Hata hivyo uongozi haujaweka wazi vigezo vya makocha wanaohitaji wala kutaja majina yao…
HATA aje nani, bado shughuli itakuwa ngumu na kocha mpya wa Yanga ambaye atakutana na kikosi kingai cha moto licha ya kuchukua ubingwa misimu miwili mfululizo. Uongozi wa klabu ya Yanga utakuwa na kibarua kigumu kumwajiri kocha ambaye atakuja kukidhi vigezo vya mafanikio yaliyoachwa na Nasreddine Nabi ambaye ametimka klabuni hapo baada ya kuongoza kwa mafanikio makubwa.
Viwango vilivyowekwa na kocha Nabi ndivyo vitakavyosumbua vichwa vya viongozi na mashabiki wa Yanga, kwamba watalazimika kutumia mafanikio hayo kama kigezo cha kumpima kocha watakayemwajiri au watakayekuwa naye kuanzia msimu ujao. Yanga wapo kwenye mawindo ya kocha mpya ambaye atatakiwa kutetea taji lao na kufunika kivuli cha mafanikio ya Nasreddine Nabi.
Vyanzo vya taarifa kutoka klabu ya Yanga vimeieleza TANZANIASPORTS kuwa uongozi wa klabu hiyo umejipangia malengo ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Rais wa klabu hiyo Hersi Said aliwahi kufichua mkakati wao wa kufuzu Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini vyanzo vingine vimeeleza kuwa kinachohifiwa na kuleta presha kwa uongozi ni kocha mpya kukidhi vigezo na kuwa na ufanisi kama wa Nasreddine Nabi. Hivyo viongozi wanaamini kuwa Nabi ndiye mwongozo wao katika kumwajiri kocha mpya.
Makocha mbalimbali wamehusishwa kwenye mchakato wa kujiunga na klabu ya Yanga wakiwemo Josef Vukusic raia wa Slovakia ambaye amewahi kufundisha vilabu kadhaa kadhaa katika Ligi Kuu Afrika kusini. Kocha huyo anadaiwa kuzifundisha klabu ya Amazulu pamoja na Kocise Fc ya huko kwako Slovakia. Kocha mwingine anayehusishwa kuinoa Yanga ni Miguel Angel Garamondi kutoka nchini Argentina ambaye kwa sasa ndiye kocha mkuu wa klabu ya Ittihad Tanger ya Morocco. Miguel anasemekana kuwa na uzoefu wa kuzitoa timu za Afrika kama vile Mamelodi Sundowns, USM Alger, Wydad Casablanca, Platinum Stars na CR Belouzidad, Esperance na msaidizi wa kocha wa timu ya Taifa Burkina Fasso. Hata hivyo uongozi haujaweka wazi vigezo vya makocha wanaohitaji wala kutaja majina yao.
Presha ya mashabiki na viongozi
Mashabiki wa Yanga nao wamejaa presha juu ya ujio wa kocha mpya huku wengi wakijiuliza swali je kocha mpya atakayeajiriwa na viongozi atakuwa na uwezo kama Nasreddine Nabi? Ni dhahiri wamenyong’onyea baada ya kocha kipenzi chao kuondoka Yanga, lakini hofu inayokabili ni mwendelezo wa furaha zaidi kwa kocha ajaye. Ni vipi kocha huyo ataweza kuwashawishi mashabiki wa Yanga kumsahau Nabi haraka kwa kuleta mafanikio klabuni. Viongozi wa klabu ya Yanga nao wanakuwa kwenye presha kubwa kutafuta namna ya kuwaridhisha mashabiki na kuwaaminisha kuwa kocha ajaye atakuwa na mafanikio na kipenzi chao. Yanga walifurahia uwanjani, wakashangilia nje ya uwanja kwa mafanikio yao. Ili wamsahau Nabi ni lazima kocha ajaye alete mafanikio klabuni.
Presha ya wachezaji
Kila mchezaji hupendelea kufanya kazi na kocha aina fulani. Wengi wa wachezaji wa Yanga ni matunda ya usajili wa Nabi katika kipindi cha miaka miwili na nusu aliyoishi nchini kama kocha mkuu. Nabi aliwalea wachezaji, akawaimarisha viwango, akawapa morali, akawahakikishia mashabiki kuwa mchezaji anayesajiliwa klabu hapo ana kiwango na uwezo wa kufanya vizuri klabuni. Ghafla wachezaji wanaona kocha wao kipenzi ameondoka, hali hiyo huzua wasiwasi juu ya nini matakwa ya kocha mpya.
Kwa kawaida baadhi ya wachezaji hutamani kuhama ili kuepuka na zama mpya za kocha mwingine. Lakini kama binadamu nao wanaamini kuwa walisajiliwa na kocha mwingine na hivyo akija mwingine wanaweza kuambiwa hawapo kwenye mipango yao. Kila kocha anakuja mfumo wake ambao unahitaji wachezaji wa aina fulani. kwahiyo katika mazingira ya namna hiyo wapo wachezaji wanaoweza kuomba kuondoka klabuni.
Ni jukumu la uongozi wa Yanga kugundua wasiwasi unaowatawala wachezaji mara baada ya kocha wao kuondoka. Ni wajibu wao kutumikia klabu na vipaji vyao vinaweza kutumika na kocha mpya, lakini mifumo ndiyo huwaondoa wachezaji katika timu. Wakati akiwa Arsenal Alexander Hleb alikuwa mchezaji muhimu sana, lakini alipohamia Barcelona mambo yalikuwa tofauti, mifumo tofauti na ikafika mahali akaonekana kama si chochote.
Hali kadhalika Thiery Henry alikuwa mshambuliaji hatari Arsenal na ndiye alikuwa akiongoza safu ya ushambuliaji lakini alipotua Barcelona akapangwa wingi ya kushoto katika mfumo wa washambuliaji watatu. Majukumu ya safu ya ushambuliaji yalihamishwa na akatakiwa kusaidia ulinzi pia. Katika hali ya kawaida mfumo uliombakiza Hnery si wote unaweza kuwafaa.
Hali kadhalika baadhi ya wachezaji wa Yanga wametumika katika nafasi tofauti kwa sababu ya imani kocha. Kibwana Shomari ni beki wa kulia, lakini chini ya Nabi amekuwa beki kushoto pia. Farid Mussa ni wingi wa kushoto au kiungo mshambuliaji lakini baadhi ya mechi amechezeshwa beki wa kushoto. Yannick Bangala amekuwa akicheza nafasi ya kiungo lakini wakati mwingine Nabi alikuwa akimpanga beki wa kati.
Mifumo ya Nabi ilimbeba kwa namna alivyohitajika, vipi kocha mpya ataweza kuwatuliza wachezaji hawa? Kuwafanya wanahitajika klabuni ndicho kibarua cha kwanza cha kocha mpya wa Yanga. Hawa ndiyo wachezaji waliowaletea mafanikio, lakini haina maana kuwa wote wanapaswa kubaki au kuhurumiwa hata hivyo kibarua kipo palepale. Ni njia ipi Yanga watachagua kutuliza presha iliyopo klabuni kwao? Hilo ndilo muhimu kwao.