Klabu ya Pamba imefanikiwa kupanda daraja na kuingia ligi kuu ya Tanzania bara na kupanda kwao kwa ligi kuu ni baada ya zaidi ya miaka 20 toka waliposhuka daraja na kasha kurudi katika madaraja ya chini. Mara ya mwisho klabu hiyo kushiriki ligi kuu illikuwa mnamo mwaka 2001 ambapo ndipo waliposhuka daraja. Miongo miwili imepita toka mamlaka ya pamba kushuhudia klabu ambayo wanaimiliki ikicheza katika ligi kuu.
Klabu hiyo imeweza kufuzu kucheza ligi kuu baada ya kuwa mshindi wa pili katika ligi hiyo ya Championship. Katika misimu ya hivi karibuni klabu hiyo ilicheza michezo ya Play offs ya kufuzu ligi kuu mara 3 na zote wamejikuta wanatolewa kwenye hatua hiyo. Katika msimu huu klabu ya Pamba imeweza kufuzu na kuingia ligi kuu baada ya kuvuna pointi 67 ambazo zilipatikana ndani ya mechi 30 ambazo walizocheza.
Safari ya kufuzu kwa klabu ya Pamba kuingia ligi kuu hauwezi kuizungumzia bila ya kumtaja aliyekuwa mkuu wa Mkoa wa Jiji la Mwanza mheshimiwa CPA Amos Makala. Bwana Makala alipoingia madarakani aliweka dhamira ya kuhakikisha klabu hiyo inapanda daraja na alianza na kuiomba mamlaka ya bodi ya Pamba kukabidhi klabu hiyo kwa halmashauri ya jiji la Mwanza. Na akaomba halmashauri iridhie kwamba malipo ya wachezaji na benchi la ufundi isimamiwe na baraza hilo. Zoezi la kukabidhiana uendeshaji wa klabu hiyo ulifikia tamati katika kikao ambacho kilikaliwa mnamo tarehe Julai 14 mwaka 2023
Mheshimiwa Amos Makala kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya mtandaoni alikuwa anatoa kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 2 mpaka 5 kama motisha kwa timu kwa kila mechi watakayocheza na kushinda. Alihakikisha klabu hiyo linachukua benchi la ufundi lenye uzoefu na masuala ya ligi za chini na ushindani wake. Aliwachukua na kuwasainisha mkataba makocha Mbwana Makata na Renatus Shijja ili kuifundisha klabu hiyo na kisha kuipandisha ligi kuu Tanzania bara. Makocha hao wana uzoefu wa kupandisha daraja timu na hatimaye kuingia ligi kuu.makocha hao katika siku za nyuma waliwahi kuzipandisha daraja na kuingia ligi kuu vilabu vya Rhino rangers, Alliance FC na Dodoma Jiji
Katika safari ya kupanda ligi kuu klabu hiyo ilisajili wachezaji wa makamo ambao wana uzoefu mkubwa sana na mashindano ya Tanzania. Walimsajili golikipa mzoefu Shaban Kado ambaye ana uzoefu mkubwa sana kwenye soka la Tanzania. Ikaingia ubia na kampuni ya uuzaji na usambazaji wa jezi na vifaa vya michezo inayofahamika kama vile NetSport ambapo klabu ya Pamba wanapata kiasi cha shilingi za kitanzania 8000 kwa kila jezi ambayo inayouzwa. Mkataba huo umeisaidia klabu hiyo kupata mashabiki maeneo tofauti kwani jezi zao ziliuzika sana na kuvaliwa na wakazi wa maeneo tofauti.
Mkoa wa mwanza umewahi kuwa na vilabu kadhaa katika miaka ya hivi karibuni kama vile Gwambina, Mbao Fc, ambazo zilikuwepo katika ligi kuu lakini zikashindwa kubaki na hatimaye zikashuka daraja. Kwa upande wa ukanda wa ziwa tunaona vilabu kama Stand United, Mwadui, biashara United navyo vilipanda ligi kuu na havikuweza kukaa sana vikajikuta vinashuka daraja.
Klabu ya Pamba kama itajipanga vizuri basi inaweza ikapata mafanikio kama ambayo waliyapata klabu ya Leicester city mnamo mwaka 2015. Klabu hiyo ilikuwa imeshuka daraja kwa miaka mingi na hatimaye ikapanda ligi kuu mnamo mwaka 2014 na mwaka uliofuata ikashangaza ulimwengu mzima wa soka kwa kubeba kombe la ligi kuu ya England.
Halikadhalika klabu ya Pamba inapita mapito ya Leicester kwani klabu hiyo nayo imekaa miaka mingi katika madaraja ya chini na ikajipanga kidogo kidogo mpaka kufikia hatua ya kupanda ngazi na kuingia ligi kuu. Leicester ilipoingia ligi kuu haikusajili mastaa sana na ilitumia wachezaji ambao hawakuwa wa bajeti kubwa sana na matokeo yake wakapata matokeo makubwa na halikadhalika klabu ya Pamba haijatumia gharama kubwa sana kwenye usajili na inatarajiwa itasajili wachezaji wa gharama za kawaida ambao wataleta matokeo mazuri.
Klabu ya Pamba ina mtaji mzuri wa mashabiki ambao wengi ni wakazi wa mkoa huo na kama wakijipanga vizuri kihamasa basi mikoa yote ya kanda ya ziwa wanaweza kujikuta wanaishabikia klabu hiyo na hilo litakuwa ni jambo lenye faida kwao hususani katika mechi za nyumbani ambazo huwa zinahitaji nguvu kubwa za mashabiki.