Menu
in , , ,

Pazia Ligi Kuu England linaposhushwa

MBIO za msimu mzima wa Ligi Kuu ya England (EPL) zinafika kileleni Jumapili hii, kila timu ikivuna ilichopanda na makocha wakiwa wamegawnayika katika makundi tofauti kulingana na ufanisi wa timu zao.

UBINGWA


Wiki za mwisho mwisho za ligi hii zilikuwa na hali zinazobadilika bila kutarajiwa, hasa kwenye upande wa uongozi wa ligi. Kwa sasa jambo moja ni wazi kwamba Manchester City wanahotaji pointi moja tu wanapocheza na West Ham ili kutwaa taji hilo.

Ili walikose kombe hilo wakienda sare, itabidi Liverpool wawafunge Newcastle mabao 13 ili wafikie uwiano mzuri wa mabao walio nao City, jambo ambalo ni gumu kwa vijana wa Brendan Rodgers.

Hata hivyo, ikiwa Man City watafungwa kwenye mechi hiyo (City wameshinda mechi 16 kati ya 18 walizocheza Etihad msimu huu chini ya Kocha Manuel Pellegrini), basi Liverpool wakishinda watatwaa taji hilo kwa mara ya kwanza tangu 1990. Liverpool wanacheza nyumbani Jumapili hii.

Maoni yangu katika hili ni kwamba suala la ubingwa kwa mwaka huu ni kana kwamba limeshamalizika na City ndio mabingwa wapya, wakiwa wanauchukua mara ya pili ndani ya miaka mitatu. Waliuchukua kwa Manchester United, halafu Man U wakachukua na sasa ngoma inarudi Etihad.

Haiingii akilini kwamba City wataacha kushinda Jumapili hii, ikizingatiwa kwamba ni Jumatano tu walipachika bao lao la 100 walipowakandamiza Aston Villa 4-0 huku Edin Dzeko akiwa amefunga mabao matano katika mechi tatu zilizopita na Yaya Toure akiwa kiungo wa pili tu kufunga mabao 20. Wanayo nguvu kubwa ya kuifagilia mbali West Ham.

NAFASI YA TATU


Vita ya nafasi ya tatu, ambayo anayeipata anaungana na bingwa na wa pili kuingia moja kwa moja kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) imekuwa ikiwaniwa na Chelsea na Arsenal. Vijana wa Jose Mourinho wanaocheza na Cardiff ugenini wanawazidi kwa pointi tatu Arsenal watakaokuwa wageni wa Norwish Jumapili hii.

Kadhalika Chelsea wana uwiano wa mabao wa +43 wakati Arsenal wanao wa +25. Nionavyo mimi ni kwamba wala hapa hakuna vita ya kweli, kwa sababu itakuwa muujiza kwa Arsenal kuweza kufunga mabao 18 kwenye mechi hiyo na wakati huo huo waombe Chelsea wafungwe.

Kwa msingi huu, naweza kusema sasa kwamba Arsenal watashika nafasi ya nne kama ilivyokuwa msimu uliopita, ambapo vijana hao wa Arsene Wenger watatakiwa kucheza mechi ya mchujo ili kuingia hatua za makundi za UCL kama ilivyokuwa mara sita za misimu nane iliyopita.

NAFASI YA NNE

evspurutd777
Kwa mantiki ya maelezo yangu ya awali kuhusu nafasi ya tatu, ni kwamba Arsenal wanatupwa hii ya nne na wameshajithibitishia kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho cha Ulaya kwa hatua za awali, kwani wapinzani wao wakubwa waliowatikisa majuzi ni Everton lakini wameshapoa na wapo nyuma yao kwa pointi saba sasa. Arsenal wameikamilisha kazi yao na sasa wanatakiwa wacheze kulinda heshima tu dhidi ya Norwich huku wakisubiri fainali ya Kombe la FA dhidi ya Hull.
Maoni yangu kuhusu nafasi waliyo Arsenal wakati huu pazia linaposhushwa huku wakiwa kwenye fainali ya Kombe la FA, ni kwamba wametimiza malengo yao, maana ni kana kwamba wamepata taji kulingana na falsafa ya kocha wao, Arsene Wenger.

LIGI YA EUROPA
Timu inayomaliza Ligi Kuu ya England ikiwa nafasi ya tano hufuzu kucheza Ligi ya Europa katika hatua za awali za mtoano. Nayo itakuwa ni Everton kwa msimu huu. Vijana hao wa Roberto Martinez wanaomaliza ngwe kwa kucheza na Hull wapo mbele ya Tottenham kwa pointi tatu. Spurs wanashika nafasi ya sita na wanatafuta kocha baada ya Tim Sherwood aliyechukua nafasi ya Andre Villas-Boas kuonekana kupwaya.

Spurs, kwa hiyo wanahitaji mabao 19 (kitu ambacho hakiwezekani) watakapocheza na Aston Villa ili wawaengue Everton kwenye nafasi hiyo. Kuna nadharia nyingine inajengeka kwamba Sherwood anaweza kupewa kazi hiyo moja kwa moja.

Kwa kuwa Manchester City walitwaa Kombe la Ligi na itashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, basi timu itakayomaliza katika nafasi ya sita itashiriki Ligi ya Europa kwa kuanzia raundi ya tatu ya kufuzu, yaani raundi ya awali kabla ya mechi za mtoano.

Wakati huu ambapo City wamefanya vyema, wapinzani wao wa jiji moja – Manchester United wameloa kwa kuangukia nafasi ya saba lakini wanaweza kubebwa na City kubeba kombe hilo la ligi ikiwa karata zitawaendea vyema United Jumapili hii.

Ikiwa Ryan Giggs atawaongoza vyema United wawafunge Southampton ugenini na Spurs wafungwe na Villa, basi Man U wataingia Ligi ya Europa. Southampton, hata hivyo, wamepoteza mechi tano to nyumbani kati ya 18 walizocheza msimu huu. United wana uwiano mzuri wa mabao (+21) kuliko Spurs wenye +1 tu.

Sasa hapa mimi najiuliza; je, United wanataka kufuzu kucheza Ligi ya Europa kweli? Kwa timu ya hadhi kama hii haina maana na tena ni mzigo mzito kuingia kwenye mashindano hayo ambayo husababisha mlundikano wa mechi na safari za mbali hivyo kuchosha wachezaji.

Tazama jinsi Liverpool walivyofaidi kwa kutokuwa kwenye mashindano hayo msimu huu. Inavyoelekea Spurs watawafunga Villa na ikiwa watafungwa labda Man U walazimishe sare kwa Saints.

FAIRPLAY


Nchi tatu za Ulaya zinazoibuka kwenye viwango vya Uefa Respect hupewa nafasi ya ziada kwenye Ligi ya Europa katika hatua ya kwanza ya kufuzu. Nafasi hii hutolewa kwa timu inayomaliza juu zaidi katika masuala ya haki michezoni kwenye ligi ya nyumbani ambayo haijafuzu Europa kwa njia nyingine.

Kwa viwango vya karibuni zaidi vya Uefa vilivyochapishwa Januari, nchi zilizo juu zaidi ni Finland, Norway na Sweden hivyo kuna dalili kwamba England haitapewa nafasi hiyo. Ikitokea England ikapanda itabidi itafutwe timu.

Hata hivyo, Liverpool, Arsenal na Everton zinazoshika nafasi za juu kwa fairplay tayari zimefuzu kwa nafasi zao kwenye ligi. Spurs wapo nafasi ya nne kwenye jedwali la fairplay. Hawa wakifuzu kwa nafasi yao ya ligi, ina maana fursa itakwenda kwa ama Fulham au Swansea (wanaowafuata Manchester City) kwenye jedwali hilo la fairlplay.

Hivyo basi, iwapo Spurs watashinda au kwenda sare na Villa, basi Swansea watakaocheza na Sunderland, na Fulham watakaokipiga na Crystal Palace watatakiwa wajitahidi kucheza rafu chache kadiri inavyowezekana dimbani ili wawe ‘watoto wazuri’ ili kama England itaongezewa nafasi, mmoja wao aingie Ligi ya Europa.

Maoni yangu binafsi katika hili ni kwamba ni kichekesho pale timu mbili zinapojaribu kufanya rafu chache kadiri inavyowezekana . kumbukumbu ingali mpya jinsi John Arne Riise alivyopata kadi nyekundu kwa uzembe wake. Itashangaza kama wachezaji watajidai kuwa wapole kwa wale wa timu pinzani, mithili ya mmoja kumwambia mpinzani wake auchukue tu mpira kwani si utamaduni wa kisoka.

KUSHUKA DARAJA


Fulham wa kocha Felix Magath na Cardiff wanaofunzwa na Ole Gunnar Solskjaer walikata tiketi za kushuka daraja wikiendi iliyopita kutokana na kupoteza mechi zao pamoja na ushindi wa Sunderland dhidi ya West Bromwich Albion.

Norwich wapo nafasi ya 18 na wana uwezekano mkubwa wa kuwafuata wawili hao baada ya mechi yao dhidi ya Arsenal. Wana pointi tatu pungufu ya West Brom ambao watacheza na Stoke. Norwich wanatakiwa kuwafunga Gunners na West Brom wafungwe na Stoke na hapo yanatakiwa mabao 17.

Nionavyo mimi ni kwamba kihesabu ni jambo ambalo linawezekana, kama ambavyo chama kipya cha ACT Tanzania kilichopata usajili wa kudumu majuzi nchini humo kinavyoweza kushinda kwenye uchaguzi mkuu unaofanyika mwakani.

Naam, hiyo ndiyo hali halisi, nimalize kwa kukuambia kwamba nitakuwa nakuchambulia mechi zote siku ya mwisho ya msimu wa Ligi Kuu ya England kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC na Ulimwengu wa Soka, http://www.bbc.co.uk/swahili/ tafadhali jiunge nasi.

51.577967-0.130467

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version