Mwanariadha mwenye ulamavu wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius ameangua kilio mahakamani na kuimba radhi familia ya Reeva Steenkamp kwa kitendo chake cha kumuua mpenzi wake huyo.
Akiwa mwenye hisia na kuonesha majonzi mazito, Pistorius alianza kujitetea kwa kuomba radhi, huku sauti yake ikionesha kutetemeka, ambapo alisema alifyatua risasi kwa ajili ya kumlinda mpenzi wake huyo.
Pistorus (27) aliyeweka rekodi kadhaa kwenye ulimwengu wa paralimpiki, alisema anajua maumivu wanayopata wanafamilia hayamithiliki lakini akasema naye ana machungu mengi na kuwa usiku hupata ndoto za ajabu ambazo humwamsha akihisi harufu ya damu ya Reeva.
Waendesha mashitaka wanadai mahakamani hapo kwamba Pistorius alimuua Reeva siku ya wapendanao Februari mwaka jana baada ya kugombana naye, lakini yeye anasema alimuua akidhani ni mwizi.
“Tangu tukio lile hakuna wakati umepita pasipo mie kuwaza juu ya familia yenu. Kila nikiamka asubuhi ninyi ndio watu wa kwanza kuwafikiria, wa kwanza kuwaombea pia. Siwezi kupata ukali wa maumivu na uchungu mnaopata kutokana na pengo nililoleta katika familia yenu.
“Nimejaribu kuweka maneno yangu haya katika maandishi mara nyingi sana ili niwafikishie ujumbe, lakini hakuna aina ya maneno yatakayotosheleza kwenu,” akasema Pistorius huku akitokwa machozi mbele ya ukumbi wa mahakama uliokuwa umejaa watu.
June, mama mzazi wa marehemu Reeva alikuwa amekaa kortini hapo akimsikiliza mkwewe kwa uso mkavu kabisa. Pistorius aliongeza kwamba amekuwa akitumia vidonge vya kuondoa msongo wa mawazo na vingine kwa ajili ya kupata usingizi lakini imekuwa ndoto.
Kijana huyo aliieleza mahakama matatizo aliyopata tangu utoto kutokana na kuzaliwa bila baadhi ya viungo kwenye miguu yake kiasi cha kulazimika kuvaa miguu bandia na kwamba wakati akikua, walipata kuvamiwa na wezi mara nyingi nyumbani mwao.
Akaiambia mahakama kwamba amepata kupigwa risasi akiwa kwenye barabara kuu na kwamab kuna wakati alifuatwa na gari hadi kwenye lango la kuingilia nyumbani kwao, ambapo baada ya watu wawili kumwona ana silaha waliondoka mbio na gari yao. Akasema hata Desemba 2012 alishambulia akiwa kwenye hafla na kujeruhiwa kichwani.
Kesi iliahirishwa baada ya Pistorius kuanza kulia mfululizo wakati akieleza umuhimu wa dini kwake, ndipi wakili wake, Barry Roux akaomba kuahirishwa. Upande wa mashitaka ulikubali lakini ukaonywa isiwe kitu cha kujirudia kila siku. Jumatatu hii ndiyo ilikuwa siku ya kwanza ya Pistorius kujitetea dhidi ya mauaji hayo na atakuwa na mashahidi kati ya 14 na 17.