Menu
in

Polisi waweka mitego Uchaguzi Mkuu TFF

BAADA ya miaka minne kasoro siku 14, Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF unafanyika leo kwenye Ukumbi wa NSSF Water Front Dar es Salaam.

Kamati ya Utendaji ya TFF, chini ya Rais wake, Leodegar Chilla Tenga inakamilisha muhula wake baada ya kupewa dhamana ambayo sehemu kubwa kila mpenda soka ameona kilichofanyika.

Timu ya Tenga ilichukua dhamana hiyo kutoka kwa uongozi wa iliyokuwa FAT na TFF, Muhidin Ndolanga na katibu wake, Michael Wambura ambaye jina lake limekatwa dakika za mwisho kwa kilichoelezwa kukosa sifa.

Katika mkutano wa leo wa uchaguzi, TFF mpya itaingia madarakani kupitia kwa wajumbe 111 ambao kwa kauli moja wataamua majaaliwa ya soka ya Tanzania kama.

Wajumbe hao wanapatikana kwa kila chama cha mkoa ambavyo vinatoa wajumbe wanne kila chama cha mkoa kwa mikoa 21 ambayo inatengeneza wajumbe 84.

Pia kunakuwa na klabu za Ligi Kuu zinazowakilishwa na mjumbe moja kila klabu – kwa kuwa klabu hizo ni 12 hivyo wajumbe ni 12 pia.

Vyama shiriki vinawakilishwa na wajumbe watatu kila chama ambavyo ni TAFCA, FRAT, SPUTANZA, TASMA (wataalamu wa Tiba) na TWFA (Wanawake), Jumla ya wajumbe kutoka vyama hivyo ni 15 ambavyo kwa jumla wanakamilisha wapigakura 111.

Wagombea watakaopigiwa kura kwa nafasi ya urais ni Tenga na Jamal Emil Malinzi wakati nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais iliyokuwa chini ya Crescentius Magori inawaniwa na watu wanne.

Wanaopigana vikumbo kuwania nafasi hiyo ni Lawrence Mwalusako, Ali Hassan Mwanakatwe na Athumani Nyamlani wakati makamu wa pili ni Damas Ndumbaro na Ramadhani Nassib. Pia nafasi za wajumbe kupitia kanda mbalimbali.

Baada ya usaili, kuanzia Desemba 6, wagombea walikuwa katika kampeni mbalimbali lengo ni kuwajengea wapiga kura mazingira ya uhalali kuingia ndani ya TFF.

Wajumbe hao walianza kwa mkutano mkuu jana uliokuwa na kazi ya kupokea taarifa ya mahesabu, mapato na matumizi katika kipindi chote walichokuwa madarakani. Zaidi ya Ajenda 13 zimeandaliwa katika mkutano huo.

Naye Mussa Mkama anaripoti kuwa, askali polisi waliokuwa na wasio na sare ni miongoni mwa vionjo vya nje ya mkutano huo.

Mwananchi Jumapili iliyokuwa ikivinjari viunga vya ukumbi huo, ilishuhudia askari hao na kubaini kuwa baadhi yao ni kutoka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa, TAKUKURU waliokuwa wakirandaranda.

Takukuru walikuwa wametinga fulana zinazofanana na walizovaa wajumbe ikiwemo jezi maarufu za Taifa Stars pamoja na vitambulisho walikuwa wakizunguka huku na kule ili kuwanasa wale wanaotoa na kupokea rushwa kwa ajili ya kupata madaraka TFF.

Majira ya Saa 2:30 asubuhi kabla ya wajumbe wa mkutano mkuu kuwasili katika ukumbi huo, ulinzi ulikuwa umeimarishwa kila kona ya ukumbi ili kuhakikisha hakutokei vurugu.

Wajumbe wa mkutano walionekana kushangaa kitendo kile ambacho hakijawahi kutokea katika mikutano inayofanywa na TFF na kusema kuwa mwaka huu kunaupinzani mkali hasa katika nafasi ya kinyanganyiro cha Urais.

Kamanda wa Kanda ya Kipolisi, Mkoa wa Ilala, Faustin Shirogile alisema wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wasiwe na wasiwasi na wala wasiogope kuona hali kama hiyo kwani hiyo yote ni kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika salama salimini.

Alionya: “Wajumbe, mmoja mmoja au kikundi wasishawishike kudanganywa na mtu kufanya vurugu ambazo zitasababisha kusimama kwa uchaguzi kwani kufanya hivyo ni uvunjifu wa amani mahala hapo hivyo atajikuta yupo mikononi mwa dola.”

Mwananchi ilishuhudia kundi la vijana wadogo ambao walikuwa wamevaa fulana zenye picha ya Jamal Malinzi, mgombea wa nafasi ya urais wakigawa vipeperushi vya kumnadi mgombea wao kila mjumbe liyekuwa akiingia ndani.

Ujio wa kundi hilo la vijana wadogo ambapo awali walikuwa wamevaa jezi pamoja na viatu vya kuchezea soka walikuwa kivutio cha aina yake.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version