Ni mchezaji ambaye kila mpenda soka alitamani kumwangalia namna anavyowachachafya mabeki wa timu pinzani..
WAKATI akisajiliwa kuichezea Simba, Yusuf Mhilu alikuwa ametokea klabu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera. Ni miongoni mwa timu zinazotoa changamoto kwa vigogo wa Soka. Yusuf Mhilu ni mchezaji ambaye huwezi kumpuuza kila umwonapo dimbani, lakini katika usajili wake Simba hajadumu wala kufurukuta.
Hali hiyo inazidisha maswali ni kwa namna gani wachezaji wazawa wanashindwa kupenya katika kikosi cha timu kama Simba. Ukimwangalia Yusuf Mhilu, ana miguu ya mpira, kipaji anacho, kasi anayo, ukokotaji wa mpira anamudu, kuwazidi maarifa wapinzani wake anaweza.
Kila anapokuwa na mpira unaweza kukisia kuwa ipo hatari inakuja kwa timu pinzani. Alipokuwa nyota wa Kagera Sugar alikuwa ndiye mtu unayempatia mpira aiongoze timu. Ni kama baadhi ya timu za Ulaya iwe klabu au Taifa wapo wachezaji ambao hukabidhiwa majukumu ya kuibeba timu. Ingawaje misfumo inabadili mambo mfano Pep Guardiola anavyoondoa utegemezi wa mchezaji mmoja, lakini bado anategemea akili binafsi za wachezaji.
Ingelikuwa Taifa Stars miaka ya nyuma ungeona mashabiki wakidai ‘mpe pasi’ Salvatory Edward atajua cha kufanya. Ama mashabiki wa Simba walivyozoea kulalamika pale Joseph Kaniki ‘Golota’ kama hakupewa pasi ndani ya 18 au eneo la hatari. Ni vile ambavyo wangelalamika kuona Emmanuel Gabriel hajapewa pasi akiwa eneo zuri la lango la adui.
Ilikuwa rahisi kujua mpira mpe Christopher Alex Masawe atajua namna ya kupanga mashambulizi kutoka eneo la ukabaji. Simba ya sasa unaweza kusema ‘mpe pasi Chama’ kwakuwa ndiye mchezaji ambaye atapanga timu ishambulie namna gani. Wachezaji wa aina hii hutokea timu mbalimbali. Yusuf Mhilu alikuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo Kagera Sugar na alinguruma haswa. Akawa nyota kikosini mwao, mpira ulimkubali na pasi ziliekea kwake.
Angeweza kuwakimbiza mabeki kwa kasi, angeweza kuwalamba vyenga, angeweza kupambana nao kwa nguvu za mwili, angeweza kupiga mashuti mengi langoni mwa adui. Lakini Yusuf Mhilu pia kwa kocha ambaye hakuwa na mshambuliaji kamili angeweza kumpanga kwenye eneo la namba tisa. Eneo hilo linamfanya kocha apate mabao kutoka Yusuf Mhilu, kutokana na kasi yake, nguvu zake na mashuti yake.
Hata hivyo Yusuf Mhilu aliyesajiliwa na Simba hakufurukuta kufanya yote hayo. Matumaini makubwa ya mashabiki kwa Yusuf Mhilu yalikuwa wazi. Hata viongozi wa Simba walitegemea kuwa nyota wao mpya angeweza kuwachachafya wenzake kikosini hasa eneo la mawinga. Yusuf Mhilu alikuwa mmoja ya vipaji vizuri vya wachezaji wazawa waliosajiliwa Simba.
Lakini mwendelezo wake wa kutamba kwenye soka uliishia Simba. Timu ambayo ina ushindani mkali wa namba kutoka kwa wachezaji wazawa hadi wale wa kimataifa. Unakutana na mchezaji ametoka kwao Malawi huko kuja kupambana kwenye kikosi cha Simba. Unakuta timu ina vipaji toka Mali, Senegal, DRC,Kenya na mataifa mengine, ikiwa ni dhahiri kila mtu mchezaji ‘ameaga kwao’. Ushindani wa namba ni kitu cha kawaida kwenye kikosi na ndicho kinawaimarisha wale wanaopangwa kikosi cha kwanza.
Fikiria ule ushindani wa John Bocco, Chris Mugalu na Meddie Kagere, kisha mfikirie kocha wa Simba mwenye wachezaji hao alikuwa analala usingizi kweli? Jibu laweza kuwa hapana au ndiyo. Lakini Yusuf Mhilu alikuwa mchezaji mwenye kila sifa ya kupambana na akina Peter Banda, Pape Sakho, Kibu Dennis na wengine. Mhilu hata alipokuwa anapewa nafasi ya kucheza bado hakuwa Yule aliyewatikisa vigogo akiwa Kagera Sugar.
Si kwamba aliishiwa makali au kipaji chake kutotosha, lakini ushindani huenda umemwondoa Yusuf Mhilu pale Simba. Imani ya mashabiki kuwa angelikuwa nyota na kiwakilishi cha wazawa lakini ilififia. Huyu ni mchezaji ambaye bila kuleta ushabiki alitakuwa kuonesha makali zaidi ya wachezaji wenzake kwenye namba walizogombania. Lakini Yusuf Mhilu hadi ameondoka Simba bado ameacha deni kubwa la kutumia kipaji chake kwa asilimia 100.
Ni mchezaji ambaye kila mpenda soka alitamani kumwangalia namna anavyowachachafya mabeki wa timu pinzani. Mhilu hakuwa mchezaji wa kuibuka kama homa za vipindi, leo amecheza lakini kesho kutwa hachezi. Na huwezi kumlaumu kocha anayemweka benchi kwani anajua kijana hajamfanyia kazi yake. Kwa hakika kila mpenda soka anapofikiria kipaji cha kijana huyo bila shaka yoyote atakuwa na huzuni.
Masikitiko hayo ni kwmaba Taifa Stars inakosa mchezaji ambaye anaonekana kabisa angelileta changamoto kwa wengine kikosini. Lakini hadi sasa haijulikani ni lini Yusuf Mhilu atatikisa tena. Haijulikani ni kwa vipi kipaji chake kitakuwa imara mbele ya ushindani wa wachezaji wa kigeni. Kama ni presha ya kuchezea timu kubwa, basi itawawia vigumu wachezaji wetu wazawa aina ya yusuf Mhilu kuhimili presha ya kucheza soka nje ya nchi.
Bado nakililia kipaji hiki, naamini kina uwezo kuleta faida kwa taifa ikiwa mhusika atatambua hilo. Nafasi anayo, uwezo anao, nguvu anazo, ni jukumu lake kuhakikisha anarudisha kile kilichowanogesha Simba hadi wanamsajili kwenye timu yao. Akirudishe kile, akifanyie kazi sasa ikiwa kimeshuka au kupotea. Hicho ndicho siri yake itakayompa nafasi ya kuchangamana na wachezaji wa kigeni na kujifunza mbinu mpya kuboresha uwezo wake. Yusuf Mhilu, endelea na mapambano.