Menu
in ,

Ni shangwe za mtoko, mapato na maendeleo ya soka 

Yanga Vs Simba

Yanga Vs Simba

Tamasha la Simba limepita mwaka huu, ambapo lilifanyika Septemba 19 kutokana na kuchelewa  kumalizika Ligi Kuu Tanzania. Tamasha hilo lilitanguliwa na lile la Yanga maarufu kama Wiki  ya Mwananchi. Kwa upande wao Azam FC hawakufanya tamasha lao la Azam Festival kutokana  na kubanwa na ratiba ya mashindano ya kimataifa, hivyo wakaenda zao Zambia kujiandaa kwa  msimu mpya. 

Katika historia ya soka nchini miaka ya nyuma hapakuwepo tamasha la michezo la klabu  kongwe za Simba na Yanga, wala la Azam Festival. Lakini chini ya uomgozi wa Hassan Dalali,  Simba walianzisha tamasha lao maarufu la Simba Day mnamo mwaka 2009.  

Ndipo watani wao wa jadi Yanga nao walikuja na Yanga Day ambayo sasa ni maarufu kama  ‘Wiki ya Mwananchi.’ Baada ya matamasha ya Simba na Yanga kuna jingine la mabwanyenye  wa Chamazi, Azam fc liitwalo Azam Festival. Tamasha kama hilo pia linafanyika jijini Mbeya  ambako likikutanisha timu zote za mkoa huo, Mbeya City, Mbeya Kwanza,Ihefu,Tanzania  Prisons na nyingi za madaraja ya chini. 

MOTISHA KWA MASHABIKI 

Hili ni jambo la kwanza. Matamasha hayo yanawapa nafasi washabiki kupata burudani kutoka  kwa timu zao. Washabiki kutoka mikoa mbalimbali hufanya safari kuelekea Dar es salaam kwa  minajili ya kushuhudia timu zao.  

Mashabiki wanatumia matmasha hayo kama sehemu ya mtoko wao, kama vile kwenda disko au  sehemu za burudani. Kwahiyo mashabiki huwa karibu zaidi na timu zao na kuongeza bondi kati  yao.  

MAPATO YA TIMU 

Matamasha yote mawili Simba Day na Wiki ya Mwananchi yameuzwa kwa Azam Tv. Kwamba  haki za maudhui ya matamasha hayo zimekuwa chanzo cha mapato kwa timu hizo mbili.  

Miaka ya nyuma hapakuwa na kitu kama hiki, badala timu zilikuwa zinajindaa na msimu mpya  kwa kucheza mechi za kirafiki pekee au kujiandaa na mazoezi mengine. Lakini sasa timu  zimetambua haki za maudhui yao ambayo yanavutia televisheni na redio kutoa fedha amabzo  zinasaidia timu hizo kufanyia shughuli mbalimbali. 

Uwanja wa Benjamin Mkapa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 unapotapika  mashabiki mfano 40,000 bado inawapa nafasi Simba na Yanga kuvuna mapato ya viingilio  ambayo n fedha zinazosaidia shughuli za timu. 

FURSA KWA WANAMUZIKI

Wanamuziki wamepata nafasi ya kutumbuiza katika matamasha ya Simba na Yanga. Kwa mfano  katika tamasha la Simba kulikuwa na wanaumiziki kama vile Profesa Jay,Mpoki,Meja Kunte,Joh  Makini,Lord Eyes,Mario,Mkojani na Tundaman.  

Matamasha yaliyopita tumeshuhudia ushindani wa Diamond Platinumz aliyetumbuiza tamasha la  Simba mwaka 2020 na Harmonize aliyetumbuiza Wiki ya Mwananchi mwaka 2020 pia.  Wanamuziki hao wanapata fursa ya kujiingizia kipato sababu ya matamasha haya, kwahiyo ni  sehemu ya fursa kwao kukonga nyoyo za mashabiki wa soka na wale wa muziki. 

NYOTA WAPYA 

Washabiki wa timu wana kawaida ya kutaka kuwaona nyota wao wapya kwa mara ya kwanza  kabla ya msimu mpya wa 2021-2022. Simba wametambulisha nyota wao kama vile Duncan  Nyoni,Peter Banda,Kibu Dennis,Pape Ousmanne Sakho,Sadio Kanoute,Israel Mwenda, Abdulswamad Kassim, Yusuf Mhilu,Henock Inonga,Ahmed Teru, Jeremiah Kisubi.  

Kwa upande wa Yanga kulikuwa na Djuma Shaban,Yusuf Athuman,Jesus Muloko, Djigui  Diarra,Yannick Bangala,Herieter Makambo, Khalid Aucho,Fiston Mayele, 

VIONGOZI KIVUTIO 

Matamasha hayo yamewavutia viongozi mbalimbali wa kisiasa ambao wamekuwa wakijitokeza  mara nyingi kushiriki. Hii ina maana kubwa katika maendeleo ya mchezo huo angalau kwa  mazingira ya Tanzania ambayo bado mafanikio yake ni haba.  

Kujitokeza viongozi wa kisiasa kama mawaziri,wakuu wa mikoa,wakuu wa wilaya, wanasiasa na  wengine ni chachu ya kuongeza mvuto wa matamasha yenyewe. 

Mfano tamasha la Simba Day mgeni mwalikwa alikuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job  Ndugai, huku viongozi wengine akiwemo Mkuu wa wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo  akinogesha tamasha hilo. 

THAMANI IMEVUKA BODA 

Chama cha soka nchini DRC kililazimika kufanya marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu nchini  humo ili kuwapa nafasi TP Mazembe washiriki mchezo wa tamasha la Simba Day.  

Septemba 19 TP Mazembe walikuwa na ratiba ya kucheza mchezowa Ligi Kuu, lakini chama  cha soka DRC kiliamua kuwapa nafasi kusafiri hadi Tanzania kushiriki sherehe za Simba ikiwa  na maana ya kuwapa thamani kubwa waandaaji na soka kwa ujumla.  

Ni uamuzi unaoonesha kuwa thamani ya Simba Day au mengine kama Wiki ya Mwananchi au  Azam Festival matamasha hayo yamepanda thamani na kuwavutia wageni. Haitashangaza  kushuhudia kuuzwa kwa haki za maudhui ya televisheni kwa nchi jirani au inakotoka timu  mwalikwa.

WACHEZAJI CHIPIKIZI,WANAWAKE 

Katika matamasha haya tumeona timu za vijana nazo zikipewa nafasi ya kuonesha umahiri wao,  kama ilivyo kwa timu za wanawake. Vijana wa Simba chini ya miaka 20 ilipepetana na JKU ya  Zanzibar na kuibuka mshindi kwa bao 1-0. Vijana hao walionesha umahiri na kuwafurahisha  mashabiki wa Simba. Vilevile Simba Queens walishiriki tamasha hilo  

KUONGEZEKA MVUTO 

Matamasha ya timu za soka yanachangia ongezeko la mvuto miongoni mwa wadau,washabiki na  baadhi ya kampuni za udhamini. Kama ambavyo kampuni za kubeti zinavyochukua hatamu  katika soka ndivyo ambavyo baadhi zimeanza kuingia katika soko la michezo nchini Tanzania.  

Hilo lina maana kuwa klabu zinatakiwa kuongeza hamasa kwa mashabiki ambao ndio chachu ya  kupatikana wadhamini wengi katika mchezo wa soka na kuuthaminisha zaidi. 

TAMASHA NA JAMII 

Katika hatua nyingine matamasha hayo yameonesha sura nyingi ya kuhudumia jamii. Yanga  walianza wiki ya mwananchi visiwani Zanzibar kwa kushiriki kutoa huduma kwa jamii.  Mashabiki wa Simba tawi la Mafinga mkoani Iringa walikabidhi msaada wa magodoro na vitu  vingine kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Makalala ikiwa ni  mchango wao kwa jamii. 

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version