Hata hivyo msimamo wa Feisal unajulikana kuwa hataki kurudi Yanga, lakini kwa agizo la Rais kuingilia mambo ya michezo maana yake hata upande wa Feisal unaingiwa na presha
SIKU chache baada ya kukosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa bao la ugenini, Yanga wanaelekea kutawazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu 2022/2023 wakiwa na presha kubwa ndani nan je ya uwanja. Uhakika wa kutetea ubingwa wao wanao. Lakini kuhimili presha mpya ndani na nje ya uwanja ni kitu ambacho uongozi wa Yanga unatakiwa kuwa makini na kufanya kazi kwa maarifa zaidi ili kuepuka mtego huo.
Baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho, wachezaji wanne wa Yanga walitajwa kuingia kikosi bora cha mashindano hayo na kuinua sifa na morali ya timu na viongozi. Wachezaji hao ni Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto,Fiston Mayele na Djigui Diarra. Hata hivyo Yanga wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwalinda wachezaji wake na benchi la ufundi.
Wakubwa wenye fedha
Kaw akawaida vigogo wa soka kote duniani wananyakua watumia misuli yao ya kifedha kwa kunyakua wachezaji kutoka timu nyingine. Timu hizo hutumia nguvu ya fedha kwa kuwasajili wachezaji tegemeo katika kikosi kilichofanya vizuri kwenye mashindano kama walivyo Yanga. Kwa mfano, barani Ulaya klabu za FC Porto (Ureno) na Ajax (Uholanzi) zinafahamika kwa kuwauza wachezaji wake nyota inaowasajili kwa dau dogo na kuwapika kuwa wakubwa. Mafanikio ya timu kama Ajax na Porto hugeuka maumivu baada ya timu kubwa zenye fedha kuvamia na kuwasajili wachezaji wao tegemeo.
Klabu ya Simba nchini Tanzania misimu kadhaa iliyopita nayo ilivamiwa na timu zenye fedha na kulazimika kuwauza nyota wake wawili Cletous Chama aliyekwenda RC Berkane na Luis Miquisson aliyesajiliwa na mabingwa wa soka Afrika klabu ya Al Ahly ya Misri. Wachezaji hao walikuwa tegemeo na walizitetemesha timu kubwa zote zilizotia pua zao kwenye dimba la Benjamin Mkapa.
Katika klabu ya Yanga wapo wachezaji wengi wenye uwezo wa kupata nafasi kikosi cha kwanza cha Mamelodi Sundowns, Orlando Pirates, Wydad Casablanca, Esperance, Club Africain, JS Kabylie,TP Mazembe kwa kuwataja vigogo wachache. Presha ya kuwazuia wachezaji wake kusajiliwa na timu za nje ni kubwa. Mfano, Fiston Mayele, Yannick Bangala,Bakari Mwamnyeto,Lomalisa Mutambala,Dickson Job, Ibrahim Bacca,Djigui Diarra, Kennedy Musonda, Clement Mzize ni baadhi tu ambao wanaweza kusajiliwa na miamba mikubwa ya soka Afrika. Kwahiyo utaona hii ni presha nyingine kutokana na mafanikio yao msimu huu.
Benchi la Ufundi
Nasredine Nabi ni raia wa Tunisia. Huyu kocha mwenye uzoefu na soka la Afrika ambapo msimu huu ameibuka na Yanga kabambe iliyotetemesha vigogo. Bila shaka yoyote kiwango na ufundi wa Yanga ni sifa za benchi la ufundi likiongozwa na Nasrideine Nabi.
Vigogo wa soka wanaweza kumchomoa kocha huyu ili aende kuzifundisha timu zao. Fikiria Esparance iliyompoteza kocha wao baada ya kuchapwa mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Ahly jijini Cairo, bila shaka itakuwa inawinda kocha mpya. Kwa sasa Nabi ni lulu ambayo inatia presha katika klabu ya Yanga.
TP Mazembe ambayo imepoteana pakubwa katika soka, ni miongoni mwa sehemu ambazo Nabi anaweza kutua ikiwa bilionea Moise Katumbi ataamua kumwaga fedha za kuvunja mkataba wake na Yanga. Inafahamika kuwa mkataba wa Nabi na Yanga unaelekea ukingoni hivyo kibarua kipo kumshawishi abaki huku kukiwa na presha nyingine kutoka kwa vigogo wa soka Afrika.
Nabi ana uwezo mkubwa wa kuzinoa Esparance, Pyramid,Orlando Pirates,Mamelodi Sundwons,TP Mazembe na nyingine nyingi hapa Afrika. Sioni uwezekano wa Nabi kushindwa kumudu timu yoyote labda wamiliki wawe watu wa ovyo. Katika mazingira hayo Nabi bila shaka atatamani kufanya kazi na msaidizi wake Cedric Kaze raia wa Burundi. Hii ina maana presha kwa Yanga inapanda kwani wakubwa wenye fedha wanaweza kunyakua vyota kadhaa klabuni hapo pamoja na benchi zima la ufundi kwa nia ya kupata ujuzi wao. Hapo ndipo unaona presha waliyokutana nayo Simba inawanyemelea Yanga.
Sakata la Feisal Salum
Yanga kama taasisi msimamo wao upo wazi na wameonesha weledi katika kusimamia. Hawana tatizo lingine, taratibu wanazozitaka zifanyike. Lakini ghafla wamepata presha nyingine kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye amewataka viongozi wa Yanga kumaliza sakata la mchezaji Feisal Salum.
Rais huyo alikaririwa na vyombo vya habari kuwa kusema “taasisi inagombana na katoto” ikiwa na maana kuwaomba,kuwaelekeza na kuwataka walimalize suala hilo. Katika kukazia hoja yake Rais Suluhu Hassan alisema licha ya kuwaomba viongozi wa Yanga pia anategemea kupata mrejesho wa suala hilo. Hii ina maana Rais Samia ametia presha nyingine Yanga ambao wanapaswa kulimaliza sakata hilo, ingawa haijulikani ni njia zipi kati ya kuvunja mkataba na kumwacha mchezaji huyo, Yanga kulipwa fidia au kuendelea kumwamuru arudi kikosini na kuitumikia timu hiyo kwa mara nyingine.
Hata hivyo msimamo wa Feisal unajulikana kuwa hataki kurudi Yanga, lakini kwa agizo la Rais kuingilia mambo ya michezo maana yake hata upande wa Feisal unaingiwa na presha hivyo nao uwezekano wa kushusha madai na kurudi kundini huenda ikawa mojawapo ya suluhiho. Kwa hakika hizi ndizo presha zinazoukabili uongozi wa Yanga chini ya Rais Hersi Said.