Hadi sasa ukitazama kikosi cha Manchester City utagundua ndicho chenye wachezaji majembe zaidi kuliko timu zingine. Ni kikosi ambacho kila kocha angetamani kuwa nacho, lakini kina changamoto ya kutokuwa na historia yoyote kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Historia na hadhi ya timu vina nafasi kubwa ya kuwashawishi wachezaji kujiunga na timu hizo. Pengine ofay a fedha inatangulizwa mbele lakini hadhi na historia ya timu ni vitu muhimu kwa wachezaji karibu wote duniani.
Manchester City katika historia yao wamefanikiwa kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Nje ya hapo hawajawahi kulitwaa kombe hilo, kwahiyo wao sio daraja moja la watemi kama Nottingham Forest ambayo imewahi kulitwaa taji hilo. Manchester City inaweza kuwa daraja la Leeds United kwa kuchachafya kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya lakini inakuwa haina historia yoyote ya kutwaa taji hilo.
Hata hivyo hayo hayamfanyi kocha Pep Guardiola kushindwa kujenga kikosi cha kushindana na yeyote barani Ulaya. Kikosi chake kimejengwa katika mitazamo yake na anahitaji majembe ya nguvu ambayo yanavipaji na nakshi zina aina yake kwenye kandanda.
Pep Guardiola hivi karibu alieleza jambo ambalo ndilo hoja yangu ya leo. Kocha huyo aliulizwa swali juu ya mafanikio ya timu yake katika soka la Uingereza. Jibu lake lilikuwa rahisi sana, kwamba ana bahati Man City wana fedha nyingi ambazo zinawapa nafasi ya kununua wachezaji wa daraja la juu.
Guardiola alizungumzia hayo baada ya kushuhudia timu yake Manchester City ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Borussia Monchengladbach na kumaliza michezo 19 kwa ushindi. Ukitazama kikosi chao kinaonekana wazi kimepania kulitwaa taji la Ligi Kuu Uingereza msimu hii, na huenda likawa taji la tatu kwa kocha huyo ndani ya miaka minne.
Hadi sasa Man City wanatajwa kuwa timu ambayo inaweza kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Man City wanatajwa pia huenda wakalitwaa taji la Carabao msimu huu, huku wakiwa kwenye mawindo ya kulitwaa taji la FA kwa mara ya nne ambako wamefika hatua ya robo fainali.
Pep Guardiola amekiri kuwa timu yake imebahatika kuwa chini ya umiliki wa mtu mwenye uwezo mkubwa wa fedha na kununua wachezai anaowahitaji.
Katika kikosi kilichoanza mchezo dhidi ya Borussia kilikuwa ghali sana. Wachezaji wake walinunuliwa kwa fedha nyingi na ambao wamekuwa wakiipa Man City jeuri ya kupambana na timu zozote barani Ulaya.
Ederson (alinunuliwa kwa pauni milioni 35); Walker (Pauni milioni 54), Ruben Dias (Pauni milioni 64), Laporte (Pauni Milioni 57), Joao Cancelo (Pauni milioni 55); Rodri (Pauni milioni 65), Gundogan (Pauni milioni 21), Sterling (Pauni milioni 49), Bernardo Silva (Pauni milioni 43), Foden (Akademi), Gabriel Jesus (Pauni milioni 27). Gharama ya kikosi hicho ni jumla ya pauni milioni 470.
Na kufuatia ushindi wao dhidi ya Borussia Gladbach jumatano iliyopita kwenye Ligi ya Mbaingwa, Guardiola alisema hawezi kujigamba kuwa uwezo wake mkubwa wa kufundisha soka ndiyo chanzo cha mafanikio ya Man City, badala yake anasema utajiri wa fedha za wamiliki wa timu hiyo ndicho chanzo cha mafanikio wanayopata. Fedha za mafuta na gesi kutoka kwa wamiliki wa timu wanaoishi huko Abu Dhabi ndiyo kiini cha mafanikio ya Man City.
“Tuna fedha nyingi za kununua wachezaji wenye viwango vya juu. Ni kweli kwamba Man City na wachezaji wake ni wa kipekee. Uhusiano baina ya wachezaji wa kikosi hiki ni mkubwa na wanaishi katika uungwana wa hali ya juu. Kila mechi wanacheza kwa malengo ya kushinda tu, wao akili zao zipo kushinda hawajui mambo ya kufungwa fungwa,” alisema Guardiola baada ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya
Kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita Man City wametumia kiasi cha pauni bilioni 2 kununua wachezaji wa daraja la juu, pamoja na mmiliki wa timu hiyo Sheikh Manson amekuwa akiingiza fedha nyingi za kununua wachezaji pamoja na kulipa mishahara minono tangu aliponunua timu hiyo mwaka 2008.
Bernardo Silva na Gabriel Jesus, wote kwa pamoja walifunga mabao katika mchezo dhidi ya Borussia Monchengladbach, wamenunuliwa kwa fedha nyingi kipindi Guardiola akiwasili klabuni hapo.
Tangu Guardiola awe kocha wa Man City mwaka 2016 kumeshuhudiwa matanuzi makubwa sokoni baada ya kuwanunua wachezaji karibu pauni milioni 700. Kwa mfano Riyad Mahrez (alinunuliwa kwa pauni milioni 60), Bernardo Silva (pauni milioni 43), Leroy Sane (pauni milioni 37), Gabriel Jesus (pauni milioni 27), Ikkay Gundogan (pauni milioni 21) na Rodri (pauni milioni 65) kwa malengo ya kuboresha safu ya ushambuliaji
Lakini safu ya ulinzi ya Man City ni Ruben Dias pekee ndiye amenunuliwa kwa fedha nyingi, ambazo ni pauni milioni 64. Wengine ni Kyle Walker (pauni milioni 54), Aymeric Laporte (pauni milioni 57), Joao Cancelo (pauni milioni 55), Nathan Ake (pauni milioni 40), Benjamin Mendy (pauni milioni 52), John Stones (pauni milioni 47.5) na Danilo (pauni milioni 27) ambapo wote wamenunuliwa katika kipindi cha Gaurdiola.
Katika nafasi ya golikipa, Guardiola alitumia pauni milioni 35 kumnunua Ederson na Claudio Bravo kwa pauni milioni 17. Ni Bravo pekee ambaye hakupata mafanikio katika klabu ya Manchester City. Tunaweza kusema katika nafasi hiyo Guardiola alipata hasara kwa kumnunua Claudio Bravo pekee.
Ujio wa Ruben Dias, umeboresha ukuta wa Man City, ambapo ili kumpata beki huyo kisiki iliwalazimu kulipa pauni milioni 64. Kwa kiasi fulani hadi sasa beki huyo ameleta matumaini na kuifanya safu ya ulinzi ya Man City kuimarika zaidi.
Licha ya timu mbalimbali kuathiriwa kimapato kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona, kwa upande wa Man City hali imekuwa tofauti kwani hawaonekani kama wamekumbwa na mdororo wa fedha kama timu zingine ambao zimelazimika kupunguza kiwango cha mishahara ya wachezaji wake pamoja na kutonunua wachezaji wapya. Sasa wanatawala Ligi kuu England na wanaelekea kutamba kimataifa.
Hadi sasa wanaongoza Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi 10 huku zikiwa zimebaki mechi 13 kumalizika ligi hiyo. Pia wapo kwenye mawindo baada ya kutinga fainali ya kombe la Carabao, ambapo wanatarajiwa kumenyana na Tottenham Hotspurs mwezi Aprili mwaka huu.
Ushindi wao wa mabao 2-0 jumatano dhidi ya Gladbach umewaweka mguu moja ndani kutinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa. Hadi sasa wana uhakika kuwa watafuzu kwa hatua hiyo na huenda wakalitwaa kwa sababu vigogo vya soka kama Bayern Munich, Real Madrid na Barcelona wamepepesuka. Tishio pekee litakuwa PSG ambao wanakuja kwa kasi kwenye michuano hiyo.