Menu
in , ,

PAZIA LA MSIMU ENGLAND:

Arsenal wawafyatua Chelsea

Hatimaye kocha Arsene Wenger wa Arsenal amefanikiwa kumaliza ukame wa kumshinda mwenzake wa Chelsea.

Rekodi hii imewekwa katika mechi ya kufungua pazia kwa msimu mpya wa soka ya England, ambapo Arsenal kwa mara ya pili mfululizo wametwaa taji hilo.

Katika Uwanja wa Wembley, alikuwa ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya England, Alex Oxlade-Chamberlain aliyefunga bao hilo muhimu kwa kiki ya nguvu iliyokita kwenye kona ya juu, lakini akitumia mguu wa kushoto ambao hauna nguvu sana.

Nusura Chelsea wasawazishe pale Ramires alipotengewa pande na mshambuliaji wa kati aliyechezeshwa Jumapili hii, Loic Remy, lakini akashindwa kulenga goli lililolindwa vyema na kipa wa zamani wa Chelsea, Petr Cech.

Mmoja wa wachezaji waliochanua sana kwenye Ligi Kuu ya England msimu uliopita, Eden Hazard alikaribia kuzifumania nyavu za Arsenal lakini mpira wake uliotoka kwa Oscar uliparazwa na Cech akiokoa.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa kipa huyo wa zamani wa Chelsea aliyesajiliwa kwa pauni zaidi ya milioni 10 kucheza kucheza dhidi ya klabu yake ya zamani na aliwaonesha kwamba bado yumo, ikiwa ni pamoja na kuzuia vyema mpira wa kichwa wa Kurt Zouma.

Arsenal walionekana kujiamini na nusura wafunge bao la pili kupitia kwa Santi Cazorla na Kieran Gibbs.

Hii ni mechi ya kwanza kwa bosi wa Arsenal, Wenger kumshinda mwenzake, Jose Mourinho baada ya kushindwa kufanya hivyo kwenye mechi 13 zilizopita.

Februari mwaka jana, Mourinho alidai kwamba Wenger amebobea katika kushindwa kwenye kazi na Oktoba bosi wa Washika Bunduki wa London nusura wampeleke chini Mourinho baada ya kumkabili kwenye eneo la makocha.

Arsenal tayari wametwaa makombe mawili wanapojiandaa na Ligi Kuu, ambapo walichukua lile la Barclays Asia na la Emirates. Mchezaji pekee waliyemwongeza kwenye kikosi cha kwanza ni kipa Cech.

Wenger akizungumzia mchezo huo amesema kwamba walikuwa na shida kwa sababu dimba halikuwa zuri, tofauti na walivyotarajia lakini amewasifu mabeki wake ambao hata kwenye mechi nyingine za kabla ya msimu walikuwa wazuri.

Mourinho alidai kwamba Chelsea ndio walikuwa wazuri zaidi kitimu, kwa sababu walikuwa wabunifu na kumiliki mchezo, akiongeza kwamba Arsenal walikuwa wakilinda sana lango lao na walikuwa na mpango mzuri katika hilo.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version