Barca vs Bayern, Real Madrid vs Juve
Droo ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) imezikutanisha timu mbili ambazo kocha Pep Guardiola anazijua barabara.
Bayern Munich wanaofundishwa na Guardiola watavaana na Barcelona ambao Mhispania huyo amewafundisha na kuwapa makombe 13 ukiwamo ubingwa wa Ulaya.
Real Madrid kwa upande mwingine, wamepewa ile baadhi ya wachambuzi wanayoona ni timu isiyo ngumu kama nyingine – Juventus.
Juventus wamefika hatua hii kwa mara ya kwanza tangu 2003 na sasa watawajaribu mabingwa watetezi wanaofundishwa na Carlo Ancelotti.
Bayern waliingia nusu fainali kwa ushindi mkubwa wa 6-1 dhidi ya Porto baada ya kuwa wameduwazwa katika mechi ya mkondo wa kwanza kwa kunyukwa 3-1.
Bila shaka mechi baina ya Bayern na Barca itakayochezwa kati ya Mei 5 na 6 itavuta macho na masikio ya wengi zaidi, kutokana na historia ilivyo.
Guardiola amekaa miaka minne Barcelona kabla ya kuondoka na kukaa mwaka mmoja bila kazi, ndipo akarejea na kujiunga na Bayern.
Katika miaka yake sita akiwa kocha Guardiola alifanikiwa kufika nusu fainali ya UCL mara sita, nne akiwa na Barca na mbili na Bayern.
Ancelotti naye atachuanana moja ya timu alizopata kufundisha, kwani alikuwa Juve tangu 1999 hadi 2001.
Rekodi zinaonesha kwamba Real waliwafunga Juve katika fainali ya 1989. Droo hii pia inatoa uwezekano wa fainali kukutanisha timu za nchi moja – Barcelona dhidi ya Real ikiwa zitavuka.
Msimu uliopita Real walicheza fainali dhidi ya mahasimu wao wa Madrid, Atletico lakini Madrid na Barca hazijapata kukutana kwenye fainali za UCL kabla.
Msimu huu Real wamefika nusu fainali kwa kuwatoa watani zao hao Atletico kwa bao 1-0. Barcelona walipata ushindi kirahisi kwa kuwapiga
Paris St-Germain (PSG) kwa jumla ya mabao 5-1.
Juventus waliwatoa Monaco kwa 1-0. Fainali za mwaka huu zitafanyika Juni 6 katika Dimba la Olimpiki jijini Berlin.
Katika nusu fainali ya Ligi ya Europa, mabingwa watetezi Sevilla wa Hispania watacheza na Fiorentina wa Italia, wakati Napoli nao wa Italia na wanaofundishwa na Rafael Benitez watachuana na Dnipro wa Ukraine.
Nako kuna uwezekano wa fainali kukutanisha timu za Serie A ya Italia.
Mechi za mkondo wa kwanza zitafanyika Mei 7 na marudiano wiki moja baada. Fainali itafanyika Mei 27 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Warsaw, Poland.