Menu
in , , ,

Platini naye kikaangoni FIFA

*Ni kama Baba na Mtoto*

Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini aliyekuwa mstari wa mbele kumtaka Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Sepp Blatter aachie ngazi, naye anachunguzwa kwa madai ya kupokea mlungula.

Platini aliyekuwa anatajwa kuwa katika uwezekano wa kuchukua nafasi ya Blatter, anadaiwa kwamba alipokea hongo ya pauni milioni 1.35 kutoka kwa Blatter ili kuondoa jina lake kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi.

Kwa msingi huo, sasa ameanza kuchunguzwa na Kamati ya Maadili ya FIFA, wakati Blatter mwenyewe amefunguliwa jalada na anachunguzwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) wa Uswisi kwa madai ya kujihusisha na wizi, rushwa na utakatishaji fedha.

Habari hizi ni za kushitua ulimwengu wa soka, kwani Platini alionekana mtu safi wa kuweza kuisafisha FIFA na mazongezonge yaliyoiharibia jina kiasi cha Blatter mwenyewe kutangaza kwamba ataachia ngazi, siku nne tu baada ya kushinda uchaguzi uliopita.

Kamati ya Maadili inachunguza mazingira ya upokeaji wa fedha hizo mwaka 2011, muda mfupi kabla ya uchaguzi wa rais wa FIFA, zikidaiwa kwamba ni malipo ya kazi aliyokuwa amefanya miaka tisa kabla.

Platini amepata kufanya kazi kama mshauri wa ufundi wa Blatter kati ya 1999-2002 amehojiwa pia kama shahidi na maofisa wa Ofisi ya AG wanaomchunguza Blatter, lakini hadhi yake kwenye mahojiano hayo ilikuwa ni shahidi.

Madai kwamba Blatter, 79, binafsi aliidhinisha malipo kwa Platini yalikuwa kwenye andiko la AG wa Uswisi, wakati akitangaza kuanza kwa uchunguzi dhidi ya Blatter. Wapelelezi wanaamini kwamba Blatter alitumia vibaya madaraka yake kwa kutumia fedha za FIFA kumpa mgombea aliyekuwa anamna wakati mgumu kwenye uchaguzi huo.

Wawili hao walikuwa wakirejewa kama mafahali kwenye mchuano ambao ungefanyika Juni 2011, ukihusisha wapiga kura kutoka mabara yote, lakini ghafla Platini akajitoa. AG anajiuliza kwa nini malipo ya miaka tisa nyuma yafanyike wakati huo, kabla ya uchaguzi, na baada ya hapo Platini akajitoa kwenye uchaguzi. Wote wawili, Blatter na Platini wanakanusha kutenda kosa.

 

Advertisement
Advertisement

Platini alionekana kuwa mgombea mwenye nguvu, na ndivyo wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya FIFA, kama Mohammed bin Hammam walivyochukulia. Bin Hammam, mjumbe kutoka Qatar aliyekuwa pia Rais wa Shirikisho la Soka la Asia. Blatter alikuwa amewaahidi Qatar kwamba angeachia ngazi na kumpa nafasi Bin Hammam kuchukua kiti chake.

Hata hivyo, Blatter alikengeuka ahadi yake na kutangaza kugombea tena, na hapo nyaraka zilizovuja zinaonesha kwamba Platini alisafiri kwenda Malaysia na huko akakutana na Bin Hammam, wakafanya kikao, wakapata mlo wa mchana pamoja Januari 29, 2011, ambapo Bin Hammam aliahidi kumuunga mkono Platini ili wamng’oe Blatter.

Platini alikubali dili hilo, na kampeni za chini chini zikaanza, ambapo Februari ilipofika anadaiwa alipewa mlungula na Blatter na ilipofika Machi akatangaza kujitoa kwenye kinyang’anyoro na kuwaacha Qatar njiapanda.

Mei mwaka huo huo, Platini alisaini azimio linalotaka wanachama wote 53 wa mashirikisho ya soka ndani ya UEFA kumchagua Blatter, ikionekana kama mwangwi wa hongo ile. Uchaguzi ulipowadia, inadaiwa Bin Hammam alijaribu kumzuia Blatter kwa kugawa hongo zilizokuwa kwenye bahasha ya kaki kwa wajumbe wa Caribbean, lakini Blatter akashinda.

Chanzo kilicho karibu na Bin Hammam kinasema kwamba kiongozi huyo alikuwa amechoshwa na Blatter kuvunja ahadi zake. Baada ya Platini kujitoa, ilidhaniwa Bin Hammam angewania, lakini akapendelea zaidi kucheza nyuma ya pazia, lakini akashindwa.

Platini ni mchezaji maarufu wa zamani wa Juventus na Timu ya Taifa ya Ufaransa, lakini hayupo kwenye uchunguzi wa AG wa Uswisi wala ule wa Wamarekani, lakini atatumiwa kutoa taarifa muhimu zinazohitajika.

Platini tayari ametoa taarifa, akisema kwamba yalikuwa malipo halali ya kazi aliyoingia mkataba na FIFA kati ya 1999 na 2002 ya ushauri kwa Blatter. Kwenye uchaguzi wa mwaka huu, Blatter alichaguliwa baada ya kuvuna kura 133 huku mpinzani wake, Prince Ali Bin al-Hussein wa Jordan kupata kura 73 kwenye raundi ya kwanza.

Prince Hussein alijitoa kwenye awamu ya pili ya kura iliyokuwa ifanyike, akikiri kushindwa na kukubali kwamba Blatter amepita.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version