LIGI Kuu England itaendelea wikiendi hii baada ya kumalizika ratiba ya mechi za Kimataifa za kufuzu Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 huko Qatar barani Asia. Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizokuwa na mechi katikati ya wiki hii ambako waliizaba mabao 3-2 wageni wao Madagascar. Heko kwa Tanzania kuongoza kundi J ikiwa na pointi 4 lenye timu za DRC,Benin,Madagascar na Tanzania wenyewe.
Baada ya ratiba hiyo sasa EPL inarejea kama kawaida, ambapo England walicheza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Poland mjini Warsaw katika mfululizo wa mechi za kufuzu fainali za kombe la dunia mwakani huko Qatar.
EPL kama ilivyo kawaida huwa inabeba mechi kali na zakusisimua kila wikiendi. Kwa mfano wikiendi hii kuna mechi takribani 8 kwa siku ya Jumamosi peke yake. Ni mechi hizo ndizo zimenichochea kuandika uchambuzi huu kuhusu mwenendo wa kocha wa mabingwa watetezi Pep Guardiola, pamoja na mabingwa wa Ulaya Chelsea waliopo chini ya Thomas Tuchel watakaopambana na Aston Villa.
Mechi zingine za siku ya jumamosi ni Patrick Vieira atakiongoza kikosi chake cha Crystal Palace kumenyana na Tottenham Hotspurs, wakati Arsenal watakuwa wenyeji wa Norwich.
Wageni Brendford watawakaribisha Brighton, halafu Manchester United wakiwa na Crsiatiano Ronaldo watakuwa wenyeji wa Newcastle United. Kisha watakatifu Southampton watawakaribisha West Ham United, huku Watfrod wakipepetana na Wolves.
Mechi nyingine kali na ambayo ndio hoja yangu itazikutanisha Leicester City na Manchester City. Kocha Brendan Rogers amtamkaribisha Guardiola katika uwanja wa King Power akiwa ana kila sababu ya kujisifu kuwa ndiye anayemtetemesha bingwa wa EPL kwa sasa.
Brendan Rodgers akiwa na Leicester City msimu uliopita alikutana na Pep Giardiola katika mchezo wa fainali wa Kombe la FA. Katika mchezo huo Brendan Rodgers aliibuka kinara na kumnyang’anya tonge mdomoni Guardiola.
Ulikuwa ushindi mzuri n amuhimu kwa Rodgers ambaye anafundisha soka maradadi. Yeye ni kati ya makocha wazuri waliopo EPL. Ikumbukwe ni mwanafunzi wa Jose Mourinho katika kazi ya ukocha kwa sababu alijifunza akiwa Chelsea.
Hata hivyo Brendan anafundisha soka tofauti na mwalimu wake huyo. Rodgers anapenda timu imiliki mpira na kupigiana pasi nyingi kuelekea lango la adui, pamoja na kubadilika kucheza kwa mashambulizi ya kasi na kushtukiza.
Kana kwamba haitoshi, ni Brendan Rodgers kwa maranyingine alimtetemesha Pep Guardiola katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambaohutumika kama kiashirio cha kufunguliwa pazia la Ligi Kuu England. Katika mchezo huo Leicester City waliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kumwachia vumbi tupu Guardiola kwa mara ya pili mfululizo.
Kwenye mchezo wa fainali ya FA uliokuwa wa kukata na shoka unaweza kusema ilikuwa bahati mbaya Guardiola kufungwa, lakini unapokumbuka amefungwa na Brendan Rodgers lazima utakubali kuwa alizidiwa maarifa na mwenzake.
Kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ungeweza kusema Pep Guardiola alikuwa na silaha zote na nafasi muhimu ya kulipa kisasi pamoja na kumwonesha mpinzani wake kuwa yeye ni gwiji na moto wa kutea mbali. Hata hivyo hali haikuwa hivyo kwa sabahu kipigo cha pili kikamkuta Guardiola.
Minong’ono kuwa Gaurdiola anaelekea kumshindwa kocha wa pili wa EPL ilianza rasmi. Sababu kubwa ni kwamba inafahamika kuwa Guardiola amekuwa akikosaujanja na maarifa mbele ya kocha mwenzake Thomas Tuchel wa Chelsea ambaye amewahi kumponda mara mbili ikiwemo mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Sasa kuibuka kwa Brendan Rodgers kumtetemesha Guardiolandiko kunakoifanya mechi itakayochezwa King Powrr jumamosi wikiendi hii kuwa na hamasa ya aina yake. ni ama Pep Guardiola alipe kisasi cha kufungwa mara mbili au Brendan Rodgers adhihrishe tena ubabe wake mbele ya Mhispania huyo.
Na bila shaka ikiwa Leicester City watashinda mchezo huo utaongeza sifa kwa Rodgers ambaye wacheza kamari wamesema huenda akapewa mikoba ya kuinoa Arsenal. Watabiri wanasema Mikel Arteta aba maisha mafupi klabuni hapo kutokana na matokeo mabovu.
Kama kuna mchi ambayo mashabiki wa soka wanaisubiri kwa hamu baada ya Ronaldo na Man United yake basi kuna hii ya Leicester City na Man City pale King Power. Ni namna gani Pep atamshinda Rodgers, hilo linasubiriwa kwa hamu. Ni namna gani Rodgers ataendeleza ubabe na kumgeuza Pep kuwa kibonde wake, hilo nalo linasubiriwa kwa hamu kubwa.
Ni ama Pep aendelee kuwa kibonde au amshinde Rodgers kumaliza utemi wake. Na hii ndio wikiendi kabambe EPL.