*Tumetoka mbali sana kama Taifa
PICHA inayomuonesha Rais wa wakati huo wa Sudan, Jaafar El Nimeiry akisalimiana na wachezaji wetu waliokuwa vifua wazi, ni picha maarufu sana kwenye sehemu mbalimbali ikiwemo humu www.tanzaniasports.com/new lakini si wengi wanaifahamu hadithi inayohusu tukio hilo la mwaka 1972, miaka 41 iliyopita.
Kwa kutoifahamu hadithi hiyo, kuna baadhi ya Watanzania kwenye mitandao kadhaa ya kijamii wamewahi kuijadili picha hiyo katika mtazamo wa jinsi Tanzania ilivyokuwa bado nyuma kimaendeleo kiasi cha wachezaji wake kucheza bila jezi, wakidhani hiyo ilikuwa ni hali ya kawaida miaka hiyo. Si kweli. Jezi zimevaliwa nchini mwetu tangu klabu ya kwanza ya soka kuundwa ambayo ni African Sports ya Zanzibar kwenye miaka ya 1920, miaka 52 kabla ya tukio la picha hii ya vifua wazi.
Ukiitazama picha hiyo, unamuona nahodha wa timu yetu ya Taifa wa miaka hiyo,kiungo mahiri Abdulrahman Juma, mzaliwa wa Kondoa, mkoani Dodoma ambaye pia alikuwa nahodha wa timu ya mkoa wa Pwani uliojumuisha Dar es Salaam miaka ile na pia alikuwa nahodha wa timu yake aliyokuwa akiichezea ya Yanga. Hapo anaonekana akimtambulisha Rais Nimeiry kwa wachezaji wa Tanzania. Kwa sasa mchezaji huyo mkali kwa kuchonga kona ni marehemu.
Aliyeshikana mkono na Rais Nimeiry ni Omar Zimbwe wa African Sports ya Tanga. Huyu alikuwa ni beki wa kati kisiki ambaye alikuwa maarufu kwa kupiga penalti. Wa kwanza kushoto ni Mohammed Chuma ambaye alipewa jina la “Chuma” lililomnata na kuwa lake rasmi kutokana na ugumu wake kama chuma katika kupitwa na washambuliaji. Jina lake halisi ni Mohammed Ali.
Beki huyo wa kushoto alichezea timu ya Taifa mfululizo kuanzia mwaka 1964 mpaka mwaka 1975 alipostaafu kuichezea timu hiyo na kubaki kuichezea timu yake ya Nyota ya Mtwara. Alifanyiwa sherehe kubwa ya kustaafu iliyojumuisha mechi baina ya Tanzania na Kenya na kuzawadiwa vya kutosha. Chuma, mzaliwa wa Mtwara, naye ni marehemu.
Kulia kwa Abdulrahman Juma na kushoto kwa Zimbwe ni Kitwana Manara “Poppat” wa Yanga aliyekuwa mkali wa kufunga mabao hasa ya kichwa na hasa hasa ya kona za Abdulrahman Juma. Kitwana alikuwa mshambuliaji wa kati ambapo, kwa mfumo wa enzi hizo, alikuwa namba tisa. Ana asili ya mkoa wa Kigoma lakini ni mkazi wa Dar es Salaam tangu enzi hizo. Alianza soka akiwa kipa akamaliza akiwa mfumania nyavu.
Uso unaoonekana kati kati ya Abdulrahman Juma na Rais Nimeiry ni wa Mshambuliaji matata wa wakati huo, Abdallah Kibaden aliyekuwa namba 10. Kwa sasa Kibaden ni kocha wa Kagera Sugar ya Bukoba. Ni mzaliwa wa Dar es Salaam. Waliobaki pichani wameshindwa kutambulika kutokana na sura zao kutoonekana lakini mwenye jezi anayeonekana kipande mwisho kulia anaweza kuwa kipa Omar Mahadhi wa African Sports ya Tanga wakati huo kwa sababu kipa huyo aliingia uwanjani siku hiyo akiwa amevaa jezi.
Mahadhi, ambaye kwa sasa ni marehemu, alikuwa kipa namba moja wa Tanzania kuanzia mwaka 1971 alipoibuka kwenye timu ya “Taifa Cup” ya mkoa wa Tanga. Aliichezea timu ya taifa mfululizo mpaka mwaka 1978. Sifa ya Mahadhi ilikuwa uwezo wa kucheza vizuri akiwa golini na akiwa mshambuliaji. Akicheza kama mshambuliaji, hasa kwenye timu yake ya African Sports na timu ya mkoa wa Tanga, alikuwa hatoki bila kutikisa nyavu!
Hakucheza mbele akiwa timu ya Taifa na akichezea Simba aliyojiunga nayo mwaka 1975 mwishoni. Akiwa kipa wa timu ya Taifa, aliwahi mwaka 1975 kupiga mpira uliojaa wavuni kwenye lango la Kenya lakini mwamuzi alikosea kwa kuamuru ipigwe kona kuelekea Kenya. Sunday Manara (Yanga) alipiga kona hiyo na Gibson Sembuli (Yanga) alifunga bao.
Kuhusu picha hii maarufu, mwaka 1972, liliandaliwa tamasha la soka kusherehekea miaka 18 ya chama cha TANU (Tanganyika African National Union) kilichoanzishwa Tanganyika Julai 7, 1954. Chama hicho kiliungana na ASP (Afro-Shiraz Party) ya visiwani na kuzaliwa CCM (Chama cha Mapinduzi) Februari 5, 1977.
Tamasha hilo la shereha ya Saba Saba 1972 lilihusisha timu za Taifa za Tanzania, Sudan na Nigeria. Mechi ya kwanza ya tamasha hilo ilikuwa inayohusu picha hii ya historia. Ilikuwa ni mechi baina ya Tanzania na Sudan. Siku hiyo hapo uwanjani kulikuwa na marais wawili, mgeni Nimeiry wa Sudan na mwenyeji Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania, Nimeiry akawa mgeni rasmi. Wakati timu zinakaguliwa, Nyerere alikuwa jukwaani.
Sasa timu zilipoingia uwanjani, wachezaji wa Sudan wakawa safi na jezi zao lakini wa Tanzania wakaingia na bukta, soksi na viatu bila fulana za juu isipokuwa kipa Mahadhi aliyevaa jezi kamili. Watu walipigwa butwaa na kufadhaika ambapo aliyefadhaika zaidi alikuwa Mwalimu Nyerere aliyekiita kitendo hicho kama timu ya nchi yake kuingia uwanjani uchi! Aliagiza apewe maelezo mapema kuhusu aibu hiyo.
Baadaye, wachezaji hao waliingia vyumbani na walipotoka walikuwa wamevaa jezi na kucheza wakiwa wamevaa jezi. Kumbe kilichotokea ni kwamba jezi walizotakiwa wavae zilifuliwa na zilikuwa hazijakauka, huku timu zikiwa zimeitwa uwanjani. Hatua kali ilichukuliwa baadaye kwa waliohusika na uzembe huo uliotusababishia aibu huku Mwalimu Nyerere akiapa kutohudhuria tena uwanjani kutokana na kudhalilishwa huko.
Hata hivyo, miaka mitatu baadaye, yaani mwaka 1975, alipobembelezwa sana alihudhuria mechi ya Tanzania na Ethiopia ya kutafuta nafasi ya kucheza fainali ya mataifa ya Afrika mwaka 1976. Alitoa angalizo kwamba ukitokea udhalilishwaji mwingine, siku hiyo ingekuwa mwisho kwa yeye kuingia uwanjani kutazama mpira.
Kwa bahati mbaya sana, akiwa jukwaani siku hiyo, ulitokea ugomvi mkubwa wa wachezaji kupigana! Mwalimu aliondoka wakati huo huo na kuapa asingehudhuria tena uwanjani kushuhudia mechi ya soka kwani ameshuhudia kero kubwa mara mbili. Kufuatia fujo hizo, Ethiopia iliomba radhi kwani kipa wake ndiye alianzisha ugomvi huo. Matukio kama hayo yalikuwa ya kawaida miaka ile kwa wepesi wa kanuni dhidi ya matukio hayo.
Tukirudi kwenye mechi ya Tanzania na Sudan, matokeo ya mechi hiyo yalikuwa ushindi wa 3-0 kwa timu yetu, Kibaden akifunga bao la tatu kwa “counter attack” baada ya Mahadhi kudaka mpira wa shambulio la Sudan na kumrushia Kibaden aliyekimbia nao mpaka kuuweka kambani. Kwenye mechi yetu dhidi ya Nigeria,matokeo yalikuwa suluhu, yaani 0-0.
Katika tamasha hilo timu yetu ilikuwa hivi:- kipa Mahadhi (African Sports, Tanga), beki kulia Mweri Simba (Tanga), beki kushoto Chuma (Nyota Mtwara),Namba nne Hassan Gobbos (Yanga), beki tano Zimbwe (African Sports, Tanga), Kiungo namba sita, Nahodha Abdulrahman Juma (Yanga), wingi ya kulia Willy Mwaijibe (Simba), kiungo namba nane Sunday Manara (Yanga), namba tisa Kitwana Manara (Yanga), namba 10, Kibaden (Simba) na wingi ya kushoto Nassor Mashoto (Zanzibar).
Akiba: kipa Elias Michael (Yanga), kiungo Mohammed Msomali (Cosmopolitan), Winga Kassim Manga (Morogoro), namba 10 Gibson Sembuli (Yanga) na wengine wachache. Kocha; Paul West Gwivaha.
Hii ndiyo hadithi ya vifua wazi vya timu yetu ya taifa ya mwaka 1972.