*Man United walala kwa Chelsea
Arsenal watacheza fainali ya Kombe la FA na Aston Villa kwenye dimba la Wembley mwezi ujao baada ya kufuzu kwenye hatua ya nusu fainali.
Washika Bunduki wa London walifuzu baada ya kuwafunga Reading 2-1 Jumamosi wakati Villa waliwafunga Liverpool kwa idadi hiyo hiyo ya mabao.
Alexis Sanchez alikuwa shujaa Jumamosi kwa kufunga mabao yote mawili wakati kwa Villa wafungaji walikuwa Christian Benteke na Fabian Delph.
Mchezaji ambaye amekuwa akiwaokoa Liver kwenye michuano hii, Phillipe Countinho ndiye pia aliwafungia bao la kufutia machozi wakati kwa upande wa Reading alikuwa Garath McCleary aliyepeleka mechi hadi dakika 120.
LIGI KUU England
Katika Ligi Kuu ya England (EPL) Chelsea wamewaliza Manchester United kwa bao 1-0 lililofungwa na Eden Hazard katika dakika ya 38.
Kwa ushindi huo Chelsea wamekwenda pointi 10 mbele ya walio nafasi ya pili ambao ni Arsenal. Katika matokeo mengine Crystal Palace walilala 2-0 mbele ya West Bromwich Albion, Everton wakawalaza Burnley 1-0.
Mechi nyingine ilishuhudia maajabu ya Leicester kuwafunga Swansea 2-0 na Stoke wakawapiga Soithampton 2-1.
Mabingwa watetezi Manchester City wamefarijika kwa kuwafunga West Ham 2-0 wakati Newcastle wamelala 3-1 kwa Tottenham Hotspur.
Matokeo hayo yamewafanya Chelsea kuwa na pointi 76 kileleni, Arsenal 66, Manchester United 65, Man City 64 huku Liverpool wakiwa na 57 sawa na Spurs.
Southampton wanazo pointi 56, Swansea 47, Stoke 46 na West Ham wanafunga 10 bora kwa pointi zao 43.
Mkiani wamebaki Burnley wenye pointi 26 sawa na Queen Park Rangers (QPR) huku Leicester na Hull wakiwa na pointi 28 kila mmoja.