Haijapata kutokea; ndivyo unavyoweza kusema kutokana na ujio wa mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Argentina, Lionel Messi kwenye klabu ya Paris Saint-Germain (PSG).
Haikutarajiwa kwamba kinara huyo angeondoka Barcelona baada ya kukaa huko kwa muda mrefu na kuwa kama mbia, lakini Jiji la Paris limekuwa na shangwe za aina yake katika maeneo tofauti.
Ukiachilia kutambulishwa kwa Messi klabuni, mambo mengine makubwa ni misururu ya watu waliotaka kununua jezi ya Messi, ikiwa na jina lake mgongoni na namba 30. Katika duka la PSG linalokwenda kwa jina la Champs-Elysees jezi jezi hiyo ndiyo ilikuwa ikifukiziwa na washabiki wengi waliosota kwenye mstari mrefu.
Bei yake ilikuwa kadiri ya euro 160 na ni jezi iliyovutia watu wengi, wakiwamo waliotoka Matamoros, Mexico ambao ni Jorge Ruiz, Ricardo Longoria Fuentes na Rubi Compean walioazimia kufika Paris kwa ajili ya mchezaji huyo. Walichukua saa nne hadi kufanikiwa kupata jezi hizo zilizowekwa vyema kwenye mifuko ya karatasi ya rangi ya kahawia, jumlaya gharama zake zikiwa ni karibu €1500.
Ruiz alionekana kujawa furaha hasa na baadaye alitundika jezi hiyo ya Messi mabegani mwake, mithili ya mtu anayebeba mnyama aliyemuwinda, huku akitulia kwa ajili ya picha kadhaa upande wa pili wa duka la Disney. Inaonekana sasa klabu ya PSG na Jiji la Paris litakuwa na mvuto wa kipekee kutoka pande mbalimbali za dunia kwa ajili ya mchezaji huyo aliyepatakufikiriwa kwamba ikiwa angeondoka Barcelona angejiunga na Manchester City kutokana na ukwasi wao.
Ruiz na rafiki zao hao ni washabiki wa klabu ya Cruz Azul, lakini wakasema kwamba walifika Paris kwa sababu moja tu. “Tunaishi Mexico, na tumekuja hapa kwa sababu hii yu. Huyu (Messi) ni mchezaji bora zaidi duniani,” akasema Ruiz.
Kwa hakika iliyopita ilikuwa wiki ambayo PSG imeonekana kama makao makuuu ya soka ya dunia baada ya kufanikiwa kumtwaa mchezaji huyo nyota na kwa hakika mazingira ya Paris yalibadilika na kuwa tofauti kabisa kwa mvuto ulioambatana na ujio wa mchezaji huyo.
Messi alitambulishwa na kuoneshwa kana kwamba ni kombe lenyewe, akipangiwa na kukaa kwenye jukwaa la muda nje ya upande wa Mashariki wa dimba la klabu hiyo, Parc des Princes, mbele ya maelfu ya washabiki waliokuwa wamejawa furaha.
Kwa kawaida raha ya kwenye soka ni kutwaa mataji, lakini washabiki wa PSG safari hii walionesha ushangiliaji na raha ya aina yake kutokana na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34.
“Nikiwa shabiki wa Paris, kwa hakika ni raha sana kuiona Paris ikiwa na Messi,” akasema mnazi mmoja, Tom Lamothe, akiongeza kwamba hakutarajia jambo kubwa kama hilo.
Hicham Zedira, shabiki wa PSG kwa maisha yake yote alikuwa na haya ya kusema; “Tuna raha kubwa sana ya kumuona (Messi) akiwa Paris. Ni mshangao mkubwa wa majira haya ya joto, yaani kumwona hapa Paris imekuwa kama mujiza. Inashangaza sana.”
Upande wa Kaskazini wa dimba la Parc des Princes, unaotazamana na Rue Claude-Farrere, kuna ukuta wa wakongwe wa soka katika historia ya PSG; kuanzia Jean-Pierre Dogliani, Mustapha Dahleb, Jean-Marc Pilorget, Safet Susic, George Weah, David Ginola, Rai, Bernard Lama, Pauleta, Ronaldinho na Zlatan Ibrahimovic.
Mbele ya ukuta huu wa wakongwe, Abdoulaye Badiane anazungumzia juu ya msimu wa 2007/8 ambapo PSG waliwasononesha washabiki wao kwa kumaliza Ligi Kuu ya Ufaransa – Ligue 1 wakiwa nafasi ya 16, ukiwa ni msimu mbaya zaidi tangu 1975, wakanusurika kushuka daraja kwa tofauti ya alama tatu tu. Anasema hawawezi kusahau msimu huo na kwa sasa wanaona wametoka mbali sana.
PSG ni klabu ya aina yake kwenye ulimwengu wa soka na sasa wamejenga timu yenye wachezaji wenye talanta kubwa kuliko walivyopata kufanya kabla. Ni wazi kwamba hiyo ni kutokana na ukwasi mkubwa wa wamiliki wa klabu ambao ni matajiri wa Qatar.