Menu
in , , ,

Nyumba ya De Gea mnadani

*Manchester wapandisha dau lake
*City sasa wamgeukia Fabian Delph

Wakati kukiwa na dalili za kipa chaguo la kwanza wa Manchester United, David De Gea kuhamia Real Madrid, nyumba aliyoishi na familia yake Manchester inapigwa mnada.

De Gea, mzaliwa wa Madrid na aliyepata kuchezea Atletico Madrid alikuwa akiishi kwenye nyumba iliyo eneo la Altrincham kwa malipo ya pauni milioni 2.75, na tangazo la mnada huo wakati mwenyewe akiwa likizo linakoleza habari za kuhama kwake.

Tangazo la mnada wa kasri hilo lilianza kutundikwa kwenye mtandao wa Rightmove Jumatano hii na tangu hapo Manchester United wameonesha kushikilia mpini dhidi ya Real, kwani wanasema wapo tayari kumwona De Gea akiondoka bure msimu ujao.

Wanasema kwamba ikitokea watamuuza De Gea, 24, itabidi Real wavunje rekodi ya makipa wote duniani. Mkataba wake unamalizika msimu wa kiangazi mwakani na hajaamua kuzungumzia hatima yake Old Trafford, licha ya klabu kumpa ofa ya mkataba mnono.

Kipa anayeshikilia rekodi ya kuuzwa kwa dau kubwa zaidi ni yule wa Juventus na Timu ya Taifa ya Italia, Gianluigi Buffon waliyemnunua kwa pauni milioni 32.6m kutoka Parma miaka 14 iliyopita.

United pia wanajaribu kuwatega Real, ili wakitoa ofa ya kumtaka De Gea nao wawaite mezani ili beki wa kati wa Real, Sergio Ramos aingizwe kwenye makubaliano baina ya klabu mbili hizo, hasa wakati huu ambapo Ramos anataka kuondoka Real.

Klabu hiyo imekataa dau la pauni zaidi ya milioni 30 lililotolewa na United, na sasa kuna habari kwamba wakazi hao wa Santiago Bernabeu wanafanya kila njia kumshawishi Ramos abaki, ikiwa ni wiki kadhaa tangu aeleze waziwazi kukasirishwa kwake na kufukuzwa kwa kocha wao, Carlo Ancelotti.

Kwingineko, mshambuliaji wa kati wa Man United na nahodha wa zamani wa Arsenal, Robin van Persie, 31, amesema kwamba hatima yake katika klabu hiyo itaamuliwa na mkewe, Bouchra.

RVP naye amebakiza msimu mmoja tu kwenye mkataba wake na kocha Louis van Gaal amemwambia itabidi apandishe kiwango chake zaidi ili afikiriwe kupata namba msimu ujao. Amekuwa akihusishwa na kuhamia ama Italia au Uturuki.

Manchester City wanaandaa pauni milioni 10 ili kumsajili kiungo wa Fabian Delph, 25, kwani mkataba wake unasema anaweza kusajiliwa na klabu nyingine ikiwa itatoa kima hicho cha fedha.

Wakati huo huo, Villa wamekataliwa dau lao ‘dogo’ kumsajili kipa wa Stoke, Asmir Begovic, wafinyanga vyungu hao wakisema kwamba kipa wao thamani yake ni kuanzia pauni milioni nane kwenda juu.

Tottenham Hotspur wanafikriia kutoa dau la pauni milioni saba kwa Everton ili kumnasa winga wao kutoka Ubelgiji, Kevin Mirallas, 27, aliyebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, na ni bora Everton wakamuuza kuliko aondoke bure msimu ujao.

Kwa upande wao, Everton wanaendelea kumfuatilia kwa karibu kiungo wa Manchester United, Adnan Januzaj, 20,kiangazi hiki, baada ya kuulizia juu ya uwezekano wa kumpata kwa mkopo Januari. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji alicheza mechi 21 tu msimu uliopita.

Arsenal wanapanga kumnyakua kinda wa Chelsea, Charly Musonda, 18, anayedhaniwa kuwa na thamani ya pauni milioni saba. Hata hivyo, vyanzo vya ndani vya Arsenal vinaonesha wasiwasi kwamba watazidiwa nguvu na Manchester United kwenye mbio za kumnasa Mfaransa ambaye ni kiungo wa Southampton, Morgan Schneiderlin, 25.

Spurs wameanza mazungumzo na Chelsea juu ya uwezekano wa kumsajili kiungo wao, Victor Moses, 25, anayetarajiwa kuondoka Chelsea majira haya, baada ya kutolewa kwa mkopo msimu uliopita.

Swansea wanahusishwa na mchezaji wa kimataifa wa Ureno, Eder, 27, aliyefunga mabao 10 akiwa Sporting Braga msimu uliopita. Sunderland wanataka kurudi West Ham na dau kubwa zaidi ili kumnasa winga Stewart Downing, 30, baada ya kudaiwa kwamba dau la awali la pauni milioni tano lilikataliwa.

Sunderland wametoa dau la pauni milioni nane kwa mshambuliaji wa Dynamo Kiev, Jeremain Lens, 27, aliyepata kufanya kazi chini ya kocha wa sasa wa Sunderland, Dick Advocaat enzi za PSV.

Klabu ya Uturuki, Galatasaray wameonesha nia ya kumsajili mshambuliaji Mjerumani wa Arsenal, Lukas Podolski, 30, aliyeshindwa kuwika Emirates na kumalizia msimu uliopita Italia kwa Inter Milan.

Kiungo wa Manchester City, Yaya Toure, 32, amebadilika tena, safari hii akisema kwamba nataka kumalizia maisha ya soka akiwa Etihad ili awe na hadhi kubwa kama alivyo Paolo Maldini huko AC Milan. Maldini alicheza hadi akafikisha umri wa miaka 40. Toure na wakala wake wamepata mara kadhaa kueleza nia ya kuondoka Man City.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version