*Mbeya City waingia tatu bora
*Oljoro, Ashanti, Mgambo hoi
Wekundu wa Msimbazi, Simba wanaendelea na uongozi wa Ligi Kuu ya Tanzania, wakifuatiwa na Azam wana ‘Lambalamba’.
Simba walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Prisons ya Mbeya jijini Dar es Salaam Jumamosi hii na kujiweka vyema kileleni.
Watani zao wa jadi, Yanga, nao walipata ushindi wa kihistoria katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera, ikiwa ni mara ya kwanza katika muda mrefu.
Ilikuwa kawaida kwa Yanga ama kupoteza mechi au kutoka sare mjini Bukoba, lakini safari hii waligangamala, na walikuwa Mrisho Ngasa na Hamis Kiiza waliowazalisha wakata miwa hao.
Yanga walikaa katika nafasi ya pili kwa saa karibu 24 kabla ya Azam kuwashusha kutokana na ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya wanajeshi wa JKT Ruvu kwenye uwanja wa Chamazi.
Azam sasa wamefikisha pointi 17 baada ya kushuka uwanjani mara tisa, na hiyo ni pointi moja tu nyuma ya Simba na mbili mbele ya Yanga.
Mabao ya Azam katika mechi yao ya Jumapili jioni yalifungwa na John Bocco, Erasto Nyoni na Salum Abubakar.
Azam wanafundishwa na Mwingereza Stewart Hall ambaye kabla ya mechi alikamia kwamba lazima vijana wake waibuke na ushindi.
Yanga sasa wanashika nafasi ya nne nyuma ya Simba, Azam na Mbeya City. Hata hivyo, Azam na Mbeya City wamecheza mechi moja zaidi ya Simba na Yanga.
Timu za JKT Oljoro, Ashanti United na Mgambo JKT zipo katika nafasi tatu za mwisho na hivyo zinatakiwa kujifua zaidi ili kuweka hai matumaini ya walau kubaki katika ligi kuu msimu ujao.