Huenda ikawa mechi ya kisasi baina ya Yanga na Simba kuelekeaa katika nusu fainali michuano ya ‘Azam Sports Federation Cup’ (ASFC).
Mchezo wa Azam dhidi ya Simba unachezwa saa moja leo kwa saa za Afrika Mashariki, na mshindi wa hapo moja kwa moja atakutana na Yanga iliyotangulia nusu fainali baada ya kuifunga Kagera Sugar mabao 2-1.
Katika ligi, Yanga walimaliza kwa kuifunga Simba goli 1-0 goli lililofungwa na Morrison ambaye taarifa zinasema amefukuzwa kambini kutokana na utovu wa nidhamu kwa timu yake.
Huku habari zikienea kuwa alitaka kutoroka na akakamatwa na walinzi akiwatishia mambo mbalimbali.
Tuanchane na Morrison, leo mchezo utakuwa mgumu na wa aina yake, hamu iliyopo Simba kuingia nusu fainali ili kuwakwaa Yanga kwa mujibu wa shabiki wa Simba baada ya matokeo ya jumanne ya Yanga.
Kwa umuhimu wa hiyo mechi vichwa vya habari vitakuwa vinasema kufa au kupona ‘Do or Die’ kwakuwa lazima mshindi apatikane.
Wakati Yanga na Simba zilivyotoka sare ya kufungana magoli 2-2 mzunguko wa kwanza yaliibuka maneno kwa upande wa Simba yakisema kuwa wanataka kujua Yanga waliitolea wapi sare.
Ila baada yamchezo wa pili Yanga kushinda nao wakaja na maneno kuwa sare ilikua ya shughuli ambayo imehitimishwa katika mchezo wa pili ambayo ilikuwa Machi 8 siku ya wanawake duniani.
Hivyo ni raha kuona timu hizi zikikutana ili kumaliza ubishi na kutambiana hadi itakapokutana tena.
Azam FC nayo ina nafasi ya kutinga nusu fainali kwani timu hiyo iliiadhibu Yanga katika mzunguko wa kwanza ligi kuu Tanzania Bara kwa goli 1-0 hivyo itakuwa kisasi cha aina yake kama ikipita na kukutana na Yanga nusu fainali.
Yaani nusu fainali hii itakuwa ya visasi kwa timu zote yaani yoyote itakayopata kupita katika hatua hiyo basi itataka kulipa kisasi.
Yanga dhidi ya Azam mchezo wa pili ilitoa sare bila kufungana hivyo kitawaka sana kule Sumbawanga kutakapopigwa fainali ya michuano hiyo.
Kuna hatua ambazo timu zikifika huwa zinakuwa tamu sana kwani fainali itawakutanisha hawa wa leo dhidi ya Ndanda v Sahare na Namungo ambayo tayari imetinga hatua ya nusu fainali.
Turudi katika mchezo wa robo fainali Yanga dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mchezo ulikuwa mzuri kwa pande zote mbili hasa Kagera walionesha kandanda safi kabisa la kufundishwa.
Waliweza kupiga pasi ya viwango vya hali ya juu huku kila aliyekuwa anatazama mchezo huo aliamini kuwa kweli walifundishwa na wakafundishika.
Makosa ya muamuzi wa mchezo huo yaliharibu radha ya mchezo wenyewe.
Matukio matatu ambayo yaliharibu mchezo huo ni pamoja, na kutotoa penati wakati mchezaji wa Yanga Feisal Salum ‘Fei toto’ alipoangushwa eno la hatari, tukio la pili ni kuwanyima penati Kagera Sugar wakati mchezaji wao alipokatwa mtama, dhahiri na Metacha Mnata.
Huku tukio la mwisho bado halijatolewa ufafanuzi ila kutoa kadi nyekundu kwa Aweso Aweso wengi wanahisi alitukana japo haijathibitishwa.
Matukio ya kuvutia katika mchezo huo timu nzima ya Kagera Sugar ilicheza kwa kujitolea yaani kama unagawa maksi ‘Marks’ basi wote watapata 8/10 wakati Aweso Aweso ataibuka na 9/10 kwa kuonesha kandanda safi.
Kagera Sugar walitulia na walijua kuwa wanakutana na Yanga yenye wachezaji wazoefu hivyo walijipanga kwa hali na mali pamoja na kiakili.
Yanga walionesha mchezo mzuri, ndio maana katika umiliki wa mpira ilikuwa asilimia 47 kwa timu nzima kwa kugawa maksi tunawapa 6/10 huku David Molinga yeye akipata 7/10.
Muamuzi yeye anapata 4/10 kwa aina ya uchezeshaji wake na kuonekana kutaka kupoteza radha ya mpira wenyewe.
Unaweza kutuambia kupitia maoni yako hapo chini juu ya mhezo ule wewe ungetoa ‘Marks’ maksi ngapi ?