Panga la UEFA kwa England?
Majaliwa ya England kufanya vizuri kuelekea Kombe la Dunia 2014 Brazil yanazidi kuingia doa.
Safari hii ni tetesi kwamba huenda wakaadhibiwa na kulazimika kucheza bila washabiki wao kwenye uwanja wa Wembley.
Hiyo ni adhabu inayoweza kutolewa, kutokana na madai kwamba washabiki wa England waliwazomea kibaguzi Rio Ferdinand na mdogo wake Antony, baada ya Rio kuitosa timu ya taifa.
Rio na Anton ni wachezaji weusi, na hivi karibuni pamekuwapo vitendo vya kibaguzi dhidi ya wachezaji wa aina hiyo, na mamlaka za soka za UEFA na FIFA zimedhamiria kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo kama hivyo.
Rio, beki wa kutumainiwa wa kati, alikataa mwito wa kocha Roy Hodgson kujiunga na England kwa ajili ya mechi dhidi ya San Marino na Montenegro.
Alikataa mwito huo miezi michache baada ya kulalamika kutoitwa, na wakati huo Hodgson alisema ni sababu za kisoka tu. Safari hii alikataa kwa maelezo anaumwa mgongo, ana ratiba ngumu ya matibabu na mazoezi na klabu yake ya Manchester United.
Hata hivyo, wakati England wakipanda ndege kwenda San Marino, Rio alikwea yake kwenda Qatar, alikokuwa akichambua mechi hiyo hiyo kupitia kituo cha televisheni, na kulipwa kitita kizuri.
Kundi la washabiki wa England linadaiwa kutoa maneno machafu ya kibaguzi uwanjani, wakati England wakiifyatua San Marino mabao 8-0.
Pamoja na maneno mengine, washabiki hao wanadaiwa kusema Rio na Antony wanatakiwa kuchomwa pamoja na takataka kwenye moto mkubwa utakaoandiwa eneo la wazi.
Katika mechi dhidi ya Montenegro, England walicheza vyema kipindi cha kwanza, wakaongoza kwa bao moja lililorejeshwa kipindi cha pili walipocheza kichovu.
Katika mechi ijayo, England wanacheza na Moldova Septemba 6, kabla ya kwenda Ukraine Septemba 10.
England wanashika nafasi ya pili, wakiwa nyuma ya Montenegro kwa pointi mbili, na ili wajihakikishie kufuzu moja kwa moja, wanatakiwa washinde mechi zote nne zilizobaki.
UEFA imesema kwamba itawaunga mkono hata waamuzi watakaositisha mechi kutokana na kutokea mambo ya ubaguzi wa rangi.
Shirikisho hilo la soka la Ulaya, linaweza kulazimika kuwachukulia England hatua hiyo, kama lilivyofanya kwa Hungary na Bulgaria baada ya washabiki wao kutoa maneno ya kibaguzi na ishara za nyani.