Na: Israel Saria
——–
Mchezo wa soka unaingia kwenye kipindi cha mpito, ukitarajiwa kuanza kushuhudia matumizi ya teknolojia ya kutambua ikiwa goli limefungwa.
Hiyo itakuwa njia ya uhakika, badala ya kutegemea macho ya waamuzi, ambao wakati mwingine hushindwa kung’amua kwa sababu tofauti, ikiwa ni pamoja na msongamano wa wachezaji langoni.
Lawama nyingi zilishatolewa kwa viongozi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa kuchelewa kuanzisha mchakato na hatimaye matumizi ya teknolojia hiyo, kwa sababu baadhi ya mabao yaliyodhaniwa ni dhahiri yalikataliwa, huku timu nyingine zikipewa ‘mabao hewa’.
Kwa miaka mingi, pamekuwapo mjadala kuhusu kuanzishwa kwa teknolojia hiyo na kutumia viwanjani, mjadala ukihusisha viongozi wa ngazi za juu wa soka duniani, washabiki na vyombo vya habari kadhalika.
Imekuwa miaka mingi ya kusubiri kuona teknolojia maridhawa ikitumiwa kuondoa lawama kwa mabao kutolewa au kukataliwa katika mazingira ya kutatanisha.
Hatimaye sasa yamekuwa, kinachobaki ni kusubiri utekelezaji wake.
Halmashauri ya Kimataifa ya Mchezo wa Kandanda, IFAB, iliyoketi katika makao makuu ya FIFA jijini Zurich, Uswisi, umeidhinisha matumizi yake.
IFAB imeidhinisha kwa kura zisizokuwa na upinzani kwamba mifumo miwili ya teknolojia inaweza kutumika ambayo kwa ‘Hawk-Eye’ na ‘GoalRef’.
Hii ya kwanza imepewa jina hilo kutokana na kamera sita zitakazofuatilia mpira kwenye kila lango kuchukuliwa kuwa na uwezo wa ‘Jicho la Mwewe’ katika kuona kutoka kona zote. Teknolojia ya pili yaweza kurejewa kwa Kiswahili kama ‘Mwamuzi wa Goli’.
Inaelezwa kwamba teknolojia hiyo itaanza kutumiwa kwenye mashindano ya klabu ya Kombe la Dunia Desemba mwaka huu.
Ikiwa itafanya kazi vyema na kuwafaa wadau, basi itaendelea kutumika kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho mwakani na Kombe la Dunia 2014.
Mwamuzi hujulishwa kuingia bao kupitia teknolojia ya ‘Jicho la Mwewe’ pindi mpira unapovuka mstari wa goli, na njia inayotumika kufikisha ujumbe ni mawimbi ya redio kwenda kwenye saa ya mkononi ya mwamuzi ndani ya sekunde moja tu.
Ama kwa upande wa teknolojia ya ‘Mwamuzi wa Goli’, kifaa maalumu hubandikwa kwenye mpira unaotumiwa uwanjani, kifaa chenyewe kinaitwa microchip.
Hicho hufanya kazi sambamba na mawimbi ya sumaku karibu na lango na pindi mpira ukivuka tu mstari, teknolojia husika huamua ni goli na kumtumia mwamuzi ujumbe kieletroniki ndani ya sekunde moja pia.
Haya ni mabadiliko makubwa yaliyokuwa yakipigiwa kelele na wadau, changamoto iliyobaki ni utekelezaji wake miongoni mwa wadau hao na wengine.
Rais wa FIFA, Sepp Blatter alikuwa mpinzani mkali wa teknolojia hiyo, akikumbatia uhafidhina wa kuendelea kumwamini mwamuzi.
Lakini sasa, katika wakati mwafaka na muhimu kwa yeyote mwenye kushika wadhifa wa hadhi yake, amebadilika na kuamua kwenda na upepo wa mabadiliko.
Ni hali yake hiyo mpya wanayotarajiwa kuwa nayo viongozi na wadau wote wa soka duniani, wakati huu wa kipindi cha mpito kuelekea matumumizi ya teknolojia ya kutambua bao limefungwa au la.
Hii ni kwa sababu soka ni mchezo mmoja kote duniani, katika nchi zilizoendelea, zinazoendelea na zisizoendelea, hivyo lazima kuwapo ufanano katika kila ngazi na kila eneo la kijiografia.
Blatter mwenyewe aliweka hadharani kwamba alibadili mawazo yake baada ya kushuhudia moja ya matukio mengi ambayo ilikuwa lazima kuwa na teknolojia hiyo, tena katika mchezo muhimu sana.
“Kwangu kama rais wa FIFA, umuhimu wake ulionekana kwangu nchini Afrika Kusini mwaka 2010, nasema ‘asante (Frank) Lampard’.
“Nilinyong’onyea kabisa kule Afrika Kusini na kwa kweli ni kitu kilichonishangaza, ilinichukua sku moja kuonesha kuguswa. Imetokea tena Ukraine, na Ukraine bado haiamini hadi sasa,” akasema Blatter akiwa makao makuu ya FIFA.
Lampard aliifungia England goli dhidi ya Ujerumani mwaka 2010, lakini likakataliwa na mwamuzi kwa utata iwapo mpira ulivuka mstari, lakini ikaja kubainika baadaye kwamba lilikuwa halali.
Kwa hatua hii ya kukubali mifumo ya teknolojia kung’amua ufungwaji wa bao, ni dhahiri kwamba soka haitabakishwa kwenye zama za giza wakati michezo mingine ikikumbatia teknolojia.
Washabiki watapata ufumbuzi wa haraka na wa moja kwa moja wa suala lolote tata. Naam, hawataachwa tena katika mtanziko maisha yao yote, wakilaani na kujiuliza ingekuwaje kama haki ingetendeka kwa kila bao la kweli.
Kwa mtindo huu mpya, haki itatendeka kwa wachezaji wote, wakiwamo ambao wangenyimwa mabao waliyofunga kama Lampard na Marko Devic wa Ukraine aliyefunga dhidi ya England kwenye Michuao ya Euro 2012 na kukataliwa kwa utata huo huo na mwamuzi.
Mifumo ya teknolojia za ‘Jicho la Mwewe’ na ‘Mwamuzi wa Goli’ zinatumika kwa wingi kwenye michezo ya kriketi na tenisi, soka ikabaki imekabwa na ufufutende wa kuchukua hatua.
Msisimko zaidi ni kwamba tayari kuna mjadala wa moja ya mifumo hiyo miwili kuanza kutumiwa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza na Kombe la FA mapema mwakani.
Tayari teknolojia ya ‘Jicho la Mwewe’ imeshafungwa kwenye uwanja unaochukuliwa kama wa taifa wa England – Wembley.
Teknolojia hiyo ilitumiwa kwa majaribio wakati wa mechi ya kirafiki ya maandalizi ya Euro 2012 kati ya England na Ubelgiji mwezi uliopita.
Je, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Uingereza, Alex Horne ana lipi la kusema kuhusu teknolojia hiyo?
“Inawezekana kabisa kuanzisha teknolojia hiyo itumike katikati ya msimu ujao wa ligi. Tayari tuna ‘Jicho la Mwewe’ Wembley.
“Inatakiwa kuwekwa sawa tu kuhakikisha inafanya kazi inavyotakiwa na kwa leseni, ni kama tumekamilisha, tunaweza kuanza kuitumia mapema kabisa.
“Tunaweza kutumia Kombe la FA kufikia uamuzi wetu, kwamba tuitumie kwenye nusu fainali na fainali za Kombe la FA, sidhani kwamba kuna utata wowote kwenye uamuzi kama huo.
“Lakini tunao wajibu wa kwenda kuzungumza na wadau wa Ligi Kuu, ninavyosikia wanaitaka teknolojia hii. Tunaweza kufikia makubaliano ipi tununue na kutumia,” anasema Katibu Mkuu Horne.
Baada ya milango kufunguliwa, au taa za kijani kuwashwa, yaelekea kila mmoja atajitokeza na kutaka mchakato uende haraka kupata na kutumia teknolojia husika.
Ukweli ni kwamba mjadala kuhusu teknolojia hiyo haukujikita kwenye mambo ya asili na usasa katika soka, bali iwapo teknolojia hiyo inaufaa mchezo wenyewe.
Kwenye tenisi na kriketi wanaelekea kuridhishwa na matumizi ya teknolojia hiyo, lakini lazima ieleweke kwamba hii ni michezo tofauti kabisa, kwa hiyo kila upande una wajibu wa kuweka mambo yake sawa.
Bado changamoto ni kubwa, wala isifikiriwe kwamba upatikanaji na ufungaji wa vifaa hivyo ni jambo rahisi katika maeneo tofauti duniani.
Kwa upande wa Kombe la Dunia la Vilabu litakalofayika Japan, kwa mfano, mfumo wa teknolojia hiyo utafungwa kwenye viwanja viwili vitakavyotumika.
Kila kiwanja kitakuwa na teknolojia tofauti kati ya zile mbili na makadirio ni kwamba kila moja itagharimu Dola laki mbili ($200,000).
FIFA inagharimia ankara hiyo ya malipo kwa suala hili maalumu linalohusu michuano yake, unaweza kuelekeza fikara kwenye michuano tofauti ya soka katika ngazi mbalimbali duniani.
Kila kitu kipya kinakuja na changamoto lakini pia na fursa; kwa hiyo ni suala la kampuni kuanza kujitokea kuonesha uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Katika misingi ya uwazi, ukweli na uwajibikaji, imekuwa kawaida kazi kama hizo kutolewa kwa njia ya zabuni kwa kuzingatia viwango na ushindani wa wadau.
Vipi katika Ligi Kuu ya England? Tayari wadau kutoka kampuni mbalimbali wameanza kukodoa macho kuona kipi watapata kwenye hili, maana ni biashara kubwa.
Haijajulikana iwapo waendeshaji wa Ligi Kuu ya England ndio watagharimia uwekwaji vifaa hivyo kabla ya katikati ya msimu ujao wa ligi au vipi.
Kuna mambo mengi na utata haukosekani; yawezekana utekelezaji ukaanza kwa kutumia viwanja vichache, lakini pia kila klabu inaweza kugharimia na kuvifunga kwenye uwanja wake na kukaguliwa kabla ya matumizi kuanza.
Pamoja na ukweli kwamba katika nchi zilizoendelea kiuchumi na kisoka teknolojia hii inaweza kuanza ndani ya mwaka mmoja, katika nchi zilizo nyuma ni ngumu.
Ni wazi kwamba kuruhusiwa teknolojia hiyo kunayaacha mashirikisho mbalimbali ya soka duniani yakikuna vichwa jinsi ya kuipata kwa wakati na kiwango.
Pamoja na mengine mengi, kitita cha fedha kitatakiwa, iwe kinatolewa na mashirikisho au na klabu. Iwe iwavyo, kwa kuanzia lazima mashirikisho kama TFF kujiandaa, maana huu ni mradi na lazima ligharimie, kama England ilivyokwishaanza.
Tunaambiwa tayari kampuni ya Kiingereza imeshaanza kujitembeza, na kuuza pia vifaa hivyo kwa wanachama wa FIFA.
Yawezekana mashirikisho yetu yakawa yanasubiri kusaidiwa fedha na FIFA, na pengine ni sahihi, kwa sababu inasemwa shirikisho hilo limekuwa likitoa kitita cha fedha kwa nchi mbalimbali kuendeleza soka.
Ugumu wenyewe upo kwenye maeneo mengi na nchi nyingi pia – kuanzia upatikanaji wa fedha kwa kazi hiyo hadi uendelevu wa utumiaji wa teknolojia hiyo.
Vifaa vinatakiwa kutunzwa, kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara, lakini si klabu wala mashirikisho ya soka katika ngazi mbalimbali yenye uhakika wa kipato.
Klabu nyingi katika nchi kama Tanzania zimekuwa zikitegemea mapato ya mlangoni na hisani ya wafadhili, wamiliki (kama wapo) au taasisi zinazomiliki timu husika.
Mapato ya mlangoni hayana uhakika wowote, kwa sababu hutegemea upepo wa soka na ukubwa wa timu inayocheza.
Pengine Yanga, Simba na Azam, tena kwa kutegemea wafadhili na wadhamini wao ndizo zipo kwenye nafasi nzuri ya kukusanya kiasi cha fedha kinachotakiwa.
Hii ni katika mazingira ya utulivu, kwa timu mbli kubwa za awali, maana hujazungumzia mapinduzi klabuni na matatizo mengine mengi yanayozikumba.
Pengine wamiliki waviwanja vichache vilivyopo wanaweza kujikakamua wakadunduliza fedha hadi kununua vifaa husika na kuvifunga, vitabaki salama wakati wote?
Vitatunzwa na kufanyiwa matengenezo mara kwa mara ikiwa nyasi tu limekuwa tatizo sugu kwa viwanja vingi? Uwanja wa Sokoine, Mbeya; Uwanja wa Jamhuri Dodoma; Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha; Uwanja wa Jamhuri Morogoro na hata Kirumba, Mwanza, kwa kutaja vichache, haviridhishi.
Je, ni mahali mwafaka kwenye viwanja hivyo na vingine vyote mikoani kuweka teknolojia hiyo ya gharama kubwa? Tumeona jinsi viti na mabomba yanavyong’olewa na kuharibiwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam licha ya ulinzi, itakuwaje mikoani?
Changamoto nyingine ni kwamba michezo mingi imekuwa ikichezwa mchana kwa sababu viwanja havina taa kwa ajili ya mechi za usiku.
Pamoja na kutokuwa na taa, tatizo sugu la umeme limekuwa kigingi kikubwa hata Dar es Salaam nyakati fulani.
Patakuwa na uhakika gani wa matumizi ya teknolojia hiyo inayohitaji umeme wa uhakika kwa viwanja vyote vya Ligi Kuu Tanzania (na nchi nyingine zenye matatizo kama hayo)?
Katika nchi ambazo mgawo wa umeme umeshakuwa kawaida, majenereta yanaweza kuaminiwa kutumiwa kwa ajili ya kuhakikisha teknoloia za ‘Jicho la Mwewe’ au ‘Mwamuzi wa Goli’ zinafanya kazi?
Ikiwa wadau wa uwanja wa timu mwenyeji, wakiwamo meneja wa uwanja, chama cha soka na wengineo hudaiwa kuhujumu matokeo kwa njia mbalimbali, watairuhusu teknolojia ifanye kazi, hata kwa majenereta?
Simulizi za kukatika kwa umeme si za Tanzania tu, tunazo za Nigeria umeme kukatika kwa saa kadhaa kwenye uwanja wa kimataifa wa ndege kiasi cha wasafiri ‘VIP’ kubaki kwenye ndege, itakuwa uwanja wa mpira?
Huenda ikawa teknolojia itakayotakiwa kusubiri muda mrefu ili kwenda sambamba na maendeleo ya nchi na maeneo husika. Vinginevyo labda vitatumika viwanja vichache kwa Ligi Kuu ya Tanzania, kama jijini Dar es Salaam, mithili ya mashindano fulani ya muda mfupi.
Swali jingine wanalojiuliza wadau ni iwapo klabu zote zitamudu kufunga vifaa hivyo? Vipi zikifunga vifaa hivi aghali, halafu hali yao ya fedha ikabadilika kuwa mbovu, utumiaji wake utakuwa endelevu kweli?
Je, timu za klabu husika zikishuka daraja zitaendelea na matumizi ya teknolojia husika iliyokwishafungwa uwanjani?
Au teknolojia iliyofungwa kwa gharama kubwa ya fedha, iwe Dola Pauni au Shilingi, itatelekezwa hapo kwa kipindi kisichojulikana hadi timu husika ije kupanda daraja kurejea Ligi Kuu?
Lakini pia kuna utata wa kuanzisha teknolojia hiyo katikati ya mashindano. Haki itakuwa wapi ikiwa tmu itaishia kushushwa daraja au kutolewa kwenye Kombe la FA kwa goli ambalo lingekataliwa kabla ya Krismasi? Maswali ni hay ohayo kwa ligi na michuano tofauti ya nchi na kanda nyingine, lakini kwa vile si vyema kuvuka mto kabla ya kulifikia daraja, ni bora kusubiri wakati wenyewe ufike.
Pengine wakati huo ndio tutaona jinsi ‘watu wetu’ walivyo watulivu, pale timu nyingine itakapofaidika kwa teknolojia hii mpya.
Kufunguliwa huku kwa milango kunaachia mambo mengi magumu, makosa ya kibinadamu ya mwamuzi yapo na ni vyema kuyarekebisha kwa wakati mwafaka ikiwezekana.
Hata hivyo, kuna dalili za pupa ya kukumbatia teknolojia ya utambuzi wa goli kuishia kuleta utata ambao ilianzishwa kuuondoa.
Kumbe tufanyeje? Tubaki tukijenga imani kwamba soka itaweza kuhimili changamoto zote hizi na nyingine zitakazojitokeza. Kubwa ni kutenda haki, ili soka uendelee kuwa mchezo wa furaha, ushindani wa kweli na mwenye kustahili ashinde mechi.
saria@tanzaniasports.com