Ipo miamba mingi ya soka imewahi kutamba na kuporomoka. Ilikuwepo Leeds United, West Ham United, Nottingham Forest, Aston Villa kwa kutaja chache, lakini katika nyakati hizi hakuna timu kati zilizotajwa hapo juu yenye uwezo wa kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England. Katika timu zilizokuwa zikifanya vizuri Manchester United ilikuwa miamba ambayo inatetemesha kila mgeni aliyewasili kwenye dimba la Ol Traford.
Haikuwa rahisi kuona Manchester United inayumbishwa na timu kama Brenford au Brighton. Lakini nyakati za sasa uwanja wa Old Traford hauogopwi. Tangu mwaka 2013 hadi leo hali imekuwa mbaya. Wamepita makocha wakubwa na wenye weledi wa hali ya juu kuanzia Louis van Gaal hadi Jose Mourinho lakini ule utemi wa Manchester United haukuwahi kuoneshwa tena kama zama za Sir Alex Fegurson.
Kwa kipindi cha miaka 26, Alex Ferguson aliifanya Manchester United kuwa klabu ya kuogopeka EPL. Man Utd ilishindana na timu kama vile Arsenal, Chelsea na Liverpool. Bahati ilivyo mbaya kwao ule umwamba wa Man United umekuwa kama ndoto isiyotarajiwa tena na ilitamkwa hadharani na kocha wake Erik Ten Hag. Hivi sasa Man United inajivunia mataji ya FA katika misimu miwili ya Kocha Ten Hag, sio ile timu iliyokuwa ikitetemesha vigogo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hakuna mfungaji bora
Klabu ya Manchester United ilipata kuwa na washambuliaji mahiri. Kuanzia Rud Van Nistelrooy,Andy Cole,Dwight Yorke,Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney. Didi Berbatov na wengineo, lakini hali ya Manchestewr tangu kuondoka kwa Alex Ferguson haijawahi kurudisha makali yake. Hivi karibuni nimesoma takwimu za mshambuliaji kama Andy Cole, ambaye aliwahi kuchachafya timu mbalimbali EPL akiwa na mwenzake Dwight Yorke waliifanya Manchester United iwe timu isiyofaa kukutana nayo kwenye mashindano. Andy Cole katika msimu wa 1998/1999 alikuwa mfungaji bora wa EPL na Ligi ya Mabingwa.
Hali kadhalika ndiye alikuwa mtoa pasi nyingi za mabao wa Ligi ya Mabingwa na EPL, na akapachika mabao 48 kwa msimu mmoja na zawadi kubwa aliyopata ni kutwaa mataji matatu katika msimu huo. Huo ndiyo msimu ambao Man United walitamba kuchukua mataji matatu rekodi ambayo imekuja kuvunjwa na majirani zao Manchester City msimu uliopita. Bahati mbaya Andy Cole hakupenya hata kwenye tatu bora za kutwaa tuzo ya Ballon dOr. Kwa sasa Manchester United hakuna mshambuliaji mwenye hazina angalau nusu ya kile alichokifanya Andy Cole kwa msimu mmoja. Hakuna mshambuliaji mwenye hadhi ya kuwapa mabao 20 kwa msimu mmoja. Nyakati zimekwenda wapi?
Hakuna beki bora
Wameondoka akina Nemanja Vidic, Rio Ferdinand, Wes Brown, Patrice Evra, na wengineo. Hivi karibuni John Evans alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo wa EPL akiwa na umri mkubwa zaidi kuliko mabeki waliopo kikosini. Kwa umri wa Johny Evans kutwaa tuzo hiyo ambapo haijachukuliwa kwa muda mrefu na mabeki wa Man United ni ujumbe kuwa nyakati zimepita na hakuna mwingine mwenye uwezo wa kuchukua.
Ule umahiri wa mabeki wa Manchester United umeadimika kama sio kuzikwa kabisa. Mabadiliko ya mifumo si sababu pekee ambayo inaweza kutumika kudai mabeki lazima wawe ‘uchohoro’, lakini ukweli unabaki kuwa hakuna beki mahiri katika kikosi cha Man Utd badala yake wapo wale wa wenye viwnago vya wastani nap engine hawana hadhi ya kuchezea timu hiyo.
Uthibitisho wa kutokuwa na mabeki wa maana ni pale Man United ilipompigia simu na kumrudisha John Evans ambaye waliachana naye muda mrefu kwa madai amepitwa na wakati au kukosa kiwnago cha kuichezea timu yao, lakini sasa mambo yamebadilika. Ukitazama vikosi vya wiki vinavyotolewa katika ligi ya England ni adimu kuona mabeki wa Man United wakiorodheshwa kuwa miongoni mwao. Hakuna Gary Neville na Phil Neville mweingine. Nyakati zimekwenda wapi kwa timu hii?
Hakuna mchezaji bora
Tuzo ya mwisho ya mchezaji bora wa Ulaya kwa Manchester United ilichukuliwa na Cristiano Ronaldo mwaka 2008. Ronaldo alichukua tuzo akitoka kuwa bingwa wa UEFA. Umahiri wake ulikuwa wa kutajika, na alijizolea wimbi la mashabiki. Hata hivyo kikosi cha sasa cha Man United hakunja mchezaji ambaye anaweza kufikiriwa kuwa atakuja kunyakua taji la mchezaji bora wa mwaka wa Ulaya. Nyakati zimewaacha nyuma, hawana umahiri tena wala kutamba.
Wepesi sokoni
Aina ya wachezaji wanaosajiliwa na Man United ni wale wanaokuja kuziba mapengo sio kuendeleza mradi wowote unaofanyiwa kazi. Usajili wa Raphael Varane, Carlos Casemiro na Hodjblund ni uthibitisho kuwa timu ilikuwa inaziba mapengo badala ya kujenga timu imara. Ni kama vile wachezaji mahiri wanakwepa kujiunga na Man United na kwmaba hawataki kuichezea timu hiyo. Katika soko la usajili Man United hawatambi tena. Hawana ubavu na hawaonekani kushindana katika manunuzi ya wachezaji mahiri hata kama itaasemwa wametumia pauni milioni 400 na ushee. Wachezaji mahiri wengi wamesajiliwa na timu zingine, lakini Man United ni wepesi sokoni.
Viungo adimu
Hakuna kiungo mwenye moyo kama wa Roy Keane, David Beckham,Paul Scholes, Nik Butt na wengine wa kaliba yao. Katika safu ya kiungo wachezaji waliopo ni wale wa kawaida. Ingawaje Man United wamejitahidi kuzalisha kipaji cha Kobi Mainoo lakini bado timu inahitaji mapinduzi makubwa kwenye eneo hilo. Kobi Mainoo bado ni chipukizi hivyo anahitaji wachezaji wenye sifa kubwa umahiri kumzidi ili aendelezwe. Viungo wenye roho ngumu, hakuna. Viungo wenye umahiri na ubunifu wa hali ya juu pamoja na moyo wa upiganaji hawapo. Timu ya sasa hatazamiki wala kufurahisha.
Manchester United hii ya akina Marcus Rashford ni sawa na kupiga mluzi huku unatafuna karanga. Imekuwa timu iliyoshuka viwango na kujivunia ‘vitaji vidogo’ kama FA huku ikiona ugumu kunyakua EPL na kudhani ‘hawana hadhi’ ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.Nyakati zimekwenda.