelezwa kwamba wangependa kumchukua katika jitihada za kujiimarisha, hasa baada ya kuibuka habari kwamba Kocha Louis van Gaal haridhishwi naye na amejaribu kumchezesha nafasi tofauti bila mafanikio.
Inaelezwa kwamba kocha huyo anapanga kununua wachezaji wengine, akiwamo winga wa PSV Eindhoven ya kwao Uholanzi, Memphis Depay (21).
Atletico Madrid nao wanaelezwa kuwa tayari kumuuza beki wao wa kati, Miranda (30) kwa pungufu ya pauni milioni 21.9, huku United wakielezwa kutaka kumchukua pia.
Reald Madrid kwa upande mwingine, wanafikiria njia rahisi zaidi ya kumpata kipa badala ya kumchukua wa Man United, David De Gea (24) kwa ajili ya kuwa mrithi wa Iker Casillas. Wanafikiria kumsajili kipa wa Bayer Leverkusen, Bernd Leno (23).
West Ham wanafikiria kumsajili mshambuliaji wa Senegal, Moussa Konate aliyefunga mabao 11 katika emchi 17 akiwa na FC Sion msimu huu.
Manchester City wanajipanga kuchuana na Bayern Munich na PSG ili kumsajili winga wa Wolfsburg, Kevin De Bruyne aliyeuzwa huko kutoka Chelsea. Bei yake sasa huenda ikafika pauni milioni 40.
Bekiw a kushoto wa City, Aleksandar Kolarov (29) huenda akaondoka klabuni hapo mwisho wa msimu, akitarajiwa kwenda kucheza katika Ligi Kuu ya Italia.
Sunderland wanamfuatilia kwa makini beki wa Liverpool, Tiago Ilori (22) kwani wanahitaji beki wa kati majira ya kiangazi. Mchezaji huyu yupo kwa mkopo Bordeaux.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez amesema hatasikiliza wala kupokea ofa yoyote kwa mchezaji wake, Gareth Bale (25)
Liverpool nao wamesema hawatamuuza nyota wao na Timu ya Taifa ya England, Raheem Sterling mwisho wa msimu huu, hata kama kinda huyo atakataa kutia saini mkataba mpya.
Neymar wa Brazil amesema hana mpango wa kuondoka Barcelona wala kucheza Ligi Kuu ya England.