*Arsenal wanamtaka Bender, Man U Vidal
*Rodriguez anauzwa Madrid kwa pauni 63m
*Atletico wamtaka Mandzukic, Lukaku hoi
Liverpool wamekubaliana na Lille ya Ufaransa na sasa watamsajili mshambuliaji wa kati, Divock Origi.
Hizo ni hatua za kuziba pengo la Luis Suarez anayetarajiwa kujiunga na Barcelona ya Hispania. Liverpool pia wanamfukuzia winga wa Serbia anayekipiga Benfica, Lazar Markovic.
Liverpool watalipa ada ya pauni milioni 10 tu kwa Origi mwenye asili ya Kenya anayechezea Timu ya Taifa ya Ubelgiji na watajadiliana naye juu ya mshahara na marupurupu wiki hii.
Markovic anatarajiwa kuwagharimu pauni milioni 25, fedha zitakazotokana na mauzo ya Suarez huko Barcelona kwa pauni zaidi ya milioni 60.
Barca wanataka kulipa pauni milioni 63 lakini Liverpool wanasisitiza kwamba lazima wakohoe pauni milioni 75.
Wangelipa pungufu iwapo Barcelona wangewapa winga wao machachari wa Chile, Alexis Sanchez katika dili hilo hilo, lakini Sanchez anakataa kubadilishwa jinsi hiyo na anataka kwenda klabu nyingine lakini Kocha Brendan Rodgers hajakata tamaa ya kumpata ila anasubiri kusikia kutoka kwake.
Liverpool bado wamekataliwa na Southampton juu ya kumchukua beki wao, Dejan Lovren licha ya kuweka mezani dau la pauni milioni 20.
Liver wameshakamilisha usajili wa mshambuliaji
Rickie Lambert (32), kiungo Adam Lallana (26) wote toka Southampton kwa ada ya pauni milioni 29 kwa pamoja.
Kiungo wa Timu ya Taifa ya Ujerumani ya vijana,
Emre Can (20) naye ameshajiunga Anfield akitoka Bayer Leverkusen kwa ada ya pauni milioni 10.
Arsenal wameweka mezani dau la pauni milioni 34 kunasa saini ya Sanchez lakini Barca wanasubiri kuona kama Juventus ya Italia watapandia dau hilo kabla ya kukata shauri.
Arsenal pia wamerudi tena Bayer Leverkusen na ‘posa’ ya kiungo Lars Bender (25) huku Mathieu Debuchy (28) wa Newcastle akitarajiwa kufanya vipimo vya afya Arsenal wiki hii.
Manchester United wameambiwa lazima waongeze ofa ili kumpata beki wa Feyenoord, Daryl Janmaat (24).
Wakati huo huo, winga wa Man U, Nani (27) huenda akajiunga na Juventus huku man U wakimpata kiungo Arturo Vidal kutoka Torino.
Southampton wanataka kumsajili kipa wa Cardiff, David Marshall (29), huku bosi wa Vardiff,
Ole Gunnar Solskjaer akimpa ruhusa nahodha Steven Caulker (22) kuamua mwenyewe iwapo anataka kubaki au kujiunga na Queens Park Rangers (QPR) ya Harry Redknapp.
Ashley Cole aliyemaliza mkataba wake na Chelsea anaendelea na mazungumzo na klabu kadhaa za Ulaya juu ya kusajiliwa, na anataka kucheza Ligi ya Mabingwa ya Ulaya (UCL).
Hull City wapo katika nafasi nzuri kuwazidi nguvu Crystal Palace, QPR na West Ham kumsajili beki wa Tottenham Hotspur, Michael Dawson.
Mshambuliaji wa Chelsea, Romelu Lukaku asiyependwa na Jose Mourinho amesema anatafakari kabla hajafikia uamuzi juu ya klabu ya kuchezea msimu ujao na si kutolewa kwa mkopo kule wazee wa Stamford Bridge wanakopenda tu.
Monaco ya Ufaransa wamesema wanataka kumsajili kiungo wa Newcastle, Moussa Sissoko anayewaniwa pia na Liverpool.
Arsenal, Spurs, Napoli na Borussia Dortmund wanafukuzana kwa ajili ya kumsajili kiungo Mfaransa wa Saints, Morgan Schneiderlin (24).
Liverpool wanatafuta mahali pa kumuuza beki wao Daniel Agger (29) na wamewauliza Barcelona kama wangependa kumsajili.
Manchester United na Paris St-Germain wanapigana vikumbo kupata saini ya winga wa Barcelona anayeuzwa, Angel di Maria.
Kiungo mshambuliaji wa Manchester United, Marouane Fellaini (26) anayepigwa bei na kocha Louis van Gaal anatarajiwa kujiunga na
Fiorentina.
Atletico Madrid wanataka kumnunua mshambuliaji wa Manchester City, Alvaro Negredo (28) kuziba pengo na Diego Costa anayekwenda Chelsea.
Atletico pia wanafikiria kumnunua mshambuliaji wa Bayern Munich, Mario Mandzukic (28) kwa pauni milioni 14.
Monaco wamewaambia Real Madrid walipe pauni milioni 63 kama wanataka kumpata kiungo mshambuliaji wao, Mcolombia James Rodriguez (22).
Kipa mkongwe wa Colombia, Faryd Mondragon (43) ametangaza kustaafu soka baada ya timu yake kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia na Brazil.
Rais wa AC Milan ambaye pia ni mmiliki, Silvio Berlusconi ameeleza wasiwasi wake kwamba hatapata dau la kufaa kwa mshambuliaji wake, Mario Balotelli aliyekuwa anatakiwa na Arsenal kabla ya Italia kutolewa kwenye Kombe la Dunia.
Kocha wa zamani wa Swansea, Michael Laudrup anayefundisha klabu ya Qatar ya Lekhwiya amesema anataka kumsajili kiungo mkongwe wa Barcelona, Xavi Hernandez mwenye umri wa miaka 34.