Mahakama Kuu ya Afrika Kusini imeamua kwamba mwanariadha mwenye ulemavu wa mguu, Oscar Pistorius hakumuua mpenzi wake, Reeva Steenkamp kwa kukusudia.
Jaji Thokozile Masipa amesema Alhamisi hii kwamba waendesha mashitaka wameshindwa kuthibitisha kwamba mwanamichezo huyo mashuhuri alimuua mpenziwe kwa kudhamiria.
Jaji Masipa ambaye ni mwanamke alipotoa tamko hilo, Pistorius (27) alibubujikwa machozi, japokuwa alisema kwamba alichukua hatua haraka mno kufyatua risasi, hivyo kuonesha wazi kwamba alifanya uzembe.
Mahakama ilikuwa ikitoa mwelekeo wa hukumu yake kutokana na hoja za pande mbili – ule wa mashitaka na wa utetezi, na Ijumaa hii itaweka bayana mbivu na mbichi, ikiwa atatiwa hatiani kwa kuua bila kukusudia au la na kama kuna adhabu ni ipi atakayopewa.
Kabla ya kuahirisha shauri hilo hadi siku ya mwisho Ijumaa hii, Jaji Masipa alisema japokuwa hakuua kwa kukusudia, mtu yeyote makini hangefyatua risasi.
Jaji alisema pia kwamba katika utetezi wake Pistorius alikuwa akiteleza lakini hamaanishi kwamba ana hatia yoyote.
Akimsafisha dhidi ya mashitaka ya kuua kwa kukusudia, Jaji Masipa alisema hangeweza kufikiria kuua mtu yeyote aliyekuwa nyuma ya mlango wa choo.
Pistorius amekana kumuua kwa kukusudia mpenziwe katika siku ya wapendanao, akisema alidhani ni jambazi amemvamia nyumbani kwake.
Anakabiliwa na mashitaka mawili, mawili ya kufyatua risasi hadharani na moja la kumiliki silaha kinyume cha sheria. Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Machi 3 mwaka huu.
Angetiwa hatiani kwa kuua kwa kukusudia angefungwa jela miaka 25, na sasa akitiwa hatiani kwa kuua bila kukusudia anaweza kwenda jela kwa kati ya miaka 10 hadi 15, uamuzi unaotolewa Ijumaa hii.