Menu
in , ,

Ni Vigil van Dijk

Tanzania Sports


*Mchezaji bora wa Ulaya, beki kisiki Liver

*Amezima ukiritimba wa Ronaldo na Messi

Mlinzi wa kati wa Liverpool, Virgil van Dijk ndiye mwanasoka bora wa mwaka wa Ulaya, akikatisha zama za ukiritimba wa akina Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Van Dijk alichangia kwa kiasi kikubwa Liverpool kuwafunga Tottenham Hotspur 2-0 kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) jijini Madrid Juni mwaka huu.

Jina lake lilitangazwa na kukubaliwa na wengi kwenye hafla iliyofanyika jijini Monaco Alhamisi hii, kukinoga kwa jinsi Ronaldo na Messi walivyokaa kwa urafiki sehemu moja, wakizungumza na kucheka, kabla ya Ronaldo kumwalika hasimu wake huyo wa miaka mingi kwa mlo wa jioni.

Van Dijk (28) alikuwa akiwania tuzo hiyo na nyota hao wawili. Huyu ni mlinzi wa kwanza kupata tuzo hiyo iliyoanza msimu wa 2010/11. Messi na Ronaldo walitwaa tuzo tano kati ya zile nane za mwanzo miongoni mwao, wengine waliochukua wakiwa ni Andres Iniesta (2012), Franck Ribery (2013) na Luka Modric (2018) wakikamilisha orodha hiyo.

Amekuwa mwanga kwa Liverpool tangu ajiunge nao Januari mwaka jana kutoka Southampton, akivunja rekodi ya mauzo ghali ya beki duniani – pauni milioni 75. Mchezaji huyu wa kimataifa wa Uholanzi amekuwa na mchango mkubwa sana kwa timu Ulaya na nyumbani, akiwasukuma Liverpool kukaribia kutwaa ubingwa ambao hatimaye ulikwenda kwa Manchester City.

Alibaki kuwa beki ghali zaidi duniani hadi kiangazi cha mwaka huu pale Manchester United walipomnunua Harry Maguire kutoka Leicester kwa pauni milioni 80.

“Naona fahari sana kupata tuzo hii. Hii si yangu bali kwa wote walionisaidia kufika hapa. Nawashukuru wachezaji wenzangu, kwani bila wao nisingeweza kupata kile nilichopata. Barabara imekuwa ndefu na ni sehemu ya safari yangu,” akasema Van Dijk.

Mtaalamu wa soka wa Hispania, Guillem Balague anasema kwamba Van Dijk anastahili tuzo hiyo kwani amekuwa ingizo la hewa mpya na safi kwa njia mbalimbali. Si tu kwa jinsi anavyocheza lakini pia anavyofanya mambo mengine. Akasema kwamba Mholanzi huyo ni kiongozi ambaye hapayuki, akimalizia kwamba ni beki wa kati asiyehitaji sana kufanya makabiliano.

Mtaliano mtaalamu wa soka, Mina Rzouki anasema hakuna ubishi hata kidogo juu ya nani alistahili. Anasema walinzi walikuwa, kwa kitambo, wakisaidia timu zao sana kushinda lakini hawakuwa wakitambulika wala kupata tuzo.

“Van Dijk ameiboresha Liverpool kwa namna nyingi sana na uhakika wake uliwapa jukwaa la kuchea soka ya kushambulia. Ni imara sana pale nyuma, akibadilisha kabisa ngome ya Liverpool iliyokuwa mbovu mno, ikiruhusu mabao mengi. Liverpool wameng’aa muda mwingi kwa sababu yake,’ akasema Rzouki.

Mtaalamu mwingine wa soka wa Ujerumani, Raphael Honigstein ana haya ya kusema: “Van Dijk amestahili kwa sababu yeye ndiye nembo ya timu. Ni nahodha asiyevaa kitambaa kile. Ndiye kiongozi na jamaa mwenye utu. Alikuwa mmoja wa wachezaji mahiri kabisa kwenye soka ya Ulaya.”

Katika hafla hiyo, mchezaji wa zamani wa Manchester United, Eric Cantona alipewa Tuzo ya Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya, kutokana na mema aliyofanya tangu kustaafu soka, ikiwa ni pamoja na kuwajali masikini na wasiojiweza, akiwatetea kupata haki sawa na wengine.

Kivutio kikubwa kilikuwa Ronaldo na Messi waliokaa mkabala, wakitaniana na kucheka. Walikuwa mahasimu wakubwa nchini Hispania, Ronaldo akiwa na Real Madrid kabla ya kuhamia Juventus majuzi huku Messi akitamba na Barcelona.

Ronaldo alisema Messi ni rafiki yake, wamepambana huko Hispania. “Tumekuwa pamoja kwa miaka 15. Sijui iwapo hiyo ilishatokea kabla – jamaa wale wale wawili kwenye jukwaa muda wote. Ni wazi, tuna uhusiano mzuri. Hatujapata kula chakula cha jioni pamoja, lakini nadhani itatokea baadaye. Tulikuwa na ile vita Hispania. Nilimsukuma naye akanisukuma pia, kwa hiyo ni vizuri kuwa sehemu ya historia ya soka,” akasema Ronaldo.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version