Jumapili ya leo ndio mwisho wa Ligi Kuu ya England (EPL), ambapo timu zote 20 zinashuka dimbani kwa ajili ya kukamilisha ratiba, lakini baadhi zikisaka vitu muhimu.
Kwa upande mmoja Liverpool na Chelsea wanawania nafasi moja iliyobaki kwa ajili ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), Liver wakiwa na alama mbili dhidi ya Chelsea ambao ni mabingwa waliovuliwa taji na Manchester City.
Nafasi za juu zimeshajazwa na City wa Pep Guardiola, Manchester United wa Jose Mourinho na Tottenham Hotspur wa Mauricio Pochettino, ikimaanisha kwamba hao ndio wawakilishi wa England kwenye UCL wakimsubiri mmoja leo hii.
Nafasi kubwa inatolewa kwa Liverpool kutokana na ukweli kwamba wana alama nyingi na wanacheza nyumbani dhidi ya Brighton wakati Chelsea walio chini ya ukufunzi wa Antonio Conte wamesafiri Kaskazini kukwaana na Newcastle wa Rafa Benitez.
Katika wakubwa hawa watano, kuna kocha mmoja ambaye huenda akaondoka, naye ni Conte, na yote itategemea tu na yeye mwenyewe, lakini pia mmiliki wa klabu Roman Abramovich. Conte alijitetea sana kwenye mkutano wake na wanahabari kabla ya mechi ya leo kwamba amekuwa na rekodi nzuri.
Conte ni mjanja; anajua wazi kwamba msimu jana walitwaa ubingwa, lakini yeye anarudi nyuma akisema kwamba timu ipo bora katika nafasi ya tano kuliko alivyoikuta katika nafasi ya 10 alipokuja msimu ule mwingine.
Lakini yote kwa yote ni kwamba msimu huu wameshuka sana na wanaingia mechi ya mwisho wakiwa na alama 23 pungufu ya zile za msimu uliopita. Arsenal wao walishagota katika nafasi ya sita, wakiwa na uhakika kwamba wanakwenda Europa tena kama msimu huu.
Walikuwa wanatishiwa na Burnley ambao kwa hakika wapo vyema, lakini waliwanyoa vizuri tu kwa 5-0 siku Arsene Wenger anaagwa Emirates kwa kuwa anang’atuka. Everton wa Sam Allardyce wapo wapo tu kana kwamba hawataki ubingwa lakini pia kushuka daraja si moja ya machaguo yao.
Baada ya Big Sam kuwasaidia kuwaondoa kwenye eneo hatari, walikuwa kama wame ‘relax’ na hawakutishia tena walio juu, licha ya kuwa na wachezaji wazuri tu na kikosi ambacho msimu juzi walitisha na kudhaniwa kwamba sasa wangekuwa washindani wa kweli wa ubingwa wa England. Washabiki wanalia na kocha na wanataka aondoke, wakidai mfumo wake wa soka hauvutii.
Kule chini hali ndiyo imekuwa hivyo mwaka huu, Stoke wameshuka na miamba wenzao West Bromwich Albion. Swansea ni kuomba tu Manani kwamba utokee muujiza wafunge mabao mengi sana na kushinda na Manchester City wawafunge Southampton mabao ya kutosha. Kihisabati inawezekana lakini kimantiki ni ngumu kusema kuwa Swansea hawashuki.
Huddersfield wamekiepuka kikombe baada ya sare dhidi ya Chelsea, ikimaanisha kwamba timu zote zilizopanda mwaka jana zimefuzu kubaki juu – Newcastle, Brighton na wao. Burnley sasa wanatakiwa wajiandae kwa mikiki ya Ulaya msimu ujao – Ligi ya Europa, wawe na kikosi kipana na wajiandae na maumivu na safari ndefu. EPL ni nzuri lakini ngumu.