Menu
in , , ,

Ni Yanga na Azam Afrika

 

*Simba washangilia Yanga lakini…

 

Huku kila timu ikiwa imebakisha mechi moja ya Ligi Kuu Tanzania, tayari wawakilishi wa taifa kwa mashindano ya mwakani wamepatikana.

Mchezo baina ya Yanga na Azam uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa uliotota maji huku mvua ikinyesha ndio ulitoa hatima.

 

Baada ya mechi hiyo Yanga walikabidhiwa kombe la ubingwa waliotwaa kitambo, zawadi na cheti kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Azam walifurahi, kwani walifanikiwa kuwafunga Yanga 2-1 na walikuwa wakihitaji ushindi huo kujihakikishia nafasi ya kushiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho la Afrika (CAF).

 

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, washabiki wa Simba walikuwa wakiwashangilia Yanga ili wawafunge Azam kisha Simba wafuzu Afrika ikiwa wangeshinda mechi ijayo na Azam kupoteza.

 

Kadhalika wanazi wa Simba walikuwa wakituma salamu za kuwatakia Yanga ushindi redioni huku washabiki wa Yanga wakiwashangilia Azam ili Simba wawe fungu la kukosa.

 

Yanga kwa nafasi yao ya ubingwa wataiwakilisha Tanzania kwenye Michuano ya Klabu Bingwa Afrika, baada ya mwaka huu kuwakilisha kwenye Kombe la Shirikisho na kuishia 16 bora.

 

Wakati Yanga wana pointi 55, Azam wamefikisha pointi 48, Simba wakiwa na 44. Kila timu imebakisha mechi moja kabla ya pazia la Ligi Kuu kufungwa rasmi.

 

Hii itakuwa msimu wa tatu mfululizo kwa Wekundu wa Msimbazi kukosa kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa.

 

Yanga kwa upande wao wamenyakuwa ubingwa wa 25 wakati Ligi Kuu ikitimiza miaka 50 tangu kuanzishwa.

 

Tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu ya Tanzania 1965 ni timu tisa tu zimetwaa taji hilo, huku Yanga wakiongoza kutwaa ubingwa zaidi, wakifuatiwa na Simba waliotwaa mara 18.

 

Wengine waliopata kutwaa ubingwa ni Mseto, Pan African, Tukuyu Stars, Coastal Union na Azam waliopokonywa ubingwa na Yanga msimu huu.

 

Wakati tmu tatu zikifurahia juu ya msimamo wa ligi, ipo hatari kwa timu kadhaa kuwa na uwezekano wa kushuka daraja, ikitegemeana na matokeo ya mechi ya mwisho.

 

Timu nyingi zimefungana kwa pointi, ambapo Mtibwa Sugar, Mbeya City, Kagera Sugar, Ruvu Stars na Coastal Union wana alama 31 kila mmoja.

 

Ruvu Shooting wanazo 29 wakati Prisons, Ndanda, Mgambo na Stand United wana 28 kila mmoja na Polisi Morogoro wanazo 25. Uamuzi wa nani anashuka ni Jumamosi hii, timu zote zitakapojitupa uwanjani.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version