Macho na masikio ya maelfu ya mashabiki wa soka nchini leo yataelekezwa kwenye uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara kati ya vigogo vya soka hapa nchini Simba na Yanga.
Huo utakuwa ni mchezo wa pili kwa vigogo hivyo kukutana ndani ya mwaka huu, ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni Aprili 19 katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja huo na timu hizo kwenda sare ya 2-2, ambapo Yanga ilikuwa na jukumu la kusawazisha.
Mchezo wa leo utakuwa na umuhimu mkubwa kwa Yanga kutokana na ukweli ina changamoto kadhaa za kukabiliana nazo.
Kocha wao mpya, Kostadin Papic aliyechukua mikoba kutoka kwa Dusan Kondic atakuwa anakalia benchi la timu hiyo kwa mara ya kwanza wiki tatu zilizopita.
Pia Yanga yenye pointi 18 itakuwa na kibarua cha kupunguza kasi ya Simba, ambayo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 27 baada ya kushinda mechi zake tisa za mwanzo.
Kutokana na ukweli kuwa ikipoteza mchezo huo ina maana itazidi kutoa mwanya kwa Simba kuzidi kupaa katika msimamo wa ligi hiyo. Yanga itakuwa fursa kwao kuendeleza ubabe wa kuifunga Simba kwa mara ya pili kwenye uwanja huo kama ilivyofanya katika raundi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu uliopita, ambako Yanga ilishinda bao 1-0, Oktoba 26,2008.
Katika mchezo huo, Simba itakuwa na kazi moja tu ya kuhakikisha wanaendeleza wimbi la ushindi kwenye michezo yake ya ligi pamoja na kutaka kuweka rekodi mpya ya kushinda michezo 10 mfululizo.
Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Yanga, Kostadin Papic alisema kuwa mara baada ya kukirekebisha kikosi chake ana matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo.
Kwa upande wake, kocha wa Simba, Patrick Phiri aliweka wazi kuwa anachohitaji ni pointi tatu kutoka kwa Yanga na uhakika wa kuzipata pointi hizo anao.
Wakati huo huo, washindi saba kati ya kumi, wamekabidhiwa tiketi zao walioahidiwa zitakazowawezesha kushuhudia pambano hilo.
Washindi hao wapata tiketi hizo, baada ya kujibu vema maswali yaliyoulizwa kwenye kipindi cha Yaliyomo yamo, kinachoendeshwa na kituo Redio One Stereo.
Hata hivyo washindi watatu walishindwa kupata tiketi zao kwa sababu wapo mikoani.
Washindi hao walikabidhiwa zawadi hizo na Mkurugenzi wa Redio One, Deogratius Rweyunga.
Walikabidhiwa zawadi hizo kwenye ofisi za Redio hiyo iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam ni Sulaka Juma, Miraji Issa, Suleiman Mushi, Enock Mathias, Isaya Kirumbi, Kwande Ismail na Adam Chiligati.