Menu
in , , ,

PSG WAMNASA RASMI NEYMAR KWA ADA YA REKODI

Tanzania Sports

PSG hatimaye wamekamilisha usajili wa Neymar aliyekuwa mshambuliaji wa Barcelona kwa ada ya paundi milioni 198. Usajili huu unasambaratisha rekodi ya ada ghali zaidi ya uhamisho iliyowekwa na Paul Pogba aliporejea Manchester United Agosti 2016 akitokea Juventus kwa ada ya pauni miloni 89. Neymar alifika kwenye uwanja wa mazoezi wa Barcelona Jumatano akiambatana na baba yake na wakala wake na kuutaarifu uongozi wa Barcelona kuhusu nia yake ya kuihama klabu.

Barcelona walitoa taarifa rasmi kwamba walimweleza Neymar kuwa kifungu cha kutengua mkataba wake kilihitaji zilipwe paundi milioni 198 ili aweze kuachana na klabu hiyo aliyodumu nayo kwa miaka minne tangu Juni 2013 akitokea Santos ya Brazil. Wakati wanasheria wa Neymar walipopeleka fedha hizo Alhamisi kwenye ofisi za La Liga, uongozi wa La Liga ulikataa kupokea malipo hayo kwa kuwa unaamini kuwa PSG wanavunja sheria za uhamisho wa wachezaji za UEFA kwa kutumia fedha nyingi kiasi hicho.

Baada ya kushindwa kuwakabidhi La Liga fedha hizo, wawakilishi wa Neymar walizilipa kwenye ofisi za Barcelona ambapo zilipokelewa na kutengua rasmi mkataba wa Neymar wa kuitumikia Barcelona akiwa ameifungia mabao 105 katika michezo 186. Alitoa pia pasi 80 za mabao akiwa ndani ya jezi ya Barcelona na hivyo amehusika kwenye mabao 185 ya Barcelona kwa kipindi cha miaka minne aliyokuwepo katika klabu hiyo.

SABABU ZA KUONDOKA BARCELONA

Inashangaza mchezaji kuiacha klabu inayoaminiwa kuwa klabu yenye mafanikio zaidi kwenye muongo mmoja uliopita na kujiunga na PSG ambao pamoja na matumizi makubwa ya fedha hawajaweza kupata mafanikio yoyote ya maana kwenye michuano ya Ulaya. Neymar mwenyewe ameitaja sababu ya kumfanya aondoke Barcelona kuwa ni kujaribu kutafuta changamoto mpya. Amedai kuwa Barcelona na jiji la Catalunya siku zote vitabaki moyoni mwake lakini alihitaji changamoto mpya kwenye maisha yake ya soka.

Hata hivyo sababu kuu inayoaminika kumuondoa Neymar kutoka Barcelona ni pesa. PSG wamefanikiwa kumvuta Neymar kutokana na dau nono ambalo waliliweka mezani ambapo atalipwa takribani paundi 520,000 kwa wiki baada ya kodi ambayo ni karibu mara mbili ya kiasi alicholipwa ndani ya klabu ya Barcelona. Mshahara huu unamfanya kumpiku Lionel Messi ambaye inaamika kuwa mshahara wake ni paundi 500,000 kwa wiki. Neymar angebaki Barcelona asingeweza kumzidi Messi kimaslahi kwa kuwa Barcelona wasingekuwa tayari kuuondoa ufalme wa mchezaji bora zaidi kuwahi kuichezea klabu yao.

Sababu kubwa ya pili inayomuondoa Neymar Barcelona ni kile kinachotajwa kuwa kukikimbia kivuli cha Lionel Messi. Unapocheza klabu moja na mchezaji mwenye rekodi ya kutwaa tuzo nyingi zaidi za Balon d’Or ni ngumu kung’ara na kuthaminiwa zaidi yake. Katika umri wa sasa wa Neymar, Lionel Messi alikuwa tayari ameshatwaa mara tatu tuzo ya Balon d’Or wakati Neymar mbaka sasa hajafanikiwa kupata tuzo hiyo ya fahari zaidi kwa mchezaji. Inaaminika kuwa huenda Neymar anajaribu kutafuta nafasi ya kutwaa tuzo kwa kukimbilia kwa matajiri wa Ufaransa ambapo atakuwa nyota muhimu zaidi kwenye timu.

BARCELONA WANAHITAJI KUZIBA PENGO LA NEYMAR

Barcelona wamepoteza mchezaji muhimu mno ambaye hawakuwa tayari kumpoteza. Uwezo wa Neymar wa kuwasumbua walinzi kutokana na ufundi mkubwa alio nao wa kukokota mpira ulikuwa ukiwapa Barcelona makali ya kutosha kwenye safu ya ushambuliaji. Neymar atakumbukwa zaidi alipoiongoza Barcelona kuwaondoa PSG kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akifunga mabao mawili na kupika moja lingine kwenye ushindi wa 6-1. Ameng’ara mno pia kwenye michezo ya kirafiki siku chache zilizopita akifunga mabao mazuri na kutengeneza mengine dhidi ya Juventus, Manchester United na Real Madrid.

Philippe Coutinho wa Liverpool, Ousmane Dembele wa Dortmund, Kylian Mbappe wa Monaco na Eden Hazard wa Chelsea ni baadhi ya wachezaji wanaotajwa kuwaniwa na Barcelona kwa lengo la kuziba nafasi ya Neymar. Si rahisi kumpata yeyote kati ya wachezaji hawa lakini pengine paundi milioni 198 walizoweka mfukoni Barcelona kwenye mauzo ya Neymar zinawapa nguvu ya manunuzi kwenye soko la wachezaji na hivyo ofa nzuri wanazotazamiwa kuziweka mezani ili kumnasa mbadala wa Neymar zinaweza kuwapa mafanikio.

Ni Philippe Coutinho anayepewa nafasi zaidi ya kujiunga na Barcelona huku ripoti zikiarifu kuwa ingawa mwenyewe anahitaji kujiunga na miamba hao wa Hispania, Liverpool hawako tayari kumuuza huku ikitajwa kuwa hawataweza kumuachia kwa dau la chini ya paundi milioni 100. Ingawa hana kiwango cha juu kumzidi Neymar, lakini nyota huyu wa timu ya taifa ya Brazil anatosha mno kuziba pengo la Neymar kwa kuwa ana uwezo mzuri wa kukokota mpira, kutengeneza mabao na muhimu zaidi uwezo wa kupiga mashuti mazuri nje ya eneo la hatari.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version