KATIKA dakika ya 99, alipokea pasi nje kidogo ya eneo la 18 upande wa kushoto, huku eneo la ulinzi likiwa na mabeki watano. Mabeki watatu walikuwa wana kazi ya kuwachunga wachezaji watatu wa Brazil ambao walikuwa wanamezea mate pasi ambayo ingetoka kwa Vinicius Junior. Katika kiungo cha Colombia kwenye tukio hilo kulikuwa na wachezaji watatu, ambapo wawili walikuwa na kazi ya kuwasaidia walinzi wao watatu, kisha mmoja alikuwa na jukumu la kuchunga eneo la kiungo upande wa kulia.
Vinicius Junior baada ya kupokea pasi ile alikimbia kwa kasi na kumshinda beki wa kulia wa Colombia, hivyo kumruhusu aingie kwenye eneo la hatari.
Kitendo cha kumruhusu kuingia eneo la hatari maana yake alikuwa anamkaribia golikipa wa Colombia. Kwa kasi ileile Vinicius Junior alisogelea zaidi huku akikokota mpira kisha akaachia shuti kali lililioingia moja kwa moja kimyani na kuandika bao la pili kwa Brazil. Bao hilo liliingia katika dakika 99 na sekunde ya 17, kwani ilibaki dakika moja tu mwamuzi kupuliza filimbi ya kumalizika kwa mchezo huo. Katika mchezo huo mwamuzi aliongeza dakika 10 kutokana na kucheleweshwa mara kwa mara.
Katika mfumo wao wa 3-3-4 hakuweza kumudu kasi ya Vinicius. Ushindi huo ulimpa tabasamu kocha wao Dorival Junior ambaye tangu alipochukua kibarua hicho alitangaza shauku ya kucheza mchezo wa fainali ya Kombe la dunia mwaka 2026. Matamanio hayo ndiyo ynasababisha wadau kuzidi kutupia macho kikosi chake na namna wanavyocheza, ikizingatiwa Brazil tangu wlaipofanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2002 hawajafanikiwa kulitwaa tena. Pia mafanikio ya hivi karibuni ni kufika nusu fainali ya Kombe hilo mwaka 2014 ambapo walizabwa na Ujerumani kwa mabao 7-1.
Je ni Vinicius atafunika kivuli cha Neymar?

Kwa umri Neymar Junior anaelekea kwenye kilele cha uchezaji wake wa soka. Kiufundi Neymar Junior ni mahiri kuliko Vinicius, lakini tofauti yao kubw ani kasi. Vinicius ana kasi kubw akuliko Neymar. Vinicius ana nguvu za mwili kuliko Neymar. Ili mabeki wamwangushe Vinicius wanatakiwa kuwenda jimu mara nyingi zaidi. Katika uchezaji wa Vinicius alichoongeza ni nguvu za mwili kwa sababu kasi na ufundi alikuwa navyo tangu alipoibuka kwenye ulimwengu wa soka.
Brazil bado ni tegemezi kwa Neymar.
Timu ya Taifa inapoitwa huwa inatengenezwa kumzunguka Neymar Junior, kwahiyo hata mazungumzo mengi ya wachezaji wa sasa ni kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 ili kumpa furaha Neymar. Kwa Wabrazil kwa sasa Neymar ndiye mchezaji ambaye anaweza kupangua safu ya ulinzi ya timu yoyote sababu ana ujuzi na ufundi mkubwa linapofika suala la maarifa ya kusaka mabao. Kila timu inakuwa na mchezaji wa namna hiyo, lakini si wote wapo kama Neymar.
Brazil wanaongozwa na Neymar iwe anacheza au hachezi, kwani mifumo yao imetengenezwa kumpa ufalme na ushindi kwneye mechi mbalimbali. Ikizingatia Neymar amefanikiwa kuzifikia rekodi za wakongwe kama Pele, Ronaldo De Lima na wengineo hivyo kila njia inafanywa ili aendelee kupanda ngazi. Hata hivyo kwenye fainali hizo endapo atakuwepo ni wazi umri utakuwa unamtupa mkono. Kibarua kigumu alichonacho Vinicius ni kufunika kivuli cha Neymar. Hili ni jukumu ambalo litakuwa na maana ya kuiletea Brazil.
Kuna Rodrygo, Savinho na Raphinha
Unapomaliza kukitazama kikosi cha Brazil, kisha ukaondoa majina ya Vinicius Junior na Neymar, basi yanayokuja ni Raphinha wa Barcelona, Savinho wa Manchester City na Rodrygo wa Real Madrid. Lakini makocha wa Brazil pia wanamtupia jicho Estavao, staa ajaye wa Chelsea pamoja na Endrick wa Real Madrid.
Hii ina maana Brazil wanakuwa wameongeza na kupata nafuu ya upana wa kikosi chao. Wachezaji vijana wenye kasi, na nguvu, maarifa na ujuzi mkubwa wakiwa wanachezea vilabu vikubwa wanaelekea kuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Brazil. Katika majina haya matatu, wote wanaweza kucheza katika nafasi za Neymar na Vinivius. Hii ina maana kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2026 Brazil wanazidi kutengeneza kikosi cha vijana ambao wenye vipaji vya hali ya juu. Je vijana hawa wanaweza kukifunika kivuli cha Neymar Junior? Ni suala la kusubiri na kuona.