Arsenal wamekamilisha usajili wa kipa mkongwe wa Chelsea, Petr Cech, akisaini mkataba wa ‘muda mrefu’.
Kipa huyo wa kimataifa wa Jamhuri ya Czech aliyecheza zaidi ya mechi 400 katika misimu 11 aliyokaa Chelsea anadhaniwa kuuzwa kwa pauni milioni 10 na atakaa Emirates kwa miaka isiyopungua minne.
Cech, 33, alicheza mechi sita tu za Ligi Kuu ya England msimu uliomalizika, baada ya kocha Jose Mourinho kuamua kumpa kipa wa kimataifa wa Ubelgiji, Thibaut Courtois nafasi yake.
Akizungumzia kuingia kwake Arsenal anasema: “Arsene Wenger alipozungumza nami juu ya mpango wake juu ya klabu hii na jinsi alivyoniona ninavyoweza kuwa sehemu ya timu, sikuwa na kigugumizi katika kufikia uamuzi.”
Katika barua yake kwa washabiki wa Chelsea, Cech alisema alidhani kwamba angestaafu katika dimba la Stamford Bridge lakini mambo yamebadilika.
“Si siku zote maisha huenda unavyodhani. Kiangazi kilichopita mambo yalibadilika na nilielewa kwamba sikuwa tena kipa chaguo la kwanza ila nikaona haukuwa wakati mwafaka kwangu kuondoka.
“Katika msimu uliopita, ilikuwa wazi kwamba hali haingekuwa nzuri zaidi kwangu – na nafahamu kwamba sipo kwenye zama za kukaa benchi – nikaamua kufanya uamuzi wa kuondoka kukabiliana na changamoto mpya, akasema Cech.”
Cech alijiunga na Chelsea akitoka Rennes ya Ufaransa Julai 2004 na amezoa mataji 13 akiwa na The Bluse, ikiwa ni pamoja na ubingwa wa Ulaya.
Ameweka rekodi kwa kutoruhusu bao katika mechi 228 kwenye mashindano mbalimbali, akiivunja ile ya kipa wa England, Peter Bonetti aliyekataa kuruhusu bao katika mechi 208.
Bosi Wenger akimzungumzia mchezaji wake huyo mpya wa kwanza kiangazi hiki amesema: “Petr Cech ni mchezaji niliyempenda kwa muda mrefu na nimefurahishwa sana kwa uamuzi wake wa kujiunga nasi.”
Huenda akachezea klabu yake kwenye mechi dhidi ya Chelsea Agosti 2 watakapokutana kwenye mchuano wa Ngao ya Jamii dimbani Wembley.
Cech amekaa miaka 11 Chelsea na katika historia hiyo anajivunia kutwaa mataji yote waliyoshindania, walau mara moja, kama vile ubingwa wa Ulaya.
Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich alitaka aachwe achague pa kwenda kama shukurani kwa utiifu alioonesha kwa klabu japo kocha Mourinho alitaka aende nje ya England.
Kuingia kwake Arsenal kunaweza kumaanisha kuanzisha safari nyingine kwa mmoja wa makipa wao, chaguo la kwanza ngwe ya pili ya msimu uliopita, David Ospina au Wojciech Szczesny.
Ospina ni kipa namba moja wa Timu ya Taifa ya Colombia aliyejiunga Arsenal msimu uliopita akitoka Nice ya Ufaransa wakati Szczesny anadakia Poland, akionekana kusukumwa chaguo la pili na kipa wa zamani wa Arsenal, Lukasz Fabianski.