RAIS wa Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), Michel Platini amependekeza kurudiwa kwa kura juu ya uenyeji wa Kombe la Dunia 2022 kutokana na Qatar kupewa nafasi hiyo baada ya kughubikwa na tuhuma za rushwa.
Inadaiwa kwamba aliyekuwa Makamu wa Rais wa Fifa, Mohammed bin Hammam alitoa mamilioni ya dola kwa wajumbe wa mkutano huo ili waiunge mkono Qatar kuwa mwenyeji, ambapo walikubali na kutoa uenyeji majira ya kiangazi ambapo ni joto kali sana Mashariki ya Kati.
Tuhuma mpya na vielelezo vimetolewa wiki hii, ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya Bin Hammam aliye kwenye Kamati ya Maandalizi ya Qatar kwa Kombe la Dunia 2022 na pia alitoa fedha taslimu kwa wajumbe.
Bin Hammam anadaiwa pia kutoa tiketi nyingi, suti, kuhudumia uenyeji wa Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Issa Hayatou na kugharimia kesi ili kuzuia mjumbe ambaye angeweza kuiunga mkono Australia kuwa mwenyeji asipige kura, na kweli hakupiga.
Platini mwenyewe aliipigia kura Qatar lakini sasa anasema kwamba kutokana na uzito wa tuhuma na kama zitathibitishwa basi hakuna budi kura hiyo kurudiwa.
Wanasheria wameshaanza upelelezi kwa kutumia vielelezo husika juu ya tuhuma za rushwa, ambapo Fifa inaonekana kuzama kwenye kashfa kubwa.