Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjær amesema licha ya wachezaji wake kuanza wakiwa ‘wamepoa’ msimu huu, ana imani kwamba watawasha moto siku zijazo, hasa eneo la ushambuliaji.
Ole akasema kwamba wapo vizuri kama timu, lakini bado washambuliaji wanatakiwa kuongeza kasi na ubunifu, hasa katika kumalizia mipira nyavuni kama alivyokuwa akifanya yeye zama akicheza hapo Old Trafford.
Akasema kwamba washambuliaji wanatakiwa kujinoa na kuwa na kumaliza kiu ya mabao na kwamba kama timu hawajakosa kujiamini licha ya mwanzo usiokuwa mzuri sana wa msimu kwao. Anataka washambuliaji wake, ambao ni chipukizi wasiokuwa na mchezaji mwandamizi kuwaongoza, wafanye kazi yao na ana imani watafanikiwa.
Baada ya kuwatoa Romelu Lukaku na Alexis Sanchez kwa Inter Milan wa Italia, Man United sasa wanaongozwa kwenye mashambulizi na Marcus Rashford, Anthony Martial na Mason Greenwood.
Walianza vyema Ligi Kuu ya England (EPL) kwa kuwakung’uta Chelsea mabao manne, lakini mechi zilizofuata wakatoa sare mbili na kufungwa moja hadi wakienda kwenye mapumziko kupisha mechi za kimataifa.
Ole anakiri kwamba kikosi chake ni chepesi kwenye shambuliaji lakini baada ya muda si mrefu vijana watakuwa wameiva kwa majukumu yao. Martial hakusafiri kwa ajili ya mechi ya wikiendi iliyopita walikoambulia sare dhidi ya Southampton kutokana na majeraha, lakini Greenwood (17) alicheza vyema akitoka benchi, huku Daniel James (21) akiwa ndiye mfungaji wao.
“Tunatengeneza nafasi, tunatengenezea wapinzani wetu shinikizo, sasa ni juu yay ale mabao ya kushitukiza. Tunao wachezaji wadogo na wanatakiwa kujifunza namna ya kufunga mabao yale ya kuudhi kama nilivyokuwa nafanya,” akasema kocha huyo.
Anaongeza kwamba ana uhakika Rashford na Martial wataendana na shinikizo lililo juu yao kwa ajili ya kuipatia klabu mabao kutokana na kutokuwapo wale washambuliaji waandamizi. Anasema wana miaka mingi kwenye klabu hiyo tangu wakiwa wachanga na hivyo anawatarajia wa nyota ongozi.
Ole anasema wachezaji wanaona na wanajua kipi kinahitajika kutokana na hali waliyokuwa nayo uwanjani kwenye mechi tatu zilizopita. Kwamba wamekuwa wakitawala mechi hizo lakini sasa cha muhimu ni kuwa wanapata ushindi na wajue jinsi ya kufanya hivyo.
Beki wa kati Mwingereza aliyesajiliwa msimu huu Old Trafford, Harry Maguire, alikubaliana na kocha wake, akisema wanatakiwa sasa kuonesha ukali kwenye ushambuliaji kwa sababu tayari kwenye ulinzi wapo vizuri, isipokuwa mbele kukiharibika wapinzani wao wanatumia fursa hiyo kuwaadhibu.