Menu
in

Nimefanya safari ya kuvitembelea baadhi ya viwanja maarufu vya timu maarufu hapa Uingereza, moja nililoliona ni Majivu ya wapenzi damu wa timu husika kutawanywa uwanjani kama muhusika aliacha wosia..na kitu cha kawaida tu..

Mara nyingi tumekuwa tukisoma na kusikiliza maelezo kuhusu vilabu maarufu vya soka katika England, hususani vile vinavyoshiriki ligi kuu ya Premiership. Maelezo mengi yanahusu muundo wa vilabu, historia yake, mafanikio na uwezo wa timu katika kushiriki katika mashindano mbali mbali.

 Nilipata nafasi kutoa heshima kwa wale wapenzi wa Liverpool waliopoteza maisha.
Nilianza safari yangu kwa kutembelea Liverpool FC  hii baada ya kupata kibali cha kuingia na kupiga picha ndani ya uwanja na maeneo mengine muhimu ya kihistoria. Uwanja wa Liverpool uko katika mtaa wa ANFIELD.(Anfield Road, Liverpool, L4 0TH).
Baada ya kulipia na kupewa mtu wa kunisindikiza katika “tour” yangu tulianzia sehemu yenye kumbukumbu za walimu waliopita wa Liverpool, Hapa niliona picha za walimu kama Billy Shankly, muasisi wa ari na nidhamu ya Liverpool, kumbuka Shankly ndiye aliyekuja na wazo la kuweka nembo ya Liverpool FC mbele ya mlango wa mwisho wa kuingilia uwanjani kwa timu husika, na sababu kuu ni kuwatisha timu ya ugenini na kuwafanya wapate hofu kabla ya kuingia kwenye mechi, huku timu ya nyumbani ikigusa na kuonyesha nidhamu kwa “THIS IS ANFIELD” ukiangalia kwa karibu utaona alama ya vidole na sugu kwenye hii nembo, kumbuka imekuwepo tangu 1959!.

 Nikiwa katika sehemu muhimu sana kabla ya mechi katika Anfield
Kisha nilionyeshwa chumba chenye kumbukumbu zote za Liverpool Fc, hii ni pamoja na vikombe walivyoshinda kumbuka wakati Shankly anastaafu rasmi miaka 15 baada ya kazi ngumu, aliacha mafanikio ya Ubingwa wa ligi (championships) mara tatu, FA Cups mara mbili, na UEFA Cup.
Baadaye nikaonyeshwa chumba cha mikutano na mahojiano maalumu, mfano Club inapokuwa na hafla ya kumtambulisha mchezaji mpya, basi sherehe fupi hufanyika hapa

.Ndani ya chumba cha timu ya nyumbani
Na ndipo nilipoonyeshwa sehemu iliyonipa wasiwasi kidogo na kushangaa kwa pamoja. Kwa miaka mingi Liverpool FC, ilikuwa na utaratibu kwa wachezaji vijana wanaochipukia kutokea kwenye Academy za Liverpool, kuwasafishia viatu wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Liverpool,  hapa nazungumzia “Boot room”.
Katika chumba hiki walimu na wasaidizi walitumia muda mwingi kunywa chai, huku wakipanga mikakati ya kufanya vizuri kwa muda mrefu kwa timu yao, kumbuka Bob Paisley, Joe Fagan na Roy Evans. Paisley alikuwa na umri wa miaka 15 alipoanza kazi katika Liverpool nakuwa sehemu ya mafanikio ya kuwa bingwa mara sita wa Championships na mara tatu katika ulaya, na hatimaye kuwa mmoja wa  walimu waliopata mafaniko kama kocha wa England.Niliambiwa mara walipoacha huu mtindo wa vijana kuwasafishia viatu wachezaji waandamizi, ndio ukawa mwisho wa kushinda ubingwa wa Enland….Benetez alikuwa akifikiria kuurudisha maana ni imani iliyo hai…kabla hajaondoka.

Kisha nikaonyeshwa vyumba vya wachezaji wa nyumbani na ugenini, hapa nikaona uduni wa vyumba hivi, nikiwa na maana ya madawati ya kukalia, kiti cha kukandia wale wachezaji wanaohitaji massage nk.. nilipouliza niliambiwa sababu kubwa ni kujaribu kuwafanya wachezaji wote wawe sawa wanapokuwa katika chumba hiki na kumfanya kocha kuwa na wakati mzuri wa kuongea na wachezaji huku akiwa na usikivu makini kutoka kwa wachezaji wanaochezea timu moja huku wakilipwa malipo tofauti..

Nikaenda chumba cha wachezaji wageni, hapa nikaona mfano wa jezi za timu zilizowahi kushiriki katika michezo muhimu katika Anfield, cha ajabu ni hii picha ya mfano wa jezi ya Arsenal… kumbuka Liverpool walihitaji kushinda huu mchezo ili wawe mabingwa.. Arsenal wakawa na wazo tofauti…ni kumbukumbu chungu ila ustaarabu ni kitu cha maana sana, wanakubali na ndio maana itabaki kuwa historia kwa Liverpool FC. Pia nikakuta ujumbe wa kocha mkuu wa Liverpool Hodgson kwenye bango la matangazo akieleza jinsi anavyoamini muelekeo wa Liverpool..

 Jezi ya Arsenal ndani ya chumba cha timu ngeni katika Anfield
Kwakuwa hii ni mara yangu ya kwanza kufika katika uwanja huu sikuamini udogo wa sehemu ya kuchezea( Pitch), nilipouliza nikaambiwa ni kweli Anfield ni moja kati ya viwanja vyenye sehemu ndogo ya kuchezea 110X75 YARDS. Viwanja vingine ni Chelsea na Tottenham. kiwanja chenye sehemu kubwa ya kuchezea ni Manchester city 116X77.
Nilipofika ndani ya uwanja nikaona kuna UA katika sehemu ya goli, nilipouliza niakaambiwa ni utaratibu wa kawaida kwa wale wapenzi DAMU kuacha wosia kwamba, mauti yakiwakuta basi majivu ya mabaki ya miili yao yamwagwe uwanjani, kwahiyo siku nilipoenda mimi 13-09-2010.ilitokea hivyo. kwa kutaka kujua zaidi nikaambiwa ni vilabu viwili tu katika Premiership vinavyofanya hivyo, navyo ni Liverpool na Everton… nikajisemea moyoni. hii ikifanyika Kwa Timu zetu, Yanga, Simba, CDA au Mtibwa sijui itakuwaje ukijua hapo unapocheza jamaa unayemfahamu kasambazwa.

 Nje ya Lango kuu lakuingilia makumbusho na dula la Liverpool FC
Nilishangaa ila nikaamini imani za itikadi ni sehemu ya jamii yeyoye mahala ilipo. Kwa Liverpool ni Club kubwa na mambo yake ni makubwa.
Safari yangu ilinipeleka Everton, Stoke city na Wigan…

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version