Asubuhi ya leo nimeamka natamani angalau kuona picha za Dr. Wilboard
Slaa, mwanasiasa ambaye aliwahi kuacha alama kubwa sana kwenye jukwaa
la siasa hapa nchini kwetu.
Mwanasiasa ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa mbele ya jamii.
Mwanasiasa ambaye alikuwa anaibua mijadala ya moto hapa nchini kwetu.
Kadri nilivyokuwa nazidi kuangalia picha zake ndivyo moyo wangu ukawa
unatamani angalau nisikie sauti yake .
Nisikie akiongea na kuibua hoja za moto katika kipindi hiki.
Nimsikie akiunguruma kwenye jukwaa la siasa.
Lakini ndivyo hivo matamanio yangu yalikuwa yanazidiwa na ukweli kuwa
Dr. Slaa ashaachana na siasa za Tanzania. Siasa ambazo yeye anaziita
siasa taka.
Hatunaye tena kwenye jukwaa ingawa watu wengi wanatamani jambo kusikia
sauti yake ikiunguruma.
Hakuna mtu asiyependa watu imara, kila kitu imara kwenye maisha ni
chachu ya maendeleo.
Ndiyo maana kila siku tunalilia kuwa na ligi imara katika nchi yetu.
Ligi yenye timu imara, tukiamini kabisa ligi imara, yenye timu imara
inaleta maendeleo makubwa katika soka letu ambalo tunatamani kila siku
lifike mbali.
Wingi wa timu imara huleta ushindani ambao husababisha kumpata bingwa
bora ambaye huwakilisha vyema nchi kwenye michuano ya kimataifa.
Hata timu yetu ya taifa itanufaika kwa sababu wachezaji wetu watakuwa
wanazaliwa kwenye ligi iliyo imara.
Ndiyo maana kila mtu anatamani ongezeko la timu zenye ushindani kwenye
ligi kuu ya Tanzania.
Timu zitakazoleta changamoto mpya kwa timu kubwa ambazo ndizo tumezoea
kuziona zikishindana zenyewe kwa zenyewe.
Wakati Mbeya City inapanda ligi kuu, msimu wake wa kwanza ulikuwa
msimu wa kishindo.
Kwani walifanikiwa kufanya vizuri sana na kuleta ushindani mkubwa sana.
Ushindani ambao ulikuwa na matokeo chanya kwenye ligi yetu.
Wengi wetu tulitegemea kuwa Mbeya City imekuja kuingia katikati ya
Simba na Yanga.
Watu wengi waliiamini, wakaipenda na wakaanza kuiunga mkono Mbeya City.
Wana Mbeya wakasimama kwa pamoja na kuibeba Mbeya City .
Kiwanja cha sokoine kilitapika kila mechi, haikujalisha mechi ya Mbeya
City na timu kubwa au ndogo kwao wao kila mechi ilikuwa na kipimo
sawa.
Waliacha kazi zao iwe jumatano au siku za mwishoni mwa juma.
Walijinyima kwa kidogo ili mradi tu wahudhurie mechi ya vijana wao.
Hawakutaka kuwaacha wapweke Mbeya City, kila uchwao walizidi kusimama
na kuwapigania vijana wao.
Kwao Mbeya City ilikuwa moja ya sehemu ambayo inatoa furaha kwao.
Bila Mbeya City furaha yao ilikuwa haijakamilika.
Walijivunia kuitwa mashabiki damu wa Mbeya City.
Kwao haikuwa hasara kununua jezi na nembo za Mbeya City na kupita nazo mtaani .
Wachezaji wa Mbeya City hawakuwaangusha mashabiki wao kwa kuwapa matokeo mazuri.
Kila mechi kwao ilikuwa fainali walifanya kila iwezekanavyo washinde
ili waweke furaha ndani ya mioyo ya mashabiki wao.
Furaha ndani ya mioyo ya mashabiki ilijaa, mashabiki wakawezekeza
nguvu katika kuiunga mkono timu, timu nayo ikakubali kubebeka.
Miaka imepita, kila kitu kimebadirika pale Mbeya City.
Mashabiki hawana hamasa tena na timu yao kisa matokeo mabovu ya timu yao.
Shabiki hana cha kujivunia tena, vipigo vimekuwa kitu cha kawaida pale
Mbeya City.
Ile Mbeya City ngumu, haipo tena. Kuna Mbeya City laini tu ambayo
imefanya mioyo ya watu wengi kuwa laini na kushindwa tena kusafiri na
timu kila mkoa ilipokanyanga timu kwenda kuishabikia.
Mauzo ya vifaa vya Mbeya City yamepungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu
ya matokeo mabovu ya timu.
Mbeya City ile nimeikumbuka maana hii iliyopo hainipi nafasi ya kuipenda.
Hainivutii kama ile ya Mwanzo ambayo kila Mtanzania hata asiye mwana
Mbeya City alitamani kuwa shabiki wa timu.